Kitaifa
Utata madai ya Sheikh kufia gereza la Ukonga
Dar es Salaam. Utata umegubika kifo cha Sheikh Said Ulatule (80), anayedaiwa kufariki dunia akiwa katika gereza la Ukonga jijini hapa, huku uongozi wa Magereza mkoa ukisema kuwa haufahamu tukio hilo.
Sheikh Said, aliyeshikiliwa katika gereza la Ukonga kwa tuhuma za ugaidi inaelezwa kwamba alifikwa na umauti wakati akiwasilisha kero zake kwa Jaji wa Mahakama Kuu, Salma Magimbi aliyefika gerezani hapo kusikiliza changamoto wanazopitia.
Inadaiwa kwamba baada ya wenzake kuwasilisha kero zao na Sheikh Said naye kutakiwa kueleza yanayomsibu gerezani hapo, alisimama na kushindwa kuongea na hatimaye kuanguka chini.
Akizungumza jana na Mwananchi kwenye mazishi ya Sheikh Said yaliyofanyika Kata ya Kivule, mtaa wa Magole A, makaburi ya Nyang’andu, mtoto wa marehemu, Mohamed Said alisema baba yake alifia gereza la Ukonga alikokuwa akishikiliwa kwa tuhuma za ugaidi.
“Baba alifariki dunia gereza la Ukonga na ameacha watoto sita na mke mmoja na hapa alipozikwa ni kwa mwanaye,” alisema.
Pamoja na kwamba tukio hilo linaripotiwa kutokea kwenye gereza la Ukonga, Mwananchi ilipomtafuta Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, George Wambura alisema halifahamu tukio hilo.
Hata hivyo, baadaye alipopigiwa tena simu saa 11 jioni, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa simu na kumtaka mwandishi kufika ofisini kwake leo.
Mwananchi lilipomtafuta Mkuu wa Gereza la Ukonga, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Josephat Mkama na kumuuliza kuhusu kifo hicho alisema: “Sasa kama kafia Gereza la Ukonga nisiwe na taarifa? Si unakuja ofisini, nitajuaje kama wewe ni mhusika?”
Huku akiendelea kusisitiza kuwa hafanyi kazi kwa simu, Mkama alisema, “Kwani mtu anastahili kufia wapi? kwamba sehemu fulani ndio sahihi? Kwa hiyo kama nilivyokwambia, mimi siwezi kufanya kazi kwa simu.”
Akisimulia tukio la kifo cha Sheikh Said, Katibu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda alisema kifo cha Sheikh huyo kilitokea Machi 4, mwaka huu gerezani hapo.
Alisema siku hiyo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Salma Magimbi alifanya ziara katika gereza la Ukonga Dar es Salaam kwa lengo la kusikiliza kero na shida za wafungwa na mahabusu.
“Baada ya jaji kuwasikiliza wafungwa iliwadia zamu ya mahabusu, wakiwemo Waislamu wanaotuhumiwa kwa madai ya kufanya vitendo vya ugaidi, hawa ni mahabusu wa kidini wanaoshikiliwa katika magereza mbalimbali nchini kwa muda kati ya miaka sita hadi 10 bila kupewa haki ya kujitetea.
“Katika kikao hicho, Sheikh Said Ulatule aliinua mkono na jaji alimpa fursa ya kueleza shida zake, hata hivyo hakuweza kusema lolote, bali alianguka na kufariki papohapo mbele ya jaji, wafungwa na askari wa magereza,” alidai Sheikh Ponda.
Baada ya kutokea tukio hilo Machi 4, Sheikh Ponda alisema Machi 6 mwaka huu, Shura ya maimamu wakiongozwa na Sheikh Ponda, walifika gerezani hapo na kufanya mazungumzo na uongozi wa gereza na gereza lilimteua ofisa wake aliyepewa jukumu la kushirikiana na viongozi hao wa dini kupata taarifa za uchunguzi za kifo.
Kutokana na ripoti hiyo, Sheikh Ponda alisema walikabidhiwa mwili wa marehemu ambao ulifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Sheikh Ponda alisema majibu ya daktari baada ya uchunguzi huo yalionyesha Sheikh Said aliathiriwa na shida ya mshtuko wa moyo ambao ulishindwa kufanya kazi.
Alisema Shura ya Maimamu ilikabidhiwa mwili huo juzi, saa 11:00 jioni na waliuhifadhi katika chumba cha maiti kilichopo katika makaburi ya Mwinyimkuu Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Kutokana na tukio hilo, Sheikh Ponda ameitaka Serikali kuangalia kama ni sahihi kwa vyombo vya dola kuendelea kuwakamata na kuwaingiza watu gerezani kwa muda au miaka waitakayo.
Alisema; “Utaratibu wa kufuta kesi za hawa masheikh ulikuwepo, lakini baadaye ukasita, mpaka sasa katika gereza la Ukonga kuna masheikh 70, wengine 23 wapo mkoani Arusha, 23 mkoani Tanga na 21 Morogoro.”