Connect with us

Kitaifa

Chadema: Tuko tayari

Moshi/ Dar. Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) limesema chama hicho kimejipanga kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu ujao ili watatue changamoto zinazowakabili Watanzania.

Akizungumza katika mkutano wa Bawacha uliohudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan mjini Moshi jana, Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Sharifa Suleiman alisema kina mama wa chama hicho wamejiandaa kupambana.

“Tunataka kutatua changamoto zinazotukabili Watanzania ndani ya miaka 62 kwa sasa ambazo zimeshindwa kupatiwa ufumbuzi,” alisema Sharifa.

“Wanawake sio tu jeshi kubwa, lakini tumejiandaa na tuko tayari kuongoza kuhakikisha Chadema inashika hatamu.”

Alisema wingi wa wanawake waliojumuika jana katika maadhimisho hayo ni dhahiri wako ‘serious’ kushika dola na kurejesha heshima ya Taifa la Tanzania.

Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge alimwomba Rais Samia kuandika historia itakayosomwa na vizazi vyote kwa kuwezesha upatikanaji wa Katiba mpya.

“Tunafahamu unafanya jitihada kubwa na Mwenyekiti Mbowe (Freeman) kuhakikisha tunapata Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi kabla ya mwaka 2025, usiogope hujuma za wanaotaka ushindwe kama wao walivyoshindwa huko nyuma,” alisema Catherine.

“Ukichunguza vizuri mheshimiwa Rais hata hao wanaopinga dhamira yako ya kupata Katiba mpya hawakupingi, bali wanakupima, ni wakati wako sasa kuandika historia ambayo itasomwa vizazi vijavyo.”

Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, John Mnyika alisema nchi ni ya wananchi, lazima wakati wote vyama vikuu viwasikilize na kutekeleza matakwa yao.

“Watanzania wanalia hali ngumu ya maisha, Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Safari mliyoianza kuanzia Mwenyekiti Mbowe (Freeman) alipotoka gerezani ya kuliunganisha Taifa naamini ikiendelea tutafika katika nchi tunayoitafuta,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu alitumia mkutano huo kushitaki kitendo cha kuzuiwa kuotesha miche ya matunda katika Shule ya Sekondari Kiboriloni iliyopo Manispaa ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.

“(Machi 3) Tulifuata taratibu zote za maandalizi. Tulipofika Moshi tulikutana na upinzani mkubwa katika Shule ya Sekondari Kiboriloni, tulifanyiwa unyanyasaji, tulinyimwa kuotesha miti tuliyonunua kwa fedha zetu kutoka mifukoni mwetu,” alisema Kiwelu.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alimtoa hofu Kiwelu akisema yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Shamrashamra Moshi

Maadhimisho hayo yalitanguliwa na maandamano ya wanawake kuanzia soko kuu la kati mjini Moshi hadi ukumbi wa Kuringe, huku maandamano hayo yakishinikizwa na kilio cha Katiba mpya.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi na makada mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Mwenyekiti wa Mkoa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa mkoa huo, Elizabeth Minde na baadhi ya wabunge wa chama hicho.

Baadhi ya wabunge waliokuwepo ni wa Moshi mjini (CCM), Priscus Tarimo na wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela, huku karibu wanawake 100 wa chama hicho wakihudhuria ufunguzi huo.

Kwa jumla, mji wa Moshi ambao uko katika mkoa unaotajwa kuwa moja ya mikoa ambayo ni ngome ya upinzani, ulionekana kurejesha uhai wake wa kisiasa uliozoeleka kuanzia mwaka 1995 hadi ziliposinzia baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Katika Barabara Kuu ya Himo-Bomang’ombe maeneo yalipokuwa yakifanyika maadhimisho hayo kulionekana bendera za Chadema na CCM, huku mitaani kukiwa na wanachama wa Bawacha wakiwa na mavazi rasmi ya chama.

Moja kati ya mambo yaliyokuwa kivutio kikubwa na kuvuta hisia za wachangiaji wengi katika mitandao ya kijamii ni picha zilizokuwa zikionyesha makada wa CCM, akiwamo Minde, wakipeperusha bendera zenye nembo ya Chadema ukumbini. Utambulisho wa mbunge wa zamani wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema uliibua furaha ukumbini, shangwe, nderemo na vifijo.

Maoni mengine

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha St Joseph Dar es Salaam (SJUIT), Dk Kassim Nihuka alisema kinachofanywa na Rais Samia ni dhana mpya kuiona katika siasa hasa za nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Rais Samia amejipambanua kufanya siasa zake akijenga umoja wa kitaifa, mimi nauona ni mwelekeo mzuri na unajenga mustakabali mzuri wa taifa,” alisema Dk Nihuka.

Hata hivyo, alisema kwa siasa zinazofanywa na mkuu huyo wa nchi iwapo vyama vya upinzani havitapambanua mambo kwa kina vitajikuta vinamalizwa taratibu.

Hoja yake hiyo inatokana na kile alichokisema kuwa, wakati mkuu huyo wa nchi akihudhuria mikutano ya wapinzani kuwafurahisha, humohumo anapenyeza ajenda zake za kuendelea kusalia madarakani.

“Bila shaka kwa kufanya hivyo wapo atakaowavua watamuunga mkono, akiwa kwenye mkutano huo aliwaambia waziwazi kuwa sioni kwenye nyuso zenu kwamba mnataka kuongoza 2025 maana mnajua mama yupo,” alisema.

Mwanasiasa Mkongwe, Dk Wilbroad Slaa alisema ni tukio la kihistoria katika siasa za Tanzania kwa kuwa muda mrefu haikuwahi kutokea ushiriki wa mkuu wa nchi kwenye mikutano ya vyama vya upinzani.

“Hili linaturudisha kule kwenye ukweli kwamba siasa si uadui, ni urafiki pamoja na utofauti wa sera na ilani kati ya chama kimoja na kingine,” alisema.

Dk Slaa, ambaye hivi karibuni ameonekana akipanda kwenye majukwaa ya Chadema tangu alipokiacha chama hicho mwaka 2015, alisema inawashangaza wengi kwa kuwa ulifika wakati siasa ilichukuliwa kama uadui na si tofauti ya mitazamo kama inavyotakiwa.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Janeth Joseph na Florah Temba (Kilimanjaro) na Juma Issihaka (Dar).

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi