Kitaifa
Mbowe ataja masharti Dk Slaa kurejea Chadema
Arusha/Dar. Wakati vuguvugu la Dk Wilbroad Slaa kurejea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) likishika kasi, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema hajapokea taarifa yoyote kuhusu kiongozi huyo wa zamani kurejea.
Hata hivyo, Mbowe ametaja masharti ya kurejea kwa mwanachama yeyote aliyewahi kushika wadhifa wa juu na kuondoka kwa kukikashifu chama hicho, anapaswa afanye uungwana wa angalau kuzungumza na viongozi.
Kauli hiyo ya Mbowe inakuja ikiwa ni siku nane tangu Dk Slaa ambaye ni katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema aonekane akizungumza na wanachama wa chama hicho wilayani Karatu.
Septemba mosi, 2015, Dk Slaa alitangaza kuondoka ndani ya chama hicho na kustaafu mambo ya siasa akiwa ndani ya vyama, kwa kile alichoeleza kuwa hakuridhishwa na mwenendo wa Chadema.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Mbowe alisema chama cha siasa ni chombo cha watu, hivyo kina uwezo wa kuwapokea na kuwaachia akisisitiza: “Hakuna urafiki au uadui wa kudumu katika siasa.
“Kwa mtu ambaye alikuwa kiongozi mwandamizi ndani ya chama chetu ujio wake hauwezi kuwa sawasawa na mwanachama wa kawaida, lakini sisi hajatufikia.
“Kazungumza na wananchi kule Karatu kamaliza ametoa kauli kali kali saa nyingine dhidi yetu, saa nyingine kutuunga mkono, yote hayo ni mambo ya kibinadamu ya kimaisha, maisha lazima yaendelee,” alisema.
Lakini alisema angetamani kwa wanachama walioondoka kwa kashfa na kukidhalilisha chama hicho, wanapotaka kurejea watafute uungwana wa kuzungumza na viongozi na kutoa taarifa.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kutokana na mfumo wa chama hicho ni vigumu kubaini kama Dk Slaa ni mwanachama ama la.
“Kwa sasa tupo kidigitali, mtu akiwa na simu yake nyumbani anaweza kujiunga na chama bila wewe kujua, kwa hiyo kuthibitisha kama ni mwanachama au la ni ngumu,” alisema.