Kitaifa
Mhasibu wa benki atekwa, auawa kwa kuchomwa moto
Pwani. Jeshi la Polisi mkoani Pwani limethibitisha kutokea kwa kifo cha Martha Towo (30) ambaye aliuawa kwa kuchomwa moto baada ya kutekwa usiku wa Machi 3 mwaka huu wilayani Kibaha.
Martha ambaye ni mkazi wa Mbonde na Mhasibu wa Bank of Africa (BOA) tawi la Kahama aliuawa kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana baada ya kwenda kwao Kibaha kwa ajili ya kuwasalimia wazazi wake.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutumo amesema tukio hilo lilitokea Machi 3 mwaka huu baada ya kutekwa nyara majira ya saa 4:30 usiku na baadaye alikutwa akiungua maeneo ya Mitamba kata ya Pangani.
“Watu wasiojulikana walimteka kisha kummwagia Petroli na kumchoma moto” alisema Lutumo.
Baada ya taarifa za wasamaria wema polisi walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wake kisha wakaupeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi.
Aidha Kamanda Lutumo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika na wanaendelea na uchunguzi zaidi.