Connect with us

Kitaifa

Aina mpya dawa za kulevya hatari zaingia mtaani

Dar es Salaam. Vita dhidi ya dawa za kulevya inazidi kuwa mbichi.

Hivi sasa watumiaji wa ulevi huo, wamekuja na mbinu nyingine ya kutumia dawa za kutibu binadamu kama mbadala wa dawa za kulevya.

Mbinu hiyo ni matumizi ya dawa aina ya methamphetamine’ ambayo kwa sasa inatumika kwa kasi na kuanza kuwa tishio nchini.

Dawa hiyo ipo katika kundi la dawa za kulevya za vichangamshi na hutengenezwa kutokana na kemikali aina ya ‘pseudoephedrine’ kupitia viwanda bubu.

Kwa mujibu wa wataalamu, dawa hiyo hutumika kwa njia ya kuvuta puani, kuvuta mdomoni na kujidunga dozi ndogo. Pia hutumiwa kwa mfumo wa kidonge.

Kamishna Msaidizi Tiba na Huduma na Utengamano wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA), Dk Cassian Nyandindi anaeleza kuwa methamphetamine ni moja kati ya dawa ambazo madhara yake ni magumu kutibika kwa kuwa zinasabababisha athari ya kudumu katika ubongo.

Dawa hiyo ya kulevya imepewa majina mengi, ikiwemo black beauties, ice, glass, speed, crystal, crystal meth, crank, tweak, go-fast na uppers.

“Methamphetamine ni moja kati ya dawa za kulevya iliyo na uraibu wa hali ya juu na hivyo kumsababishia mtumiaji kuingia katika uraibu wa dawa hiyo na watumiaji wengi wamekuwa wakieleza kuwa wanajikuta katika hali ya uraibu pindi tu wanapoanza kuitumia kwa mara ya kwanza,” anasema Dk Nyandindi.

Baadhi ya watumiaji wa dawa hizo waliozungumza na Mwananchi wamesema huzitumia kwa kujipaka mwilini, kuvuta kama sigara, kuvuta puani na kujidunga mwilini.

Mwananchi lilifanya mahojiano na mmoja wa watumiaji, eneo la Vingunguti jijini hapa ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini; alisema dawa aina ya methamphetamine ina ‘speed’ kwa mtumiaji hata anayetumia njia ya kujipaka mwilini anajikuta yupo kwenye hali ya uraibu.

Hii dawa ninaitumia kwa kupakaza kwenye mwili na inafanya kazi kwa haraka kama nilikuwa na mawazo yote yanaondoka. Sihitaji kujidunga sindano kama wengine wanavyofanya,” anaelezea mtumiaji huyo.

Anasema dawa hiyo inauzwa kwa siri na wamesikia kuwa zinatengenezwa kwenye viwanda nje ya nchi, zikiwemo nchi za Ulaya, ambapo watumiaji wa dawa za kulevya wameamua kutumia methamphetamine kwa kuwa heroin na cocaine hazipatikani kirahisi.

Mkazi mwingine katika eneo hilo, Israel Raphael anasema aliwahi kutumia mara moja dawa hiyo, kabla ya kuachana nayo baada kushindwa kupata usingizi na kuona vitu visivyokuwepo.

“Siku nilipotumia dawa hii nilikosa usingizi kabisa na nilikuwa naona vitu visivyokuwepo na kuna mtu namfahamu ambaye anatumia dawa hizo amekuwa mtu mwenye hasira na ni mgomvi wa mara kwa mara na mwenye visasi,” anasimulia Raphael.

Madhara ya muda mfupi

Dk Nyandindi anaeleza kwa anayetumia aina hiyo ya dawa anapata madhara ya kukosa usingizi, utulivu, kuwa na hali ya wasiwasi, kichefuchefu, kujihisi mwenye nguvu kuliko uhalisia, kuwa na tabia ya ukorofi na kuhisi kukerwa

Madhara mengine ni mapigo ya moyo kwenda kasi, kupoteza hamu ya kula, kupungua uzito, kuwa na hasira kali na kuchanganyikiwa.

‘‘Dozi inavyozidi kuwa kubwa ndivyo mtumiaji anavyokuwa kwenye hali ya kupata madhara zaidi kama vile kuongezeka kwa hali ya hofu na wakati mwingine mtumiaji kuleta vurugu,’’ anaeleza.

Dk Nyandindi alitaja madhara mengine wanayoyapata watumiaji wa dawa hizo, ni kuona au kusikia vitu visivyokuwepo, kuhisi kufuatiliwa na watu wanaotaka kumdhuru au kuwa na hofu juu ya usalama wake pamoja na kupata degedege, ambayo inaweza hata kumsababishia kifo.

Wataalamu wanaeleza, mtumiaji wa dawa za kulevya aina ya methamphetamine, huunda hisia bandia ya kuwa na nguvu nyingi, inayoweza kusukuma mwili zaidi na haraka kuliko anavyoweza.

Huwa inaongeza mapigo ya moyo, shinikizo la damu na humweka mtu katika hatari ya kupata kiharusi.

Pia anayetumia dawa hiyo anaweza kuhisi uchovu usioisha au kujisikia huzuni sana au kupatwa na sonona.

Aidha, watumiaji wanaojidunga kwa kuchangia sindano wako hatarini kupata maambukizi ya VVU au ugonjwa wa Ukimwi.

Watumiaji dawa hizo wanaweza kufa kutokana na joto jingi linalotengenezeka mwilini, degedege, uharibifu wa ubongo na kutawaliwa na uraibu.

Ukitaka kumtambua mtumiaji, utamjua kwa dalili kama vile kutopata usingizi, kukerwa kirahisi, kupiga kelele, anafanya mambo bila kujali, muoga, hujikunakuna, kusinzia. Pia anaonekana kama mtu aliyechanganyikiwa na pia kukosa hamu ya chakula.

Madhara ya muda mrefu

Dk Nyandindi anasema watumiaji wa dawa hizo wanapata madhara ya muda mrefu kama kupata uraibu, kuongezeka kwa mapigo ya moyo na shinikizo la damu, kupata ugonjwa wa kifafa, kansa ya ini, kuharibika kwa figo na mapafu.

Pia wanaathirika sehemu za ubongo hivyo kupunguza uwezo wa kumbukumbu na uwezo wa kuelewa na kutafakari mambo, kuathiri mishipa ya damu kwenye ubongo na kumsababishia kiharusi au mapigo ya moyo yawe nje ya utaratibu wa mwili, kupata shida ya mishipa ya moyo na hata kifo.

Sheria inasemaje kuhusu methamphetamine?

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, matumizi na biashara ya dawa ya kulevya aina ya methamphetamine katika ni haramu nchini.

Pia kujihusisha kwa namna yoyote na methamphetamine (kutengeneza, kuhifadhi, kuuza, kutumia) ni kosa la jinai.

Wananchi wametakiwa kutojihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya kwa namna yoyote, ikiwamo dawa ya methamphetamine kwa kutengeneza, kuhifadhi, kuuza na kutumia. Na ni kosa la jinai ambalo adhabu yake inaweza kuwa hadi kufungwa maisha.

TMDA yanena

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Dk Yonah Mwalwisi anasema dawa aina ya methamphetamine ni za tiba na zinatumika kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye matatizo ya akili.

“Methamphetamine zimepigwa marufuku kwa kuwa zinatumiwa na waraibu wa dawa za kulevya kama dawa za kulevya,” anasema Dk Mwalwisi.

Anasema kama kuna uhitaji nchini, lazima mamlaka husika ziombe kwenye nchi inayotengeneza dawa hizo kwa kibali maalumu na zitolewe sababu ya kuagiza kiasi husika cha dawa hiyo.

Dk Mwalwisi anasema mwagizaji wa dawa hizo ni Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hivyo hospitali yenye uhitaji huo, inatakiwa iombe kibali kutoka TMDA ili ikanunue MSD.

“Vituo vyote vya hospitali wakitaka kutumia dawa hizi TMDA lazima tuwajue wanaohitaji na kiasi gani wanachotaka, hivyo lazima waje kuomba kibali kwetu ili tuweze kuwaruhusu,” anasema Dk Mwalwisi.

Anaeleza kuwa dawa hiyo inatunzwa sehemu maalumu na haichanganywi na dawa nyingine.

‘‘Anayekabidhiwa funguo ni mtu mmoja tu, lengo isije ikatumiwa vibaya kwa matumizi mengine kama dawa za kulevya.

“Ikifika hatua ya mgonjwa kutakiwa kutumia dawa hiyo kwa njia ya sindano, TMDA watahitaji kujua mgonjwa yupi na kiasi gani cha dawa anachohitaji kutumia,’’ anafafanua.

Dk Mwalwisi anasema chupa ya dawa hiyo iliyotumika, lazima isimamiwe na kamati maalumu ya hospitali husika iliyoteuliwa kwa ajili ya kuteketeza na wasipodhibiti dawa hizo zitatumika vibaya.

Wito

Anawataka wananchi waachane na matumizi holela ya dawa zenye asili ya kulevya, kwani zina madhara, ikiwemo mhusika kujiingiza kwenye uhalifu kama vile mauaji na wizi.

Jeshi la Polisi

Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2022, Jeshi la Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, lilikamata jumla ya gramu 234 za dawa hiyo.

Pia Desemba mwaka 2022, DCEA iliwakamata watuhumiwa wanne wakisafirisha gramu 655.75 za cocaine na gramu 968.67 za metamphetamine.

Januari 25, 2023 katika maadhimisho ya wiki ya sheria, aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Geralda Kusaya alikiri bado kuna changamoto ya matumizi ya dawa za binadamu zenye asili ya kulevya kutumika kama mbadala wa dawa za kulevya.

Alitaja baadhi ya dawa hizo zinazotumika ndivyo sivyo kuwa ni pamoja na ephedrine inayotumika kutibu kifua; ketamine inayotumika kuondoa maumivu kwenye operesheni na ipo ya aina mbili, ya vidonge na maji. Pia kuna tramadol inayotumika kuondoa maumivu na vallium inayotibu mafua na kupata usingizi.

Kusaya alisema dawa hizo hutumika kwa sababu wahusika wanakosa kile wanachokihitaji, hivyo ikitokea bahati mbaya matumizi yakawa makubwa, mtu anaweza kupoteza hata maisha.

Ijue methamphetamine

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya dawa za kulevya iliyotolewa na DCEA Juni 2021, dawa ya methamphetamine imo katika jamii ya dawa za kulevya ya Amphetamine (ATS), zikiwamo pia amphetamine na ecstasy.

Aidha, taarifa ya dawa za kulevya ya dunia ya mwaka 2021, inaonesha kuwa, takribani watu milioni 27 walitumia ATS mwaka 2019 ambao ni sawa na asilimia 0.5 ya watu wote duniani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiwango kikubwa cha matumizi kiliripotiwa Amerika ya Kaskazini kwa asilimia 2.3 na kiwango kidogo barani Afrika kwa asilimia 0.4. Takribani watu milioni 20 walitumia ecstasy mwaka 2020.

“Matumizi ya dawa hizi kwa njia ya kujidunga yameendelea kusababisha maambukizi ya VVU katika maeneo mbalimbali duniani,” ilisema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kati ya mwaka 2015 na 2019 zaidi ya asilimia 95 ya maabara haramu za ATS zilizogunduliwa zilikuwa zinatengeneza methamphetamine.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi