Kitaifa

Uzembe, mwendokasi vyatajwa ajali iliyoua 10

Geita. Mwendokasi wa gari pamoja na dereva kuongea na simu wakati akiendesha, vimetajwa kuwa sababu ya ajali iliyotokea mkoani Geita juzi na kusababisha vifo vya watu 10 na majeruhi 49.

Ajali hiyo ni ya pili katika kipindi kisichopungua wiki moja ambapo ajali nyingine ilitokea Machi 6 na kusababisha vifo vya watu tisa na majeruhi 30 baada ya gari inayofanya safari zake kutoka Kigoma kwenda Mpanda kuacha njia, kisha kupinduka.

Ajali hiyo iliyohusisha basi la Shertaon linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Ushirombo Wilaya ya Bukombe ilitokea juzi, eneo la Ibandakona wilayani Geita na kusababisha vifo vya watu 10 akiwemo mwandishi wa gazeti la Nipashe, Richard Makore na majeruhi 49.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa Geita, Dk Mfaume Salum akizungumza na Mwananchi jana alithibitisha kupokea miili hiyo na watu tisa walifariki eneo la ajali na mmoja alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita.

Alisema majeruhi wanne ambao hali zao hazikuwa nzuri wamepewa rufaa kwenda Hospitali ya Kanda Bugando kwa matibabu zaidi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay alisema chanzo cha ajali ni tairi ya mbele ya gari kupasuka na kusababisha gari kutumbukia kwenye korongo na kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha dereva alikuwa kwenye mwendokasi.

Akizungumza baada ya kutembelea majeruhi waliolazwa hospitalini hapo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amelitaka Jeshi la Polisi kuchunguza na kukagua vyombo vya usafiri kama vinafaa kuendelea na safari na vile visivyo na sifa vifungiwe hadi vitakapofanyiwa marekebisho .

Pia amelitaka jeshi hilo kuwakagua na kuwachukulia hatua madereva wanaoendesha kwa mwendokasi barabarani, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Majeruhi wasimulia

Mmoja wa abiria aliyekuwa kwenye gari hilo, Pascal Sengerema, alisema dereva alikuwa kwenye mwendokasi na alikuwa akizungumza na simu mara kwa mara akitaka kuwahi, ili akangalie mechi kati ya timu ya Simba na Vipers ya Uganda iliyokuwa ikionyeshwa kwenye televisheni kutoka Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Alisema wakiwa kwenye safari hiyo ghafla walisikia kishindo na gari kutumbukia kwenye korongo.

“Baada ya kutoka Sengerema gari ilikua inaenda kwa kasi, lakini hatukuwaza ajali na dereva alikuwa anaongea na simu mara kwa mara na ghafla nilisikia kishindo na gari likahama ikaingia kwenye korongo tuliokuwa nyuma hatukuumia sana ndiyo tukajisaidia kutoka na kusaidia wenzetu na kuokota simu za watu baadaye ndiyo tukaanza kuletwa hapa hospitali,” alisema Sengerema.

Gires Rweyemamu aliyekuwa kwenye gari hiyo alisema alipanda gari stendi ya Sengerema, licha ya kuona gari hilo limejaa lakini alipanda ili awahi alikokuwa akielekea.

“Madereva wasijaze sana abiria na waende mwendo wa kawaida, ingekuwa haina mwendokasi hata pancha iliyotokea ajali isingekuwa mbaya kiasi kile,” alisema.

Stephano Nyamsekela, alisema kuna uwezekano gari lilikuwa bovu kwa kuwa tangu wanaanza safari lilikuwa likipiga kelele mbele na hakuna aliyezungumzia hali hiyo hadi walipopata ajali.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Geita, Edward Nyaulingo aliwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri barabarani kutoruhusu chombo kuingia barabarani bila kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Nyaulingo pia aliwataka madereva waache uzembe, mwendokasi na wasikubali kuendesha magari mabovu kwa kuwa ni hatari kwao na abiria wanaowabeba.

Alisema wataendelea kutoa elimu kwa abiria na madereva, ili kupunguza ajali zisizo za lazima zinazotokea mara kwa mara.

Nyaulingo aliwataka abiria kuwa wepesi kutoa taarifa kwa askari waliopo barabarani au kutumia namba za polisi zilizoko kwenye magari, ili madereva wazembe wachukuliwe hatua kabla ya kusababisha ajali.

“Abiria wetu nao wasikubali kunyamaza kimya wanapoona dereva anafanya uzembe au amefanya uzembe, hii tabia ya kusubiri mpaka tatizo litokee ndipo waeleze kuwa dereva hakuwa anafuata sheria za usalama barabarani haitusaidii kwa kuwa tunakuwa tumeshapoteza ndugu, tumezalisha majeruhi na uharibifu wa mali” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi