Kitaifa
Majeruhi ajali ya mwendokasi aruhusiwa kurudi nyumbani
Dar es Salaam. Siku 38 baada ya matibabu kufuatia ajali ya basi la mwendokasi iliyotokea Februari 22 jijini Dar es Salaam hatimaye Osam Milanzi ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Mifupa (MOI) alikokuwa akipatiwa matibabu.
Milanzi ambaye alikuwa majeruhi pekee katika ajali hiyo ameruhusiwa baada ya afya yake kuimarika kufuatia matibabu ya huduma za kibingwa aliyopata katika kitengo cha dharura (EMD), ICU, HDU na wodi 2A .
Majeruhi huyu ambaye hakuwa sehemu ya abiria waliokuwa ndani basi alikumbwa na kadhia akiwa anapita nje ndipo basi hilo lilipomvamia na kumzoa.
Akizungumza na Mwananchi Meneja uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi amesema uamuzi huo ulifikiwa baada ya jopo la madaktari kujiridhisha kwamba afya yake inaweza kuendelea kuimarika akiwa nyumbani.
Amesema Milanzi alipokelewa MOI akiwa ameumia kichwa, mguu wa kushoto, mkono na bega upande wa kulia.
“Jopo la madaktari limemfanyia tathmini na kuona anaweza kuendelea na matibabu mengine akiwa nyumbani, akiwa na familia yake kuna uwezekano wa afya yake kuimarika kwa haraka zaidi akaweza kuendelea na shughuli zake.
“Anachotakiwa kufanya kwa sasa ni mazoezi tiba ambayo ataendelea nayo akiwa nyumbani, pia ataendelea na huduma kama mgonjwa wa nje na atarudi kliniki baada ya wiki mbili.