Connect with us

Kitaifa

Mbu hatari wa malaria anyemelea

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiwa katika jitihada zinazoelekea mahala pazuri pa kutokomeza ugonjwa wa malaria, mbu vamizi anayeeneza kwa kasi vimelea vya ugonjwa huo, ameibuka Kaskazini mwa Kenya akileta changamoto mpya kwa kuzua hofu.

Matumizi ya chandarua, dawa zenye viuatilifu na chanjo zilitoa matokeo chanya, lakini kuibuka kwa mbu huyo kumeibua mjadala katika jamii juu ya kumkabili.

Taarifa za awali zinadai kuwa mbu huyo amejenga usugu dhidi ya dawa zinazotumika nchini.

Mbu huyo aliyegundulika katika kaunti ndogo za Laisamis na Saku, ametajwa kuzaliana kwenye maji yaliyotuama, matairi, matanki yaliyoachwa wazi, mifereji ya maji machafu, matanki ya juu na chini ya ardhi na katika mazingira machafu.

Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya imesema mbu huyo aina ya Anopheles stephensi mwenye asili ya Asia Kusini na Mashariki ya Kati husambaza vimelea viwili vya malaria ambavyo vina hatari kubwa ya ugonjwa na husababisha kifo.

Takwimu kutoka hospitali katika maeneo yaliyoathiriwa na mbu huyo zimeonyesha kuongezeka kwa wagonjwa wa malaria nje ya msimu wa kawaida wa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Shirika la kuhudumia watoto duniani (Unicef), malaria huambukizwa kwa kung’atwa na mbu jike Anopheles ambao huua mtoto mmoja chini ya miaka mitano barani Afrika kila dakika moja.

“Malaria ni tatizo kubwa la afya ya umma nchini Kenya kwa sasa. Ugonjwa huu umeenea katika sehemu tofauti za nchi na karibu asilimia 70 ya watu wote wako hatarini,” ilieleza taarifa ya Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya.

Kugunduliwa kwa mbu huyu kunaibua tishio kubwa kwa afya ya umma nchini Kenya na nchi jirani, ikiwemo Tanzania ambako kumekuwa na taarifa za kupungua kwa maambukizi ya malaria.

Mbu huyo vamizi ametajwa kuenea haraka zaidi katika maeneo mapya na kwamba anaweza kuishi eneo lolote bila kujali hali ya hewa, ikilinganishwa na mbu wengine ambao hustahimili zaidi maeneo ya joto.

Uvamizi wa mbu huyo unaleta tishio kwa juhudi za nchi kudhibiti na kumaliza ugonjwa wa malaria, huku wataalamu wakishauri kuwa nchi lazima ichukue hatua za haraka kutathmini na kuweka mikakati ya kuzuia tishio hilo.

Serikali yaanza utafiti

Kaimu Meneja, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria Wizara ya Afya, Dk Samwel Lazaro alisema katika udhibiti wa malaria nchini Serikali imekuwa ikidhibiti mbu asiweze kueneza ugonjwa huo kupitia afua mbalimbali, hasa matumizi ya vyandarua, upuliziaji wa dawa na viuatilifu.

Alisema uwekaji viuatilifu umekuwa ukifanywa zaidi Kanda ya Ziwa kwa kupulizia ndani ya nyumba, pamoja na kunyunyizia dawa kwenye mazalia ya mbu ili kuua viluwiluwi kabla mbu hajafikia hatua ya kuwa mbu pevu ambapo huwa na uwezo wa kuambukiza malaria.

“Ili kuhakikisha dawa zilizopo zote zinafanya kazi huwa tunafanya ufuatiliaji, tunamfuatilia ili kuona iwapo dawa tunazoweka kwenye vyandarua, kupulizia au viuatilifu vyote vinafanya kazi ambayo hufanywa na Taasisi ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu Tanzania (Nimr) na Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) na taasisi nyingine za utafiti hapa nchini.

Alisema mpaka sasa Tanzania inao mbu ambao wanadhibitiwa na dawa zinazowambwa kwenye vyandarua na kuta za nyumba, kutokana na utafiti uliofanywa katika halmashauri 62 kupitia kituo cha Amani kilichopo Muheza, Tanga.

Hata hivyo kutokana na mabadiliko ya mbu huyo ambayo hutokea mara kwa mara kwa kutengeneza mazingira ya kutoathirika na dawa, yameilazimu Serikali kuanza utafiti.

“Mbu mpya ambaye ameshagundulika Kenya, wamemgundua ana sifa sugu kwenye dawa tunazotumia kudhibiti malaria, lakini pia anazaliana kwenye mazingira ambayo yana miundombinu ya mijini sugu kwa dawa zinazodhibiti mbu, anakua na kuzaliana zaidi maeneo ya mijini na anasambaza malaria zaidi,” alisema Dk Lazaro.

Alisema Serikali ina taarifa kupitia taasisi za utafiti na kwamba imeshajipanga baada ya kukutana na wataalamu wa mbu na wadudu wanaodhuru wa malaria na wamejadiliana na kuweka mikakati mbalimbali.

“Tunaongeza mifumo ya ufuatiliaji wa mbu ili kukusanya mbu mijini na vijijini kuangalia ni wa aina gani ili tuweze kujua kama kwetu wapo au hawajaingia ili tujue namna ya kuwadhibiti,” alisema Dk Lazaro.

Wataalamu wa mbu

Mtafiti Kiongozi kutoka Nimr, Kituo cha Amani – Muheza Tanga, Dk William Kisinza alisema mbu huyo tayari yupo Kenya na kwa Tanzania bado hawajajua kama yupo au ni vinginevyo na kwamba tayari wameanza kufanya ufuatiliaji.

“Sisi si kisiwa, uwezekano mkubwa anaweza kuingia wakati wowote au yupo hatujamgundua, ana tabia tofauti sana na wengine, ni mbu ambaye anaeneza malaria kwa kasi katika maeneo ya mijini na vijijini,” alisema.

Alisema mbu huyo hueneza vimelea kwa kasi na anazaliana kwa wingi ukilinganisha na mbu mwingine, iwapo mtu ataugua anaweza kutibiwa lakini bado vimelea vikabaki kwenye ini na hivyo ikaibuka wakati mwingine hata kama hakung’atwa na mbu,” alisema.

Alisema mbu huyo ambaye hasikii dawa za kupambana na malaria, anaifanya dunia inakuwa na wasiwasi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuambukiza kwa kasi.

“Sasa anapokuwa ameingia hata juhudi zilizofanyika na sasa tunakaribia lengo la kutokomeza, zitakwama, inabidi kujiandaa sana, tunaamini nchi zenye hawa mbu zinapaswa kufanya ufuatiaji wa hali ya juu kuhakikisha mazalia yanatokomezwa,” alisema.

Alisema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Nimr wanafanya ufuatiliaji kubaini uwepo wa mbu huyu katika Halmashauri 32 sambamba na kuelimisha jamii.

Akielezea zaidi kuhusu mbu huyo, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Afya ya Mazingira na Ikolojia kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) Dk Emmanuel Kaindoa, alisema mbu huyo ni jamii ya Anopheles lakini ripoti zinaonyesha ni mgeni katika ukanda wa Afrika.

Alisema kwa mara ya kwanza alionekana Afrika mwaka 2012 katika nchi ya Djibout, lakini baadaye ulifanyika utafiti akaonekana pia katika nchi za Somalia, Ethiophia na Eritrea na tafiti zilivyoendelea akaonekana katika nchi ya Sudan mwaka 2019.

Akielezea tabia za mbu huyo, Dk Kaindoa alisema mbu huyo anapenda kuzaliana maeneo ya mijini zaidi ikilinganishwa na vijijini lakini katika mazalia ya mabaki ya vitu kama makontena, vifuu vya nazi, maji yaliyoituama na kwenye mazingira machafu.

Katika namna nyingine alimtaja kuwa ni mbu anayependa tabia za mbu wale wasioeneza ugonjwa wa malaria pamoja na tabia za mbu anayeeneza ugonjwa wa dengue.

Dk Kaindoa ambaye pia ni Mkuu wa idara inayohusika na utafiti wa mbu na malaria, alisema mbu huyo ni tofauti na wengine kwa sababu pia anaweza kueneza aina mbili za ugonjwa huo.

Alisema anapong’ata kwenye vimelea anavichukua vinakaa mwilini mpaka siku 10 baadaye ndiyo anaeneza malaria.

“Mbu huyu anaweza kubeba vimelea vya aina mbili, ukiangalia inaleta shida namna ya kuvitibu, ni hatari sana na malaria yake ina tabia ya kujificha na kuwa na ile malaria ya ghafla.

“Tabia nyingine aliyonayo anaweza akala kwa binadamu na kwa viumbe vingine ambavyo si binadamu, tabia inayomfanya awe tofauti, lakini kwa tafiti zilizofanyika Misri na Djibout anaweza kueneza malaria kwa kiwango kikubwa.

“Mbu huyu vamizi anapomng’ata binadamu mwenye vimelea anaweza kupata maambukizo na kukua mwilini mwake, lakini kuwa na uwezo wa kung’ata na kuambukiza baada ya siku 10,” alisema Dk Kaindoa.

Alisema mbu huyo akichukua damu kwa binadamu hukaa siku tatu na kisha hutaga mayai na siku ya nne hurudi tena kutafuta damu nyingine, hapo atamwambukiza mwingine na huishi kwa siku 30 ambapo huenenda na mzunguko huo mpaka anapokufa na kwamba hutaga mayai 300 kwa wakati mmoja.

Mwongozo WHO

Mwaka 2019 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa mwongozo wa nini nchi zinapaswa kufanya ili kupambana na mbu huyo vamizi mwenye madhara zaidi.

Miongoni mwa maelekezo hayo iliagiza kushirikiana nchi kwa nchi, hasa maeneo ya mipakani, kuongeza nguvu katika ufuatiliaji wa mbu, ubadilishanaji wa taarifa, kutoa taarifa na kuweka vipaumbele katika kupambana na ugonjwa huo.

“Wenzetu Kenya walikuwa wanafanya ufuatiliaji ndipo walipobaini uwepo wa mbu hao, lakini tafiti zetu Tanzania bado hatujabaini kama yupo au atakuja baadaye, mbu ni mgeni ikolojia yake haijasomeka vizuri,” alisema Dk Kaindoa.

Hali ilivyo Zanzibar

Akizungumzia tishio la mbu huyo mpya, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Mazrui alisema kisiwa hivyo kinatumia wataalamu watafiti kuhakikisha wagonjwa wote wanaopatikana na malaria wanafuatiliwa.

Alisema kwa sasa ugonjwa huo upo chini ya asilimia moja, kwani walishafanikiwa kutokomeza malaria ambayo hapo awali iliathiri sana watoto na kinamama, hasa wajawazito.

Waziri Mazrui alisema matokeo ya utafiti wa wataalamu yanaonyesha vimelea kwa sasa havitoki Zanzibar, vingi vinatoka katika nchi jirani.

“Wafanyabiashara wanaotoka nchi jirani ndiyo wanaleta malaria na wale wanaokuja kutoka nje, tukizungumza na wagonjwa tunagundua ni wale ambao walisafiri kwenda nje au walipata mgeni kutoka nje,” alisema.

Mazrui alisema pindi wanapogundua mgonjwa huenda eneo analotoka na huchukua hatua za kuangamiza vimelea kwa kupuliza dawa ili kuua mazalia.

“Mbu ambaye hasikii dawa sisi Zanzibar tayari tuna maabara nzuri, tunapima majibu yote yaliyokutwa na vimelea vya ugonjwa huo kubaini kama ni aina hiyo ya mbu, kwetu ni rahisi kuingia kupitia Pwani ya Mombasa kuja Zanzibar ya Pemba.

“Mpaka sasa hatujapata hiyo aina ya mbu ambaye hasikii dawa na wote wenye malaria wanatibiwa na kupona na tumeanza kupiga dawa kwenye madimbwi ya maji ili kuzuia asiingie nchini,” alisema Mazrui.

Tabia za mbu

Anopheles stephensi ni aina ya mbu aenezaye malaria ambaye hawezi kuuawa na aina yoyote ya dawa ya viuatilifu, kwa maana ya dawa ziwekwazo kwenye vyandarua, za kupuliza na aina nyinginezo na kwamba hadhibitiwi na chanjo.

Stephensi ameacha madhara mengi katika miji ya India. Hata hivyo, mbu huyu ametajwa kugawanyika mara mbili kulingana na tofauti katika vipimo vya mayai na idadi ya matuta kwenye mayai yake ambayo imetajwa zaidi kuwepo mijini.

Aina nyingine imetajwa kuwepo katika maeneo ya mashambani, vijijini na maeneo ya pembezoni mwa miji, ingawa hali yake ya vekta haijulikani.

Kwa mujibu wa WHO, takriban asilimia 12 ya wagonjwa wa malaria nchini India wanapatikana na ugonjwa uliosababishwa na aina hii ya mbu.

Novemba mwaka 2015, kikundi cha utafiti cha Marekani kiligundua mbu huyo aliye na mabadiliko ya kijeni anaweza kupunguzwa uwezo wa kusambaza malaria, na kwamba asilimia 99.5 ya watoto wa mbu waliobadilika pia walikuwa na kinga.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi