Connect with us

Kitaifa

Wasafiri kupimwa joto Kagera, watakaobainika kuzuiwa kusafiri

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya kutangazwa kuibuka kwa ugonjwa wa Marburg nchini, Serikali imetoa mwongozo wa wasafiri kote nchini kwa kuzingatia kanuni za kimataifa, huku ikiagiza utekelezaji wake uanze mara moja.

Machi 21 Serikali kupitia Wizara ya Afya ilithibitisha uwepo wa ugonjwa Marburg katika Wilaya ya Bukoba Vijijini, Kata ya Maruku na Kanyangereko, Vijiji vya Bulinda na Butayaibega, ambao uliua watu watano na watatu kupata maambukizi.

Mwongozo huo namba 13 umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe kwa kuzingatia kanuni za kimataifa za afya ya mwaka 2005 ili kjutekeleza hatua madhubuti zinazohusiana na usafiri wa kimataifa.

Amesema wasafiri wote wanaoondoka na wa ndani kutoka Mkoa wa Kagera watahitajika kujaza fomu ya mtandaoni ya ufuatiliaji wa wasafiri kupitia wavuti www.afyamsafiri.moh.go. .tz

Ameagiza kuwa watu wote walio katika orodha ya ufuatiliaji kutokana na kuwa karibu na wagonjwa wanapaswa kufuatiliwa mara kwa mara na kuzuiwa kuondoka katika maeneo yao ya kujitenga na kusafiri.

“Kwa wasafiri wote wanaoingia katika viwanja vya ndege, kivuko cha ardhini au bandari, watapimwa halijoto ya mwili na kwamba watu wote wataokutwa na hali ya homa wanapaswa kuzuiwa kusafiri ndani na nje ya nchi hadi watakapomaliza muda wa ufuatiliaji na kupewa kibali cha kusafiri na Mamlaka ya Afya ya Bandari,” amesema Dk Shekalaghe.

Amesema wasafiri wote watapewa kadi za maelezo ya afya zenye nambari ya bila malipo ambayo ni  199 na wanashauriwa kujifuatilia na kuripoti iwapo wana dalili za Marburg.

Dk Shekalaghe amesema walio na alama na dalili watapimwa na kutibiwa katika vituo vya afya vilivyoteuliwa kuhudumia wagonjwa hao vya serikali.

“Wakiwa nchini, wasafiri wote wa kimataifa wanapaswa kuzingatia kanuni za kuzuia na kudhibiti maambukizi kama vile usafi wa mikono, kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu na  kuripoti ishara au dalili zozote kwa kutumia nambari ya bure.

“Wamiliki wote wa vyombo vya usafiri wanapaswa kuzingatia kanuni zote za kinga na udhibiti wa maambukizi pamoja na usafi wa mikono na matumizi ya vipukusi,” amesema.

Dk Shekalaghe amesisitiza kuwa wasafiri wote wanapaswa kuzingatia hatua za kuingia, kutoka na kaguzi zote zinazotekelezwa ndani ya nchi.

Machi 21 Tanzania ilitangaza mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Marburg ambao umeathiri kata mbili za Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera iliyoko Kaskazini-Magharibi mwa nchi

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi