Kitaifa
Mabadiliko tabianchi yanavyoibuka na changamoto za kiafya
Dar es Salaam. Ongezeko la magonjwa ya mfumo wa upumuaji, maambukizi ya malaria, kipindupindu na yale ya mlipuko pamoja na kupungua kwa uwezo wa mbegu za kiume, imetajwa kuchangiwa na mabadiliko ya tabianchi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokumbwa na changamoto hiyo kwa kupata magonjwa ya mlipuko ukiwamo Uviko-19 pamoja na magonjwa ya mfumo wa upumuaji.
Hata hivyo, mwingiliano kati ya mabadiliko ya tabia nchi yanayoongeza joto duniani na athari zinazotokea katika afya unazidi kuimarika huku watoto wadogo wakitaabika.
Wakati hili likitokea, misimu ya joto imeelezwa kuwaathiri zaidi watoto kwani hawawezi kudhibiti joto la mwili kama ilivyo kwa watu wazima.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) iliyochapishwa Oktoba 2022 inasema jumla ya watoto milioni 559 duniani wanataabishwa na joto kali kwa sasa na kwamba idadi itaongeza mpaka zaidi ya bilioni mbili mwaka 2050.
Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef, Catherine Russell anasema wakati joto linaongezeka kuna hatari ya zebaki pia.
“Tayari mtoto mmoja kati ya watatu anaishi katika nchi zenye joto kali na hali itazidi kuwa mbaya zaidi,” anasema Catherine.
Rais mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko anasema mabadikiko ya tabianchi ndiyo yanayoongeza joto na likiongezeka halimuathiri binadamu pekee bali mazingira yote.
“Kuna athari zitatokea katika mimea na ardhi ambazo zitaathiri pia afya,” alisema.
Dk Nkoronko alisema joto likiongezeka husababisha majimaji ya mwili wa binadamu kupungua kupitia kutoa jasho.
“Ukitokwa sana jasho utapungukiwa maji mwilini katika kila mfumo kuanzia wa ubongo, mishipa ya fahamu, moyo, mapafu figo hivyo itakulazimu kunywa maji mengi ili kurudisha kiasi kilichotoka,” anasema.
Katika hali hiyo, anafafanua kuwa watoto wanaathirika zaidi kutokana na udogo wa miili yao hivyo kupoteza maji mengi.
Kukikosekana mavuno ya uhakika, anasema watu hawatapata chakula cha kutosha, watoto watadumaa kimwili na kiakili.
“Ieleweke kuwa ongezeko la joto linasababisha kuzaliana kwa bakteria wanaofurahia zaidi joto, huko huwa na uwezo wa kubadilisha tabia hata magonjwa anayougua binadamu yatabadilika kwa kiasi fulani,” anasema.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, joto linapokuwa kali hushusha uwezo wa kende kuzalisha mbegu za kiume hivyo kuongeza idadi ya wagumba.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi wa Hospitali ya Salaaman, Dk Abdul Mkeyenge anasema ili mbegu za kiume zizalishwe vizuri hazihitaji joto kubwa.
Maeneo mengi ya mjini anasema kuna viwanda vingi vinavyochochea wanaume kupata shida katika mfumo wao wa uzazi.
“Mbegu hukosa sifa za kumpa mwanamke ujauzito, hili pia ni miongoni mwa visababishi vya tatizo la ugumba katika jamii yetu,” anasema Dk Mkeyenge.
Kujikinga na joto
Wataalamu walishauri kuzingatia ulaji, unywaji, uvaaji na mtindo wa maisha unaofaa ili kupunguza kero ya joto na kuepuka magonjwa yatokanayo nalo.
Kunywa maji ya kutosha, kula matunda yenye majimaji na mbogamboga kwa wingi, ni kati ya vitu muhimu vinavyoshauriwa.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Pallangyo anasema ili kuuweka mwili sawa katika msimu wa joto inashauriwa kunywa angalau lita tatu mpaka sita za maji kila siku.
Dk Pallangyo ambaye ni mkuu wa kitengo cha utafiti JKCI, alisisitiza kuwa wenye magonjwa ya moyo na figo ni vizuri wabaki na kiasi walichoshauriwa ili wasilete madhara zaidi.
“Tunashauri vyakula vyepesi ili kuepuka kuchoka. Ni vema chakula kikawa laini na chenye majimaji au mchuzi wa kutosha na matunda yanayoshauriwa zaidi ni matikiti, matango, machungwa na mengine yenye majimaji ya kutosha,” anasema Dk Pallangyo.
Kuhusu mavazi, anasema watu wanashauriwa kuvaa nguo nyepesi zinazoruhusu ngozi kupumua hasa za pamba, linen na silk.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Andrew Foi anasema ni vema kuacha kufanya shughuli kwenye joto au jua kali na kuepuka kuwapaka watoto mafuta mazito mwilini.
“Tusiwaache watoto wacheze juani, tusiwapake mafuta ya mgando yanayoleta joto bali tutafute mafuta ya nazi au lotion. Tuangalie nguo wanazovaa na watoto wachanga tusiwafunike sana tuwaache wapate hewa ya kutosha,” anashauri daktari huyo.
Hata hivyo, Dk Foi anasema jua likizidi linaweza kusababisha mshtuko wa joto ndipo hutokea kupooza na akashindwa kuhimili jua na viungo vya ndani vikashindwa kuhimili joto.
Anasema kawaida binadamu jotoridi lake huwa sentigredi 36.9 na linapozidi hutambulika kuwa na homa na nyakati zingine anaweza kupata madhara.
Mtaalamu wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk Maghuha Stephano anasema unywaji maji wakati wa joto kali ni njia rahisi ya kuifanya ngozi isishambuliwe na saratani ya ngozi.
Athari kwa mifugo
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mwaka 2022, ulibaini athari nyingi ukiwamo ukame uliosababisha kupaa kwa bei ya vyakula na kufa kwa mifugo. Ripoti hiyo iliyochapishwa Novemba 2022, iliangalia mabadiliko ya tabianchi na athari za ukame.
Upungufu wa malisho uliojitokeza umechangia mifugo kufa. Mwaka 2021 pekee ng’ombe 90,000 walikufa wilayani Simanjiro mkoani Manyara. Hali kama hiyo pia ilijitokeza Longido, Bagamoyo na Kisarawe.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unashauri jamii kulinda mifumo ya ikolojia hasa misitu na uhifadhi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Viongozi wa sekta za afya barani Afrika kupitia mkutano wa Ajenda ya Afya Afrika 2023 (AHIAC) wamekubaliana kuwa na kauli moja kuhusu changamoto za kiafya zinazolikabili.
Ingawa Afrika inachangia kidogo katika kuzalisha hewa chafu na ongezeko la joto duniani, ndiyo iliyo hatarini zaidi kwa athari zake, wataalamu wa afya wanasema.