Kitaifa
Sababu za Lissu kurejea tena Ubelgiji
Dar es Salaam. Wiki mbili baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu kurejea nchini Ubelgiji, ameliambia Mwananchi atarejea nchini baada ya kupata visa yake Machi 19.
Lissu alirudi nchini Januari 25, mwaka huu akitokea Ubelgiji alikokwenda tangu Novemba 2020 akihofia usalama wake, ikiwa ni mwezi mmoja tangu kumazika kwa Uchaguzi Mkuu.
Katika uchaguzi huo, Lissu alikuwa mgombea urais akichuana na wagombea wengine, akiwemo John Magufuli wa CCM aliyekuwa akitetea nafasi hiyo. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza Magufuli mshindi.
Lissu alirejea nchini baada ya kuishi huko tangu Januari 2018 alikopelekwa kwa matibabu akitokea Nairobi nchini Kenya, baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mchana wa Septemba 7, 2017.
Januari 25, Lissu alirejea tena nchini na kupata mapokezi makubwa jijini Dar es Salaam na siku hiyo alifanya mkutano wa hadhara Temeke. Februari 15, mwanasiasa huyo aliondoka tena kwenda Ubelgiji na kuibua mijadala sehemu mbalimbali wakihoji sababu za kuondoka kwake. Akizungumza na Mwananchi, Lissu alisema alilazimika kurudi Ubelgiji kukutana na daktari wake na kuhuisha visa yake iliyokwisha muda wake.
“Nimeshangaa kusikia mjadala huu wa bure kabisa, mimi wala sikai sana huku.
“Fikiria hali yangu ya kiafya, nilisema nakwenda kuonana na daktari wangu aliyenitibu kwa miaka mitano, ndiye daktari mwenye kumbukumbu zangu zote,” alisema.
Kuhusu visa, alisema baada ya kuonana na daktari wake anafuatilia kupata visa ya Schengen itakayomwezesha kutembelea nchi 33 za Ulaya. “Nimeshapata appointment (wito) Machi 19 asubuhi kwenda kufanya mahojiano ya visa, nilifanikiwa na ninaamini nitafanikiwa, nitarudi mara moja Tanzania,” alisema na kuongeza:
“Siwezi nikakaa huku wakati bado nina kazi nyingi Tanzania, lakini hata nikija huko nitakuwa ninatoka. Hii visa ninayopata inaniwezesha kutembelea nchi 33 za Ulaya, ni jambo jema kwa chama chetu,” alisema.
Lissu alirudi nchini kwa mara ya kwanza kutoka Ubelgiji Julai 2020 kwa ajili ya kugombea urais kupitia Chadema.
Baada ya uchaguzi huo, Lissu alidai kutishiwa maisha na kuhamia kwenye makazi ya Balozi wa Ujerumani nchini kabla ya kuondoka Novemba 2020. Awali, Msaidizi wa Lissu, David Jumbe aliliambia Mwananchi Februari 17, 2023 kwamba kiongozi huyo amekwenda Ubelgiji kuonana na daktari wake kwa vipimo vya kawaida pamoja na kuhuisha visa yake inayomaliza muda wake leo Ijumaa.