Connect with us

Kimataifa

Wafuasi wa Odinga wajitokeza kupinga ongezeko gharama za maisha, polisi waimarisha ulinzi

Nairobi. Vikosi vya polisi wa kutuliza ghasia nchini Kenya vimeingia mitaani leo Machi 20 kukabiliana na maandamano ya amani yaliyoitishwa na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga kupinga gharama za maisha nchini humo, licha ya maandamano hayo kupigwa marufuku.

Katika Kitongoji cha makazi duni ya Kibera jijini Nairobi, waandamanaji walichoma matairi huku vijana kadhaa wakikamatwa katika moja ya maeneo ya maandamano katika mji mkuu wa Nairobi.

Odinga ambaye alishindwa katika uchaguzi wa Rais, Agosti 2022 dhidi ya William Ruto, ameapa kwamba mikutano hiyo itaendelea.

“Ninataka Wakenya wajitokeze kwa wingi na kuonyesha kukerwa na yanayoendelea nchini mwetu,” aliwaambia wafuasi wake Jumapili.

Wakenya wanateseka kutokana na kupanda kwa bei ya mahitaji ya kimsingi, pamoja na kushuka kwa kasi kwa shilingi ya Kenya dhidi ya Dola ya Marekani na ukame ambao umewaacha mamilioni ya watu wakikosa chakula.

“Siku ya pambano,” ndiyo kichwa cha habari katika gazeti la The Standard la Kenya leo Jumatatu Machi 20, 2023.

Mkuu wa polisi wa kaunti ya Nairobi, Adamson Bungei alisema jana Jumapili kwamba polisi walipokea maombi ya kufanya maandamano mawili mwishoni mwa Jumamosi na mapema Jumapili wakati kwa kawaida taarifa ya mkutano wa hadhara inatakiwa kutolewa siku tatu kabla.

“Kwa usalama wa umma, hakuna chochote kilichotolewa,” alisema.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki pia alitoa taarifa siku ya Jumapili akionya kwamba yeyote atakayechochea ghasia za umma au kuvuruga amani atachukuliwa hatua.

Barabara zimekuwa tulivu kuliko kawaida jijini Nairobi leo Jumatatu na biashara nyingi zimefungwa kabla ya maandamano hayo, huku baadhi ya waajiri wakiwaambia wafanyakazi wao wafanyie kazi nyumbani.

Odinga alisema ameitisha maandamano kupinga “kupanda” kwa gharama za maisha na uchaguzi “ulioibiwa” Agosti 2022.

“Tangu Ruto aapishwe miezi sita iliyopita, ameendelea kuendesha nchi kwa dharau nyingi,” alisema huku akiangazia gharama za juu za mambo ya msingi kama vile mafuta, mafuta ya kupikia, karo za shule na umeme.

Odinga, kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja, amekuwa akipinga kwa muda mrefu kwamba uchaguzi wa Agosti ulikuwa na udanganyifu na kuishutumu serikali ya Ruto kuwa “haramu”.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Odinga ambaye alikuwa akigombea urais kwa mara ya tano, alishindwa na Ruto kwa takriban kura 233,000, moja ya tofauti zilizo karibu zaidi katika historia ya nchi.

Mahakama ya Juu ilitupilia mbali rufaa yake huku majaji wake wakitoa uamuzi kwa kauli moja kumthibitisha Ruto kwa kuwa hakukuwa na shahidi wa tutuma za Odinga.

Ruto kwa upande wake alitangaza kwamba hatatishwa na maandamano ya upinzani, akisema: “Hutatutishia kwa kauli za mwisho na fujo na kutokujali.”

“Hatutaruhusu hilo,” alisema Ruto huku akimtaka Odinga kuchukua hatua “kisheria na kikatiba”.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi