Kitaifa

Sababu vijana kukwepa kuoa

Dar es Salaam. Umefikia umri wa kuoa? Umewahi kwenda kwa wazazi wa mwenza wako kuanza taratibu za kufanikisha hilo? Walikueleza nini? Kipi kilikufurahisha na kipi kilikukera au kukukatisha tamaa?

Majibu ya maswali haya yanaakisi uhalisia wa wanayoyapitia vijana wengi wanapoanza mchakato wa kufunga ndoa kwa kupitia taratibu za kimila, hali inayotajwa kuchangia uwepo wa ndoa zisizo rasmi.

Vijana wanasema masharti ya baadhi ya wazazi wa waolewaji yanaweka mazingira magumu kwa wao kuoa na wengine huishia kuishi na kujenga familia bila ndoa kutokana gharama za mahari.

Hoja hiyo ya vijana inatajwa na wazee wa kimila kuwa inatokana na kumomonyoka kwa maadili kunakowafanya waone michakato na taratibu za ndoa ni gharama, lakini kila jambo lina taratibu zake katika jamii husika.

Mikasa ya ndoa

Johnson Mandela, mkazi wa Dar es Salaam, anasema ndoa ilimshinda kutokana na wingi wa masharti aliyopewa na wazazi wa mwenza wake.

Ingawa wawili hao wanaishi pamoja, anasema hawakuwahi kufunga ndoa kwa kuwa alishindwa kutimiza matakwa ya wakwe zake.

“Tulikwenda kujitambulisha, nikaambiwa nipeleke barua nikapeleka, ikajibiwa baada ya siku kadhaa, ndani yake ikaandikwa vigezo ninavyopaswa kutimiza,” anasema Mandela katika mahojiano maalumu na gazeti hili.

Mandela anasema miongoni mwa vigezo hivyo alivyopaswa kulipa mbali na mahari ni ng’ombe wawili dume na jike, mablanketi manne, mavazi ya babu na bibi na fedha ya walezi.

“Wakaniambia hivyo vyote natakiwa kuvithaminisha kwa fedha isipokuwa mablanketi tu, kwa hiyo nikatakiwa kupeleka Sh2.5 milioni nje ya mahari na mahari nilitajiwa Sh2 milioni, kwa hiyo jumla nilitakiwa kuwa na Sh4.5 milioni,” anasema Mandela.

Katika masharti hayo, anasema Sh2.5 milioni alitakiwa kuilipa yote na alipangiwa kufanya hivyo baada ya miezi miwili, huku mahari akitakiwa kulipa angalau asilimia 70 baada ya muda huo.

“Kwa kuwa naishi na mwenzangu bila wazazi kujua, tukasema tujipange mambo yakiwa sawa tutafanya, lakini huu ni mwaka wa tano sasa na tuna watoto wawili, kusingekuwa na masharti mengi kiasi hicho ningeshafunga ndoa,” anasema.

Yaliyomkuta Mandela hayatofautiani sana na Caroline Mihizi, anayeishi na mwenza wake mwaka wa tatu sasa, anasema alishindwa kulipwa faini ya kuzalishwa mtoto kabla ya kuolewa, jambo ambalo mila za baadhi ya makabila haziruhusu.

“Nilipata mimba kabla sijaolewa nikazaa, mwenzangu akasema twende nyumbani, tulipofika kwa wazazi wangu, pamoja na masharti mengine mwenzangu alitakiwa kulipa Sh3 milioni kama faini ya kunizalisha bila kunioa,” anasema Caroline.

“Wazazi wake walikuja kuomba punguzo la faini wakaambiwa ni matusi, kwa hiyo haipungui, kwa kuwa mimi na mwenzangu tunapendana tukaamua kuishi bila kuoana.”

Caroline anasema pamoja na wazazi kuweka ugumu wa ndoa hiyo kwa sababu ya faini, sasa hivi wanamtambua mwenza wake kama mkwe wao na wanamshirikisha hata kwenye masuala ya kifamilia.

Tofauti na mitazamo ya vijana hao, Muhsin Yassin anasema hakuna gharama kubwa kama kijana umejipanga na umedhamiria kuoa.

Anasema wakati anafanikisha hilo, alilipa Sh5 milioni ya masuala ya kimila na mahari.

“Haikunisumbua kwa kuwa nilikuwa na dhamira, hivyo nilijipanga mapema, nimeoa Pemba, huko wengi wanasema kuna gharama lakini ukiwa na dhamira unajipanga unafanikisha,” anasema Yassin.

Anasisitiza vijana wengi wanaona masharti ya ndoa magumu kwa kuwa tayari wameshaishi na watarajiwa wao, hivyo hawana tena shauku ya kuona watakutana na nini baada ya kuwaoa.

“Wewe umeishi na mwanamke miaka miwili alafu unataka kumuoa ukitajiwa hata Sh50,000 utaona kubwa kwa sababu tayari unamjua, hakuna kipya ndani yake, unatamani upewe hata bure,” anasema Yassin.

Dickson Mlai anaeleza hakuna sababu ya kuwekwa masharti kwa kuwa, hata usipooa utapata haki za ndoa.

“Wazazi wangejiongeza ujue, sawa unanipa masharti mengi lakini hata bila masharti yako mimi naweza kuwa na mwanao, mimi naona bora upunguze masharti ili uepushe kuletewa mjukuu bila mwanao kuolewa,” anasema Mlai.

Anasema hofu ya vijana si mahari, bali ni zile taratibu nyingine za kimila zinazotajwa, wakati mwingine huzidi hata kiwango cha mahari.

“Umeniambia mahari Sh2 milioni, vinahitajika na vitu vingine thamani yake inazidi Sh2 milioni eti mila, nitakuletea mjukuu tuone kama hutampokea,” anasema Mlai.

Kauli hizo za vijana, zinamuibua Silas Martin, mmoja wa wazazi anayesema wingi wa vigezo ni kipimo cha uwezo wa muoaji kama ataweza kumhudumia vema mwenza wake.

“Usipoweka kipimo hicho utaruhusu mwanao aolewe na mtu ambaye hata mlo wao wa siku changamoto, sasa kama mtu amemudu kuleta vitu vya kimila inatosha kumpima kuwa atamudu majukumu ya familia yake,” anasema Martin.

Anasema baadhi ya makabila, vifaa vya kimila ni muhimu kulipwa, tena vinapaswa kuanza kabla ya mahari ili kuepuka laana kutoka kwa wazee waliotangulia.

Mzazi mwingine, Mwantum Tebweta anasema kama mwanawe amependa hana budi kumrahisishia mazingira ili waowane kuepusha matokeo mengine.

“Unamuuliza binti yako mwenzio unamuonaje, hali yake kiuchumi kama anamudu majukumu ya familia, mwanao atakwambia; sisi Waislamu mahari anataja binti.

“Kwa hiyo atamtajia mwenzie kiwango anachoona atamudu, kuhusu mambo ya kimila tutataja kuendana na uchumi wa mwanamume, maana tunalenga kutekeleza sio kukwaza, ndoa ni jambo la heri,” anasema Mwantum.

Wazee wa kimila

Chifu wa kabila la Wapare, Ruben Muyuku anasema kuporomoka kwa maadili ndiko kunakowafanya vijana waone michakato ya ndoa ni migumu.

Anasema vijana wa sasa wanaamua wenyewe kuhusu ndoa bila kuwashirikisha wazazi, hatimaye wanapopewa taratibu za kimila huziona kama vikwazo.

“Unajua sisi zamani wazazi wa pande mbili ndiyo wanakutana wanazungumza, hata ikitajwa gharama kubwa kiasi gani na yakawekwa masharti mengi, wanajadiliana wanafikia muafaka.

“Kutokana na umri wao wanaelewana kulipa kidogo kidogo au kupunguziana hadi kiasi kinachostahili kulingana na uwezo wa muoaji, lakini siku hizi vijana wanakurupuka,” anasema Chifu Muyuku.

Anasema kuepukwa kwa michakato na kuzirahisisha ndoa ndiko kunakozifanya zisidumu, akisisitiza umuhimu wa kufuatwa mila na desturi kama ilivyokuwa zamani.

Kuhusu kutozwa faini iwapo wawili hao wamepata mtoto kabla ya ndoa, anasema utamaduni huo umerithiwa kutoka enzi za wazee na lazima ufuatwe.

“Hiyo ni dharau, yaani mmejiamulia wenyewe mkapata mtoto leo ndiyo mnakuja kwangu, alafu unataka nisiwatwange faini, maadili yameshuka sana siku hizi,” anasema Chifu Muyuku.

Mwenyekiti wa Machifu Tanzania, Tonisiza Antonia anasema kuna haja ya kufanyika mabadiliko kwa baadhi ya mila na desturi ili ziendane na vizazi vya sasa.

Hoja yake hiyo inatokana na kile anachofafanua kuwa, vizazi vya sasa ni tofauti na zamani, hilo linatokana na namna vilivyolelewa na hata maisha vinavyokutana nayo.

“Tukilazimisha kufanya kila kitu kama zamani tutajikuta tunaangukia pabaya, kipi bora kati ya uletewe mjukuu bila matarajio na ulegeze masharti ili uletewe mjukuu kwa heshima,” anasema Antonia, ambaye ni mwenyekiti wa machifu nchini.

Anasema mahari ni jambo la msingi katika ndoa, ni wajibu wa muoaji atozwe lakini kusiwepo vizingiti vingine lukuki, vitaharibu mipango ya vijana.

“Ukisema ufananishe na zamani, enzi hizo vijana walitafutiwa wachumba, siku hizi umtafutie kijana mchumba atamkataa, wanakutana masomoni huko, wakikuheshimu ndiyo wanakuja nyumbani, lakini wengine utakuta wanaamua huko huko walipo unaletewa matokeo,” anasema Antonia.

Hata hivyo, anasema vijana wa sasa wanapaswa kusikilizwa na kupewa miongozo na sio kuweka ugumu kwenye utekelezwaji wa masuala yenye heshima ya familia.

“Tubadilike kuendana na wakati, kuna mambo yasiyo ya lazima, muhimu yapungue, dunia imebadilika sasa. Ili mila ziheshimiwe lazima tuwasikilize vijana,” anasema Antonia.

Viongozi wa dini

Akizungumzia hilo, Imam Mkuu wa Msikiti wa Temeke Mwisho, jijini Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum anasema misingi ya dini ya Kiislamu inalitaja suala la ndoa kuwa ibada na kwamba halitakiwi kuwekewa uzito.

“Mtume Mohammad (S.A.W), anasema ifanyeni dini kuwa nyepesi, ukiweka uzito unakiuka misingi ya dini,” anasema Sheikh Salum.

Anasema dini hiyo inatamka mahari kuwa jambo muhimu katika ndoa, lakini si mambo mengine kama mkaja wa babu na vinginevyo.

Sheikh Salumu anasema ingawa si mbaya kulipa hiyo kama ni hiari kati ya muoaji na muolewaji, jambo hilo hilo litageuka kuwa haramu kama litafanywa kuwa takwa la lazima.

“Mkiamua wenyewe kwa hiari yenu mtozane vitu hivyo kwa ajili ya kuonyeshana upendo au furaha katika familia si jambo baya, lakini ukilazimisha litakuwa jambo haramu, kitu muhimu ni mahari pasi na mahari hakuna ndoa,” anasema.

Kulazimishwa na masuala hayo ya kimila, Sheikh Salum anasema ndiko kunakowajengea hofu vijana ya kuingia kwenye ndoa.

Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Steven Munga anasema kwa kawaida kanisa haliingilii mambo ya mahari na vitu vingine vya kimila wanaachiwa wazazi na tamaduni zao.

Lakini kwa hali ilivyo, anasema kuna umuhimu wa kanisa kuingilia kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu suala hilo ili kurahisisha ndoa badala ya kukwaza.

“Huwa najiuliza kwa nini haya mambo ya mila hatuyaoni kwenye maeneo mengine yanajitokeza kwenye mahari tu, mimi nadhani ni uroho wa mali tu,” anasema Askofu Munga.

Anasema lazima kanisa lifundishe kuwa ndoa si chanzo cha kipato na ikiwezekana mambo yasiyo ya msingi yaondolewe kurahisisha ufungwaji wake.

Askofu Munga anasema kanisa lisipofanya hivyo, kuna hatari kwa kizazi cha sasa kuingia katika mambo yanayomchukiza Mungu, ukizingatia kumekuwa na majanga mengi siku hizi.

“Mungu hakutoa watoto kuwa msingi wa kipato, hili ni jambo jema, turahisishe watu waoane ili tuepuke athari nyingine,” anasema Dk Munga.

Mchungaji wa Kanisa la Waadventisti Wasabato, Charles Mjema anasema ipo migongano kati ya mila na dini kwenye suala la kuoa.

Anasema vigezo vya kidini ni ridhaa ya muoaji na muolewaji, wazazi, taarifa kanisani na mahari na kwamba matakwa mengine ya kimila yanahusu mila.

“Sisi kwenye dini kinachotakiwa ni muoaji, anayeolewa na wazazi waridhie, lakini taarifa itolewe kanisani, jambo lingine ni mahari, hii ni ile inayotajwa, sio vile vingine vya kimila vile vinahusu tamaduni,” anasema Mchungaji Mjema.

Pamoja na vigezo hivyo kuwatisha vijana wengi kuingia katika ndoa kwa upande mmoja, Mchungaji Mjema analitaka kundi hilo kuacha kulalamika kwa upande mwingine.

“Vijana wapunguze kupenda vya bure, hakuna ugumu kama utajipanga, wajipange, mambo yote yatakuwa sawa,” anasema.

Mchungaji Mjema anasimulia alivyowahi kuwa mshenga walitumia saa nane kujadili mahari, lakini waliafikiana.

“Wazazi walitaja kiasi cha fedha kilichozidi uwezo wa kijana aliyetaka kuoa, tukajadili wakagoma, ikabidi tukubaliane kulipa kidogo kidogo lakini vijana waowane kwanza, jambo likafanyika,” anasema.

Nadin Mwamlani ni mshenga mwingine, anasema kila kitu kwenye kuoa kitakuwa rahisi kama utashirikisha watu sahihi kwenye michakato yake.

“Kuanzia kwenye mshenga huwezi kupeleka mtu asiye na heshima, ndiyo maana kuna umuhimu wa kupeleka wazee wenye adabu wanaojua kuzungumza na angalau wawe wanafahamu tamaduni za wanaoolewa.

“Hiyo itarahisisha mazungumzo, lakini kutakuwa na undugu ndani ya mazungumzo hayo, kila kitu kinajadilika, isipokuwa vijana wa siku hizi anayeoa anaenda kujitambulisha mwenyewe, barua anapeleka mwenyewe na mahari mwenyewe na muoaji bado ni yeye yeye, haya ni mambo ya kisasa, lazima yatakukwamisha,” anasema Mwamlani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi