Kitaifa

Kesi ya kina Mdee: Dk Lwaitama adai 2020 mamlaka zilikengeuka

Dar es Salaam. Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Dk Azaveli Lwaitama amedai wakati wa utawala wa hayati John Magufuli mamlaka zilikengeuka.

Dk Lwaitama alieleza hayo jana wakati akihojiwa na Wakili Ipilinga Panya katika kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama iliyofunguliwa na Halima Mdee na wenzake 18.

Wakili Panya anayewawakilisha Mdee na wenzake aliomba wajumbe wa bodi hiyo waitwe ili wahojiwe ili wafanyiwe dodoso kwa lengo la kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa kuwa ndiyo wanaoshtakiwa kwa niaba ya Chadema.

Akiongozwa na Wakili Panya, Dk Lwaitama alipoulizwa kama anawafahamu waleta maombi (Mdee na wenzake), alidai walikuwa ni wanachama wa Chadema na walishafukuzwa na mamlaka kutokana na kuapishwa kuwa wabunge na aliyekuwa Spika wa wakati huo Job Ndugai.

Alisema chama hicho hakikuhusika na walishangaa kuona wabunge hao wanaapishwa.

Alipoulizwa kuhusu Katiba ya Tanzania inasemaje hukusu mamlaka ya uteuzi huo, mwanazuoni huyo kwa falsafa alidai wakati wa utawala wa hayati Magufuli mamlaka hizo zilikengeuka.

“Wakati wa utawala wa Magufuli mtu ulikuwa unaweza kutangazwa kuwa mbunge hata kama hujateuliwa kwa kuwa mamlaka zilikengeuka,” alidai Dk Lawitama.

Alidai katika mazingira ya kuaminiwa ya kawaida ambayo si ya 2020, Spika wa Bunge huapisha wabunge baada ya kupokea majina kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“Katiba ya Jamuhuri ya Muungano naiheshimu, ndiyo maana nashangaa kuna watu wako bungeni, ziko mamlaka kwenye chama zilishautaarifu umma kuwa taratibu za kuteuliwa kwao hazikufwatwa na sisi tukapata taharuki,” alisema.

Mahojiano zaidi yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Panya: Umejiunga lini Chadema?

Lwaitama: Mwaka 2015

Panya: Ulikuwa na nyadhifa gani nyingine?

Lwaitama: Sikuwa kiongozi yeyote kabla ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini Mei 2022 wakati wa kikao cha Baraza Kuu.

Panya: Ilikuwa tarehe ngapi?

Lwaitama: Nadhani tarehe 11/5/2022 ndio niliteuliwa na Baraza Kuu

Panya: Kwenye chama chako cha Chadema kuna miongozo?

Lwaitama: Bila shaka ipo, ni utaratibu wa taasisi yoyote.

Panya: Huo utaratibu mnaufuata?

Lwaitama: Ndio unafuatwa maana mtu anakubali kuwa kwenye taasisi lazima akubaliane kuanzia salamu na itifaki na akitaka kutoka hiari yake.

Panya: Hiyo miongozo inafuatwa na wanachama?

Lwaitama: Ndiyo inafuatwa, ni miongozo ya chama, lakini kwangu kusema mambo jumla jumla si sahihi

Panya: Mfano mimi nikitaka kujiunga (Chadema) lazima nifuate miongozo?

Lwaitama: Ndiyo, ni hiari yako kujiunga lakini ukishakuwa mwanachama usipoifuata chama kinakutenga.

Panya: Una ufahamu wa kuna haki ya kusikilizwa?

Lwaitama: Ndiyo, mimi nilipokuwa mwalimu mwanafunzi akikosea tunamwita na kumsikiliza

Panya: Unasema tarehe 11.5.2020 uliteuliwa kuwa nani?

Lwaitama: Niliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini kwenye Baraza Kuu

Panya: Unajua kuna kiapo kinzani?

Lwaitama: Ndiyo najua, nililetewa na mimi kabla ya kusaini chochote huwa nasoma

Panya: Kwa hiyo kiapo kinzani uliletewa, wewe hukuandika wewe?

Lwaitama: Nani kasema kuwa hakukiandika?

Panya: Nikuonyeshe ili uhakiki kwamba ni chenyewe?

Lwaitama: kwa nje ni chenyewe sijasoma kwa ndani nitajuaje kama kuna page umechomeka?

Panya: Hao wabunge 19 walioleta rufaa unawahamu?

Lwaitama: Ndiyo (anawataja huku akifafanua mmoja baada ya mwingine)

Panya: Hao wabunge 19 wapo wapi?

Lwaitama: Walishafukuzwa maana walikiuka taratibu za chama kwa kupeleka majina, wao wakaenda kuapishwa na Ndugai

Panya: Waliapishwa kuwa nani?

Lwaitama: Waliapishwa bila mamlaka zao kuwatangaza, ni kwamba watu walishangaa kuona wanaapishwa.

Panya: Waliapishwa na nani?

Lwaitama: Tuliona watu wanaapishwa na Ndugai nje ukumbi.

Panya: Nani aliwatangaza kuwa wabunge?

Lwaitama: Nchi hii wakati wa Magufuli mamlaka zilikengeuka

Jaji: Swali ni kuwa nani aliwateua?

Lwaitama: Wakati wa Magufuli mambo yalikuwa ovyo kulikuwa hakuna utaratibu

Wakili Ukashu: Mheshimiwa jaji, shahidi anataja marehemu.

Wakili Kibatala: Huyu shahidi nyie ndio mlimwita, kwa hiyo muwe wavumilivu kutaja Magufuli kuna tatizo gani?

Wakili Panya: Nani ana mamlaka ya kutangaza mbunge?

Lwaitama: Kuna taratibu kutoka chama chao

Panya: Mwaka 1995 kuna wabunge waliteuliwa, nani aliwateua?

Lwaitama: Katika mazingira ya kawaida ya kuaminiwa ambayo siyo ya 2020 ni Spika wa Bunge baada ya kupokea majina kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Panya: Ukiwa raia unapaswa kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977?

Lwaitama: Naiheshimu, ila nashangaa kuna watu wapo bungeni hawana chama

Panya: Nakupa Katiba ya Jamhuri Muungano nisomee ibara ya 85(a)

Lwaitama: (Anasoma ibara hiyo kwa kukwama)

Jaji: Wakili Panya msomee (anamsomea)

Panya: Kwa mazingira ya kawaida nani anateua majina?

Lwaitama: Kwa mazingira hayo wakati huo hapana, unanilazimisha niseme kuwa Chadema waliteua unanitega hapo.

Jaji: Wakili sheria haiko hivyo, shahidi kategua mitego yako

Panya: Taratibu zikoje kuteua majina?

Lwaitama: Zipo wazi ila tulishangaa watu wanajipeleka kujiapisha

Panya: Kwenye affidavit yako (hati ya kiapo) na kiapo kinzani chako kuna maelezo yako, hebu soma

Lwaitama: Hiyo lugha iliyotumika ni ya kisheria

Panya: Hayo maandishi ni ya kwako?

Lwaitama: Mwanasheria kaajiriwa na chama kakuletea ujaze, utakataa?

Panya: Nakwambia uko mbele utakuja kuona

Wakili Kibatala: Mheshimiwa jaji wakili anamtisha shahidi

Panya: Nakuonyesha kiapo kinzani chako aya 40.3. hayo maneno umeyasema kutoka kikao cha Baraza Kuu.

Wakili Panya: Mheshimiwa, jaji tumekubaliana juu muda nikimaliza tuendelee kesho

Jaji: Profesa leo tuishie hapa tukutane kesho asubuhi, utaweza?

Lwaitama: Mimi naiheshimu mahakama, nitakuwepo

Baada ya kauli hiyo Jaji aliahirisha kesi hadi leo itakapoendelea

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi