Kitaifa
Saba wafariki dunia wakichimba dhahabu kinyemela usiku
Geita. Wachimbaji wadogo saba wamepoteza maisha mkoani Geita baada ya shimo waliloingia kujaa maji na wao kushindwa kutoka.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha tukio hilo na kusema limetokea usiku wa kuamkia leo Machi 11, 2023 saa 9:30 usiku katika Kijiji cha Igando, Kata ya Magenge wilayani Geita.
Kamanda Jongo amesema wachimbaji hao walikuwa wanachimba eneo lililofungwa kwa sababu za kiusalama lakini wao waliingia kinyemela usiku.
“Utaratibu uliofanyika wakafunga migodi ambayo haikuwa vizuri kiusalama na hizi mvua zinazonyesha mashimo yalijaa maji, kumbe kuna watu walikuwa wanaingia usiku na walivyoingia wakazidiwa na maji wakashindwa kutoka,” amesema.
Kwa mujibu wa kamanda tayari wachimbaji wote wameopolewa na kutambuliwa na ndugu zao.
Mkuu wa Mkoa wa Geita na viongozi wa usalama wako njiani kwenda eneo la tukio.