Connect with us

Kitaifa

Sababu Kagera kukumbwa na majanga mengi

Unaweza kusema ni mkoa unaokumbwa na matukio ya kutisha, pengine kutokana na eneo lake kijiografia na kijiolojia.

Huo ni Mkoa wa Kagera, ulio kaskazini magharibi mwa Tanzania, ukipakana na nchi nne ambazo ni Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya kutoka Ziwa Victoria.

Mkoa huo umekumbwa na vita kati ya Tanzania na Uganda mwaka 1978, ugonjwa wa Ukimwi kuingilia mkoa huo, janga la wakimbizi kutoka Rwanda na Burundi, tetemeko la ardhi na sasa ugonjwa wa Marburg.

Kutokana na majanga hayo, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu alisema Serikali ina mpango maalumu wa kuhakikisha mipaka ya nchi iliyopo katika mkoa huo inalindwa.

Alisema kwenye mipaka yote kuna wahudumu wa afya kwa ajili ya kufanya ukaguzi kwa wale wanaotoka na kuingia.

“Kagera kwenye boda zote kuna watumishi wa afya, kwa mfano Mutukura pale kuna ofisi ambayo wanaangalia vitu vyote vinavyotakiwa kuangaliwa kwa kufuata kanuni za kimataifa.

“Nyakati zote wanapima joto la mwili, pia wanarekodi kwa ajili ya ufuatiliaji,” alisema.

Profesa Nagu alisema katika sehemu nyingine zote wanafuata taratibu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kuangalia homa ya manjano, huwa wanangalia chanjo kama wakati wa janga la Uviko-19 na magonjwa mengine.

“Watumishi wa afya wapo kila boda na wana jukumu la kuhakikisha Tanzania ipo salama na watu wote wanakuwa salama kwa maana ya afya,” alisema Profesa Nagu.

Wataalamu wa masuala ya afya wa mkoa huo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Afya wanaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha magonjwa ya milipuko hayaingii mkoani humo kupitia mipaka.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila alisema wamekuwa wakifanya ukaguzi wa raia wa kigeni kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaoingia kupitia vituo vya mpakani vya mkoa huo.

Alisema mkoa huo kijiografia unapakana na nchi tatu, zikiwemo Uganda kwa upande wa kaskazini, Rwanda na Burundi kwa upande wa magharibi.

“Kazi hii imekuwa endelevu kulingana na jiografia ya mkoa wetu. Kila anayeingia tunahakikisha tunapima joto lake la mwili, tunafuatilia pia kaguzi nyingine kama ambavyo kanuni za kimataifa zinatutaka,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikiongeza vifaa kinga na kuwawezesha kielimu wataalamu wa afya walioko katika hospitali za mkoa huo na vituo vya ukaguzi mpakani.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk Issesanda Kaniki alisema Ngara na boda ya Kakonko huwa kuna wakimbizi wa kila siku wanaingia na utaratibu waliouweka wote wanapita kwenye mipaka rasmi.

“Kwenye mipaka yetu tumeweka huduma za afya, kuna vipimo kila kitu, lakini bado tuna Kananga kuna sehemu ya afya ambayo wanapimwa, wanajaza zile fomu, kabla ya hapo wanapitia kitengo cha afya, wakitoka ndiyo wanaingia uhamiaji na kama ni wakimbizi wanapangiwa wapite wapi.

“Hata wale ambao hawapiti kwenye mipaka rasmi, kupitia Serikali ya kijiji, kata wote wanapitia huko na wanakwenda kuhakikiwa kwenye mipaka yetu, kwa upande na Ngara na maeneo mengine kiafya iko vizuri haina shida,” alisema Dk Kaniki.

Dk Kaniki alisema mikakati mbalimbali imekuwa ikifanywa katika kuhakikisha mkoa huo unakuwa salama na kuzuia magonjwa yote ya kuambukiza, yakiwemo ya mlipuko.

“Kwa sasa timu za ufuatiliaji zipo sehemu zote husika kwenye mialo, sehemu za kutolea huduma, vijijini na sehemu nyingine zote zinaendelea kufuatilia,” alisema Dk Kaniki.

Akitoa mfano, Dk Kaniki alisema kwa sasa kila halmashauri imetenga kituo kimoja ambacho kina kila kitu kuanzia miundombinu ya kumwezesha mgonjwa au mtu yeyote mwenye dalili kupata huduma zote.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe alisema wizara imekuwa ikitoa miongozo pindi milipuko inapotokea ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujikinga.

Alisema kutokana na mlipuko wa Marburg, Serikali imetoa mwongozo namba 13 kwa kuzingatia kanuni za kimataifa za afya ya mwaka 2005, ili kutekeleza hatua madhubuti zinazohusiana na usafiri wa kimataifa.

Alisema kuanzia sasa wasafiri wote wanaoondoka na wa ndani kutoka Mkoa wa Kagera watahitajika kujaza fomu ya mtandaoni ya ufuatiliaji wa wasafiri kupitia wavuti www.afyamsafiri.moh.go. .tz

“Kwa wasafiri wote wanaoingia katika viwanja vya ndege, kivuko cha ardhini au bandari, watapimwa halijoto ya mwili na kwamba watu wote watakaokutwa na hali ya homa wanapaswa kuzuiwa kusafiri ndani na nje ya nchi hadi watakapomaliza muda wa ufuatiliaji na kupewa kibali cha kusafiri na Mamlaka ya Afya ya Bandari,” alisema Dk Shekalaghe.

Alisema wasafiri wote watapewa kadi za maelezo ya afya zenye nambari ya bila malipo ambayo ni 199 na wanashauriwa kujifuatilia na kuripoti iwapo wana dalili za Marburg.

Machi 21 Tanzania ilitangaza mlipuko wa ugonjwa huo ambao uliathiri kata mbili za Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera ambapo watu wanane walipata maambukizi na watano kufariki dunia.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi