Connect with us

Kitaifa

NHC kujenga soko la madini la Sh5.4 bilioni

Mirerani. Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdalah amesema mradi wa ujenzi wa soko la madini Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, utafanyika mchana na usiku ili kuukamilisha kwa wakati.

Abdalah ameyasema hayo leo Jumamosi Machi 18 baada ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa soko la madini Mirerani (Tanzanite Trading Centre).

Amesema; “Kwa kuzingatia jitihada kubwa ambazo zinafanya na Rais Samia Suluhu Hassan, tunaahidi kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha jengo hili kukamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.”

Amesema mradi huo ulianza Mei 22 mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika Mei 21 mwaka huu na jengo hilo la ghorofa tano litagharimu kiasi cha sh5.4 bilioni.

“Hata hivyo, baadhi ya changamoto zinazotukabili ni kupanda kwa bei ya vifaa mara kwa mara na uwepo wa mvua kubwa ulioathiri kasi ya utekelezaji wa ujenzi,” amesema Abdalah.

Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda amesema kujengwa kwa soko la madini Mirerani kutaondoa hofu ya baadhi ya watu waliodhani soko la madini litahamishwa Mirerani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer ameishukuru Serikali ujenzi wa jengo hilo la soko la madini kwenye eneo hilo kwani litaongeza uchumi kwa jamii ya Simanjiro.

Hata hivyo, mjumbe wa kamati hiyo na Mbunge wa viti maalum vijana Taifa kupitia Mkoa wa Manyara, Asia Halamga ameishauri Serikali kutoa fedha kwa wakati ili kukamilisha jengo hilo kwa wakati.

“Fedha zikifika kwa wakati jengo litakamilika kwa muda uliopangwa, ila nawapongeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere na mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera kwa kufuatilia kwa karibu ujenzi wa jengo hili,” amesema Asia.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi