Connect with us

Kitaifa

Wizi wa vifaa vya daraja wasababisha hasara ya Sh21 milioni Musoma

Musoma. Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Kataryo na Wanyere Wilaya ya Musoma wanadaiwa kuiba vyuma na nati za daraja la Mto Suguti vyenye thamani ya zaidi ya Sh21 milioni hivyo kuhatarisha usalama wa daraja na watumiaji.

Daraja hilo la muda lenye thamani ya zaidi ya Sh2 bilioni liliwekwa katika eneo hilo Januari 2020 baada ya kuwepo changamoto ya kuvuka mto huo iliyosababisha athari mbalimbali ikiwemo vifo hasa vya wanafunzi waliokuwa wakivuka mto huo wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani kipindi cha masika.

Akizungumza leo Ijumaa, Machi 24, 2023 Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini ( Tarura) Wilaya ya Musoma,  Joseph Mkwizu amesema wizi huo umeibuka siku za hivi karibuni nakubaini  vifaa hivyo vinatumika kwenye mitambo ya wachimbaji wadogo wa madini  na kwaajili ya vifaa vya jembe la kukokota na ng’ombe ( plau).

“Tukiwa kwenye ukaguzi wa madaraja yetu tulibaini vyuma 16 vimeibiwa ikabidi twende kuvitengeneza sasa wakati tumekuja kwaajili ya kuweka hivyo vyuma tukabaini kuwa vingine 23 tena vimeibiwa,”amesema

Amesema hali hiyo inahatarisha usalama wa daraja hilo ambalo wameliazima kutoka  Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) huku akizitaka Serikali za vijiji hivyo viwili kukubaliana kwa pamoja namna ya kulililinda daraja hilo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma vijijini , Denis Ekwabi amewaambia wakazi wa vijiji hivyo kuwa endapo hawatashirikiana kulilinda daraja hilo basi ataishauri  Serikali iliondoe na kulipeleka sehemu nyingine.

“Serikali baada ya kuona mnapata changamoto za kuvuka hapa ikaamua kuleta daraja hili na wanufaika wakuu ni nyie pia wezi wanatokea hapa hapa na mnawajua sasa mnataka Serikali tena iwaletee mlinzi, hii haikubaliki,”amesema

Amesikitika kuona namna ambavyo wananchi hao wanahujumu mradi huo wa mabilioni na kusahau yaliyowahi kutokea kabla daraja hilo halijajengwa ikiwa ni pamoja na vifo vya wanafunzi wanane waliosombwa na maji miaka ya nyuma wakati wakivuka mto huo.

“Bahati nzuri mimi nilikuwa Diwani na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri kabla sijawa mwenyekiti wa cham, changamoto za hapa nazijua na ni miongoni mwa watu tulioomba daraja lije hapa sasa kama mnaona hamlitaki semeni  tulipeleke  kwingine ambapo wataweza kulitunza,” amesema

Baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo wamelaani wizi huo na kusema daraja hilo limekuwa mkombozi  wao kutokana na changamoto walizokuwa wakikumbana nazo kabla ya uwepo wa daraja hilo.

“Ni kweli hapa watoto walikuwa wanakufa sana kwa kusombwa na maji lakini pia wakina mama wajawazito walikuwa wakipata wakati mgumu kwenda kujifungua kwasababu huduma zote za kijamii zipo kijiji cha pili lakini baada ya daraja hili kuletwa hizo shida zote zimeisha,” amesema Ryoba Mwita mkazi wa kijiji cha Kataryo

Mkazi mwingine, Ngasa Mlima amesema awali kabla ya daraja hilo walikuwa wakilazimika kutumia daraja la miti ambalo halikuwa imara au wakati mwingine kuwatumia wapiga mbizi kuwavusha.

“Sisi huku ni wakulima wa mpunga hili daraja mbali na kuunganisha vijiji viwili lakini pia ni kiungo kati ya wilaya yetu na wilaya ya Bunda kwahiyo hawa wanaohujumu mradi huu tunaomba wakamatwe na kufungwa kabisa,”amesema Nzara Mininga mkazi wa Wanyere.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi