Kitaifa
Wakazi Magomeni Kota waendelea kususia bei ya nyumba
Dar es Salaam. Kaya 644 zimeendelea kususia bei za nyumba za Magomeni Kota zikidai haziendani na hali ya uchumi wao, licha ya Serikali kuzishusha na zikiwa ndogo kulinganisha na hali ya soko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa Februari 5 mwaka huu na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkataba wa kulipia nyumba hizo ulitakiwa kuanza kulipiwa kidogokidogo kuanzia Februari 8 mwaka huu, lakini hadi sasa hakuna kaya iliyoanza kufanya hivyo.
Februari mwaka huu, akiwa jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa TBA, Daudi Kandoro alisema awali nyumba zilikuwa zikiuzwa kwa Sh74 milioni kwa chumba na sebule na Sh86 milioni kwa vyumba viwili na sebule, lakini kuzingatia vipato vya kaya hizo walipunguza kiwango hicho hadi Sh48 milioni na Sh56 milioni.
Mwenyekiti wa Wakazi hao wa Magomeni, George Abel alisema wamekubaliana kutokuanza kulipia nyumba hizo kwa kuwa bei walizotajiwa ni kubwa. “Tunamuomba Rais Samia aingilie kati, bei iliyopendekezwa na Serikali awali ilikuwa ni Sh12 milioni hadi Sh17 milioni, lakini tunashangaa wamekuja na bei zaidi ikiwa ni tofauti na mapendekezo ya awali,” alisema Abel, licha ya kuwa kwa kiwango hicho cha pesa huwezi kupata nyumba ya viwango hivyo Magomeni.
Alipoulizwa suala hilo, Kaimu Mkurugenzi kutoka idara ya miliki TBA, Said Mndeme alisema mkataba wa kununua nyumba ni kati ya mtu na taasisi, itakuwa sio sawa kuweka wazi. Mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba, 2016 na kukamilika mwaka jana, ikiwa ni ahadi ya Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli kwa wananchi 644 waliokuwa wakiishi kwenye nyumba hizo ambao awali walihamishwa kupisha maboresho, ikiwamo kujenga maghorofa.
Nyumba hizo zilivunjwa mwaka 2009 na wananchi waliahidiwa kukaa bure kwa miaka mitano na baadaye kuzinunua kwa bei nafuu.
Wakati wakazi hao wakilalamikia gharama iliyotajwa haiendani na uchumi wao, madalali wa miradi kama hiyo wanadai kulingana na skimu ya mfumo wa malipo waliyopewa bei hiyo ni rahisi, ikilinganishwa na uhalisia bei inayopatikana sokoni kwa sasa.
Wakala wa nyumba kutoka Kampuni ya My Dalali, Arusha, Robert Makule alisema kwa bei walizotajiwa ni rahisi kulingana na hali ya nyumba za sasa, isipokuwa bei halisi ya nyumba inabebwa na aina ya vitu vinavyopatikana kwenye majengo husika.
Alisema waliosusia wafanye utafiti kwenye miradi ya Serikali na watu binafsi ambayo inafanya vizuri sokoni. “Kuna watu wana miradi Kinondoni na bei za chini kwa chumba na sebule hadi Sh78 milioni na watu wanazishangilia wanaona bei rafiki,” alisema Makule
Wakala kutoka kampuni ya Makazi Bora Dar es Salaam. Tomu Bernard alisema bei walizotajiwa ni ndogo na iwapo Serikali itaweka sokoni nyumba za mradi huo wateja watachangamkia. “Eneo lile liko katikati ya mji na bei waliyotajiwa ni ndogo kulingana na soko lilivyo, kwani bei zinaanzia Sh200 milioni hadi Sh350 milioni,” alisema Bernad.
Alisema nyumba za mradi kama Victoria vyumba vitatu bei yake ni Sh250 milioni na mradi wa nyumba za Palm Village bei ni Sh350 milioni kwa vyumba vitatu.