Connect with us

Kitaifa

Askari polisi mbaroni madai mauaji ya raia

Geita/Tarime. Matukio mawili ya mauaji ya raia yakihusisha askari wa Jeshi la Polisi, yamehitimisha mwezi uliopita vibaya, huku polisi PC 4489 Kaluletela akiwekwa mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya Ng’ondi Marwa (22), mkazi wa Mtaa wa Regoryo.

Mauaji hayo ya raia wawili yalitokea wilayani Tarime, Mkoa wa Mara na Chato, Geita kwa nyakati tofauti.

Mbali na matukio hayo, jingine ni la kuuawa mlinzi wa Msikiti wa Shree Hindu Mandal Temple uliopo mjini Kahama, Mkoa wa Shinyanga, Bakari Karasani (46) kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana kisha mwili wake kuwekwa nyuma ya msikiti.

Katika tukio lililotokea wilayani Chato, Enos Misalaba (32) alipoteza maisha akiwa Kituo cha Afya Mganza kwa madai ya kupigwa na askari, hali iliyosababisha vurugu hadi kuchomwa moto kwa kituo cha polisi.

Mwili wa Misalaba ulizikwa juzi jioni baada ya kukwama ukiwa tayari makaburini, kutokana na wananchi kupinga historia ya marehemu kueleza alifariki dunia kutokana na kuumwa kifua.

Wananchi walipinga na kuamua kubeba jeneza na kulipeleka kituo cha polisi ili wapate majibu sahihi ya nini kimemuua kijana huyo aliyekuwa mzima wakati anakamatwa, Machi 27 mwaka huu akituhumiwa kuiba betri ya gari.

Hata hivyo, kijana huyo alifariki dunia Machi 28 mwaka huu.

Kutokana na wananchi kuupeleka mwili huo kituoni, kuliibuka vurugu na kusababisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi na watu wanne walijeruhiwa huku kituo kikichomwa moto.

Mazishi ya kijana huyo aliyeacha mtoto mmoja yalifanyika juzi jioni badala ya asubuhi kama ilivyokuwa imepangwa baada ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi upya ili kujiridhisha na sababu za kifo chake.

Mkuu wa Mkoa wa Geita (RC), Martine Shigella aliyeongoza mazishi hayo alisema wamelazimika kuwapeleka wataalamu wenye uzoefu kutoka nje ya mkoa kuchunguza upya ili kujiridhisha chanjo cha kifo ili hatua za kisheria zichukuliwe.

“Kulikuwa na sintofahamu kuwa ndugu yenu ameuawa na ndiyo maana mlirudisha mwili kituoni na ili sisi tujiridhishe na malalamiko ya wananchi kama yana ukweli, tulisema lazima tufanye uchunguzi mara ya pili ili kama ni kweli tuweze kuchukua hatua kwa yule aliyehusika na kitendo hicho,” alisema Shigella

“Tumezingatia hisia za wananchi na kuamua kuzitafsiri kitaalamu na kuona wanachosema na taarifa ya mwanzo kama vinafanana. Tuliagiza wataalamu kutoka nje ya mkoa wenye utaalamu wa kufanya uchunguzi na madaktari wengine wametoka Dar es Salaam ili kujiridhisha kama walichoona kinafanana na tulichoambiwa au kinatofautiana.”

Shigella alisema uchunguzi huo umehusisha ndugu wa marehemu na kusisitiza Serikali haikubali uonevu wowote kwa raia wake na kwamba inamjali mtu bila kujali cheo, hadhi wala uwezo na kuwa inaheshimu na kujali uhai na utu wa mtu.

Waliochoma moto kituo kukiona

Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama alitumia fursa hiyo kulaani kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuchoma kituo cha polisi.

Shigella alisema kitendo hicho hakikubaliki kwa kuwa kinahatarisha usalama wa watu na kutaka wananchi watoe taarifa kwenye mamlaka pindi wanapoona jambo halipo sawa kwenye jamii.

“Tujenge misingi ya utawala bora na wa sheria, mnapokuwa hamjaridhika na jambo msijichukulie sheria mkononi. Tuwasihi vijana jambo lililofanyika halikubaliki, silaha zikiachwa hovyo zitakuja kusumbua mtaani, niwaombe lililotokea lisijirudie tena,” alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kufuatia vurugu zilizotokea baadhi ya watu waliotajwa kuwa chanzo, wakiwamo polisi wa kituo hicho wamekamatwa na wanashikiliwa kwa taratibu nyingine za kisheria.

Shigella alisema Serikali haimlindi mtu au kumtetea anayefanya mambo ya konakona na ili kumaliza tatizo katika kata hiyo, anaunda timu itakayohusisha vyombo vya usalama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wataalamu kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa ili kukomesha tabia ya watu kuonewa na kupoteza maisha.

“Nitaleta kamati na tume ya uchunguzi isiyokuwa na chombo kimoja, nitaleta yenye vyombo vyote vya usalama, watakuwepo Jeshi la Wananchi, polisi, usalama wa Taifa, Takukuru na ofisini kwangu ili muwape ushirikiano tuweze kukomesha tabia hii ya watu kuonewa,” alieleza Shigella, ambaye tangu aingie mkoani humo miezi sita iliyopita hajawahi kufika kwenye kata hiyo kuzungumza na wananchi.

Mke wa marehemu

Regina Mathias, ambaye ni mke wa marehemu Enos, aliyeachwa na mtoto mmoja alisema Machi 27, mchana mumewe alikuja na askari polisi, mgambo na mtu aliyedai kuibiwa betri na kufanya upekuzi ndani kisha kuchukua betri wanayoitumia na nyingine mbovu pamoja na tanki.

“Walikuja na gari, ndani alikuwamo yule aliyemuuzia mume wangu betri lakini yeye hakushushwa, hawa askari waliingia wakavuruga ndani, walikuwa wanampiga mume wangu wakidai ni mwizi na mume wangu aliniambia nisimfuate nikae atarudi kwa kuwa hajaiba,” alisema Regina.

Alisema siku iliyofuata waliambatana na mama mkwe kwenda kituoni na walipofika hawakumkuta, walielezwa amepelekwa hospitali usiku na walipokwenda Kituo cha Afya Mganza walimkuta amelala huku ana pingu mkononi amevimba mwili na hawezi kuongea.

Alisema alikuwa akitoa sauti ya chini ya kukoroma na baada ya dakika chache alipoteza maisha.

“Nilimshika kifuani nikaona mapigo ya moyo hayapigi na wala hapumui, nikamuita shemeji aje amuone, alivyomwangalia akasema, shemeji huyu ameshakufa, ndio mama akaingia akasema huyu mwanangu kuna mtu kweli, nesi akajibu ameshakufa.”

Polisi mbaroni kwa mauaji

Katika tukio lingine lililotokea Kijiji cha Kubiterere wilayani Tarime, polisi PC 4489 Kaluletela anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za mauaji ya Ng’ondi Marwa (22), mkazi wa Mtaa wa Regoryo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime-Rorya, Godfrey Sarakikya alikiri kutokea tukio hilo juzi kwa askari wake wa Kituo cha Polisi Sirari kumfyatulia risasi kijana huyo ambaye ni dereva bodaboda.

“Ni kwamba askari huyo kwa uzembe wake mwenyewe na bila uhalali wowote, alimfyatulia risasi raia huyo asiyekuwa na hatia na kumjeruhi kwenye paja la mguu wa kulia,” alisema kamanda.

Alisema kijana huyo alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, “alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu. Uchungu wa awali umebaini marehemu alifariki kutokana na kupoteza damu nyingi.

“Niseme kwamba, huyu ni askari polisi aliyefunzwa na kufuzu mafunzo yote ya polisi, yakiwamo matumizi sahihi ya silaha, hivyo alichokifanya ni kinyume na taratibu na sheria za nchi na anastahili kuwajibika kwa hilo,” alisema Kamanda Sarakikya.

Mwili wa Ng’ondi umehifadhiwa katika Hospitali ya Tarime ukisubiuri uchunguzi wa kitabibu.

Familia yagoma

Wakati uchunguzi huo ukisubiriwa, familia ya kijana huyo ilisema haiko tayari kuuchukua kwa maziko hadi Jeshi la Polisi litakapotoa utaratibu wa namna litakavyogharamia msiba huo pamoja na fidia.

Jana, katika uwanja wa chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo, baba mzazi wa marehemu, Marwa Masiaga alisema familia haina uwezo wa kugharamia msiba huo.

“Marehemu ameacha mjane na mtoto, tunataka kujua nini hatima ya familia yake, familia yangu ni ya uwezo wa chini, hatutaweza kugharamia huu msiba, tunaomba Serikali kwa sababu mwanangu ameuawa na polisi,” alisema baba mzazi wa Ng’ondi.

Akizungumzia gharama anazoeleza baba mzazi wa marehemu, Kamanda Sarakikya alisema tukio hilo limefanywa na mtu binafsi na sio Jeshi la Polisi, kwa kuwa askari huyo alimfyatulia Ng’ondi risasi bila sababu za msingi.

Akieleza jinsi tukio lilivyotokea, baba marehemu alisema mwanaye aliuawa baada ya kuombwa rushwa na askari huyo ili amruhusu kupita na mifuko ya saruji.

Marwa alisema mtoto wake alifariki dunia baada ya kupigwa risasi mbili, moja kiunoni na nyingine kwenye paja la kulia.

Alisema kabla ya tukio hilo, Ng’ondi ambaye ni mwendesha bodaboda alikamatwa na askari wawili akiwa amepakia mifuko mitano ya saruji.

Marwa alisema askari hao walimuomba pesa ili waweze kumruhusu kupita na mzigo huo alionunua nchi jirani ya Kenya.

“Mtoto wangu huwa anachukua oda za watu wanaotaka saruji kisha anaenda Kenya kununua kwa bei ya jumla, akishaleta wanamlipa, hiyo ndiyo biashara aliyokuwa akifanya,” alisema Marwa.

“Wapo vijana wengi tu wanaofanya biashara kama hiyo na mara zote wakifika pale Kubiterere kuna askari huwa wanawaomba hela, wakishawapa wanaruhusiwa kupita. Nimeambiwa aliombwa Sh300,000 na yeye hakuwa nazo, waliposhindwana akaamua kuondoka na kuacha saruji pale, ndipo askari mmoja akamfyatulia risasi,” alisema Marwa.

Katibu wa Umoja wa Bodaboda Tarime, Richard Christopher pamoja na kulishukuru Jeshi la Polisi kukiri askari huyo kuhusika na mauaji hayo, ameliomba kujitathmini juu ya utendaji wake.

“Polisi wabadilike, sisi ni wananchi wa kawaida wala sio majambazi, iweje askari unaamua kumuua mtu kama mnyama, wakati wewe una bunduki yeye hana silaha yoyote,” alisema Christopher.

Msikiti wavamiwa, mlinzi achinjwa

Unaweza kusema Machi imehitimishwa kwa tukio la mlinzi wa Msikiti wa Shree Hindu Mandal Temple uliopo mjini Kahama, Mkoa wa Shinyanga, Bakari Karasani (46) kuchinjwa na watu wasiojulikana.

Tukio hilo linaloacha maswali mengi, linatokea ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu kuripotiwa kwa kufuru nyingine kufanywa katika Kanisa Kuu la Jimbo la Geita, usiku wa kuamkia Februari 26, mwaka huu baada ya kijana mmoja kuvamia kanisa hilo na kufanya uharibifu mkubwa wa mali, ikiwemo eneo la Altare.

Hata hivyo, Machi 6, Elpidius Edward (22), mkazi wa Mtaa wa Katundu Wilaya ya Geita anayedaiwa kuvamia na kufanya uharibifu katika kanisa hilo alikwishafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Tukio la Msikiti wa Shree kuvamiwa lilitokea usiku wa kuamkia Machi 30 mwaka huu na inadaiwa wakati mlinzi huyo akiwa kazini ndipo alivamiwa na watu hao na kumchinja kisha kuvunja sanamu waliyokuwa wakiitumia kuabudia.

Kufuatia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme alifika kwenye msikiti huo kuona uharibifu uliofanyika na kulaani kitendo hicho.

“Mlinzi aliyechinjwa alikuwa na miaka zaidi ya 10 akifanya ulinzi kwa uaminifu kwenye msikiti huu, lakini amekuja kuuawa kikatili na watu wasiojulikana na pia wameharibu vitu vya thamani ndani ya msikiti,” alisema Mndeme.

Mkuu huyo wa mkoa alisema Serikali inasikitishwa na tukio hilo na inafuatilia watu waliotekeleza ili sheria ichukue mkondo wake huku akiahidi kulipa gharama zilizojitokeza.

Msimamizi wa msikiti huo, Niraj Kakad alisema walipewa taarifa ya mlinzi wao kuuawa na mwili wake kuwekwa nyuma ya msikiti.

Alisema vitu vilivyoharibiwa ndani ya msikiti thamani yake bado haijajulikana.

“Baada ya tukio tumekutana hapa tunajadiliana, tumezunguka nyuma tumemkuta marehemu na ndani kote kumevurugwa, tumeenda polisi kuona namna ya kutusaidia,” alisema Kakad.

Pia, alisema vitu walivyoharibu ni sanamu ya kuabudia na fedha ya sadaka, huku akiomba msaada kwa Serikali kuona namna ya kuwakaba waliofanya tukio hilo.

Mwili wa Bakari umesafirishwa kwenda mkoani Tanga kwa maziko.

Imeandikwa na Rehema Matowo (Geita), Beldina Nyakeke (Tarime) na Stella Ibengwe (Shinyanga).

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi