Kitaifa

Bajeti ya mishahara, ajira mpya serikalini

Dodoma. Serikali imewasilisha kwa wabunge mwelekeo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ikitarajia kutumia Sh44.38b trilioni, kati yake Sh10.88 trilioni zikielekezwa kwenye ajira mpya, kupandisha mishahara na madaraja kwa watumishi wa umma.

Mbali na hayo, pia katika mwaka huo wa fedha, inakusudia kutumia Sh12.77 trilioni kulipa deni la Serikali na gharama zingine za mfuko wake mkuu.

Matumizi hayo ni ongezeko la asilimia 7 la bajeti ya mwaka 2022/2023 unaoisha Juni 30 ya Sh41.48 trilioni.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha kwa wabunge Mpango wa Taifa wa Maendeleo na Mifumo pamoja na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024.

Alisema katika bajeti hiyo ya Sh44.38 trilioni, fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ni Sh29.23 trilioni, zikijumuisha Sh12.77 trilioni kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za mfuko mkuu.

Mbali na Sh10.88 trilioni zitakazotumika kwa ajili ya mishahara ikiwemo upandishaji wa madaraja kwa watumishi na ajira mpya, Dk Mwigulu alisema Sh6.39 trilioni zitatengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC), hivyo kufanya karibu ongezeko lote la bajeti kuhudumia matumizi mengineyo.

Akizungumzia matumizi ya maendeleo, Dk Mwigulu alisema yanatarajiwa kuwa Sh15.15 trilioni; kati ya hizo, Sh11.87 trilioni ni fedha za ndani (asilimia 78.3) na Sh3.28 trilioni (asilimia 21.7)ni fedha za nje.

Katika bajeti inayoelekea ukingoni ya 2022/23 fedha za maendeleo zilitengwa Sh15.0 trilioni.

Dk Mwigulu alisema ukomo wa fedha za maendeleo upo ndani ya wigo wa kati ya asilimia 30 na 40 ulioanishwa kwenye Mpango elekezi wa muda mrefu (2011/12 – 2025/26).

“Utengaji wa fedha za maendeleo umezingatia miradi inayoendelea ikiwemo miradi ya kimkakati na ya kielelezo pamoja na utekelezaji wa miradi kupitia utaratibu wa PPP (Ushirikiano wa Sekta Umma na Binafsi) ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia miradi ya maendeleo kwa utaratibu uliozoeleka,” alisema.

Waziri wa Fedha alisema bajeti ya matumizi ya kawaida imeongezeka kufuatia kukamilika kwa miradi ya maendeleo, hususan kwenye sekta za huduma za jamii ambazo kwa sasa zinahitaji fedha za matumizi ya kawaida kwa ajili ya uendeshaji.

Vipaumbele vya bajeti

Katika mwaka ujao wa fedha, Dk Mwigulu alisema Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa miradi ya kielelezo na kimkakati inayotarajiwa kuwa na matokeo mapana na ya haraka katika uchumi.

Alisema miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la Umeme wa Maji la Julius Nyerere na kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Miradi mingine ni kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi, makaa ya Mawe (Mchuchuma – Njombe) na Chuma (Liganga – Njombe) na wa kufua Umeme wa Maji wa Ruhudji (MW 358) – Njombe.

Vilevile, alisema Serikali itafanya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 pamoja na maandalizi ya Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Serikali vilevile, alisema itaendelea na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, kuimarisha mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutekeleza wa mkakati wa uchumi wa bluu.

Miradi ya maendeleo itakayotekelezwa, Mwigulu alisema itazingatia maeneo matano ya kipaumbele ya Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26.

Maeneo hayo ni miradi ambayo itachochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

Kubana matumizi

Kama ilivyokuwa katika bajeti inayoendelea kutekelezwa, Dk Mwigulu alisema katika mwaka 2023/24, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, Sheria ya Fedha za Umma, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa na Sheria ya Ununuzi wa Umma.

Alisema Serikali itaendelea kugharamia miradi ya maendeleo inayochochea ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma za jamii, kuongeza uzalishaji na mauzo nje pamoja na maeneo yenye vyanzo mahsusi kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo maalum yenye masilahi mapana kwa Taifa kama vile Mfuko wa Barabara, Mfuko wa Reli, Mfuko wa Umeme Vijijini na Mfuko wa Maji na Wakala wa Maji Vijijini.

Kipaumbele kingine, ni Serikali kudhibiti ongezeko la malimbikizo ya madai, madeni pamoja na kufanya maboresho katika mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma ili kuongeza tija, ufanisi na thamani ya fedha katika ununuzi wa umma.

Akiba na deni la Serikali

Akizungumzia hali ya uchumi, Dk Mwigulu alisema katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2022 uchumi wa Taifa ulikua kwa wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2021.

“Mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 22.5 Desemba 2022 ikilinganishwa na asilimia 10 katika kipindi kama hicho mwaka 2021,” alisema.

Vilevile, alisema akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 5,177.2 Desemba 2022 iliyotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 4.7.

“Kiwango hiki ni ndani ya lengo la nchi na lengo la kimataifa la akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuagiza bidhaa kwa miezi isiyopungua minne,” alisema Dk Mwigulu.

Kuhusu Deni la Serikali, alisema hadi Desemba 2022, lilikuwa Sh74.63 trilioni kufuatia kuendelea kupokewa kwa fedha za mikopo zinazotumika kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya kielelezo ndani ya nchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa mwenyekiti, alisema baada ya kusomwa kwa taarifa hiyo hakutakuwa na majadiliano yoyote na kwamba mbunge ambaye hakuelewa aende kusoma katika taarifa waliyoingiziwa katika vishikwambi vyao.

Walichokisema wachumi

Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka alisema Serikali ina changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.

Alisema jambo la kushirikisha sekta binafsi litasaidia katika kutoa ahueni kwa Serikali katika upatikanaji wa fedha kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Mtalaamu wa Uchumi kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara, Dk Nasibu Mramba alisema suala la kuongeza ajira mpya ni zuri kwa sababu katika utumishi wa umma zipo taasisi au ofisi ambazo zina upungufu mkubwa wa watumishi na mambo hayaendi.

“Kwa mfano tukienda katika kada ya afya kuna madaktari wengi wanafanya kwa mikataba na hawajaajiriwa, hawa ni muhimu sana hasa kwa wakati huu. Faida yake wakiajiriwa watu wapya itaongeza fedha katika mzunguko na kupunguza kilio cha ajira nchini,” alisema.

Aidha, alisema kuweka kipaumbele katika kilimo ni muhimu kwa sababu ya mfumko wa bei unaoonekana nchini ambao umekuwa mkubwa huku bidhaa za chakula zikihitajika duniani kote.

Alisema vipaumbele vyote vilivyotajwa havishangazi kwa sababu ni muhimu kuwepo katika bajeti hiyo hasa katika wakati huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi