Kitaifa
‘Aliyetekwa’ apatikana akiwa hai
Dar es Salaam. “We found him. He’s back and alive’ (Tumempata, amerudi akiwa hai). Hayo ni maneno ya mmoja wa ndugu wa Maliki Rukonge, aliyedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana siku 31 zilizopita.
Maliki alichukuliwa na watu wasiojulikana waliokuwa na gari linalotajwa kuwa Toyota Land Cruiser lenye mkonga, dukani kwake, eneo la Korogwa Dundani Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani saa 3 usiku.
Ndugu walianza kumtafuta maeneo mbalimbali bila mafanikio na gazeti hili kwa mara ya kwanza Februari 13, mwaka huu liliripoti habari hiyo na Jeshi la Polisi lilisema lina taarifa na wanachunguza tukio hilo.
Hata hivyo, jana Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Rufiji, Protas Mutayoba alipoulizwa kwa simu alisema hana taarifa za kupatikana kwa Maliki.
“Bado hatujaletewa taarifa hiyo. Pengine hao waliowapa taarifa wangekuja kuripoti Polisi kwa sababu wao ndio walikuja kutoa taarifa kwamba ndugu yao amepotea, basi waje ili tusije tukatumia nguvu kubwa,” alisema.
Maliki amepatikana wakati watu wengine waliopotea katika mazingira ya kutatanisha wakiwa hawajarudi mpaka sasa.
Miongoni mwao ni aliyekuwa mwandishi wa Mwananchi wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani, Azory Gwanda aliyechukuliwa na watu wasiojulikana Novemba 2017 na hajapatikana hadi sasa.
Mwingine ni aliyekuwa kada wa Chadema, Ben Saanane aliyetoweka Novemba 14, 2016 na ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kuonekana ofisi za makao makuu ya Chadema yaliyopo Mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni.
Akizungumzia kurejea kwa ndugu yake jana, ndugu huyo alisema Maliki alirudi mwenyewe akiwa na majeraha.
“Tulimuuliza akasema hao watu walimpa nauli, kwa hiyo alimwita bodaboda mmoja akaja kumchukua akarejea nyumbani kwake,” alisema.
Hata hivyo, alisema Maliki alitishwa na watu hao wakimtaka kutozungumza yaliyompata.
“Bado ana majeraha na alipelekwa hospitali, ila tumemficha kwa sababu tuna hofu hao watekaji wanaweza kurejea,” alisema bila kueleza maficho hayo.
“Mimi niko safarini, nitakaporudi tunaweza kumwona, lakini kwa sasa tumwache apumzike,” alisema.
Awali, Kamanda Mutayoba aliliambia Mwananchi kuwa wanawashikilia watu watatu, akiwemo ofisa wa Polisi kuhusu tukio hilo.
“Tunaendelea na uchunguzi, tumeshawahoji watu walioshuhudia tukio na wameandika maelezo yao na kuna watu wanaoshukiwa pia tumewakamata. Mpaka sasa tunashikilia watu watatu,” alisema.
Tukio lilivyokuwa
Inaelezwa Maliki alitekwa akiwa dukani kwake saa 3 usiku wa Februari 1, mwaka huu.
Mmoja wa askari mgambo wa kijiji hicho, Habibu Mohamed Salum alisema alikuwepo wakati wa tukio hilo na yeye na wenzake walifukuzia gari la watekaji bila mafanikio.
“Siku hiyo nilikuja hapa dukani, nikakuta gari kama Toyota Land Cruiser yenye mkonga nyeusi na ina mstari mweupe. Kulikuwa na watu kama wanne wanazungumza na Maliki, mimi sikutilia shaka, sikujua wanaongea nini.
“Ghafla wakati naongea na wenzangu, ikaja taarifa kuwa ile gari iliyoondoka imeondoka na Maliki, ni kama vile walimsukumia kwenye gari,” alisema.
Alisema walishauriana na wenzake na kuamua kuifuatilia gari ile iliyokuwa ikielekea barabara kuu ya Lindi -Mtwara.
“Tukaifukuzia ile gari tukaikuta maeneo ya Mtundani tukaisoma namba, tuliendelea kuifuatilia kama inaelekea Mkuranga Polisi tutoe taarifa.
“Lakini ile gari ikaelekea Dar es Salaam, ikatuacha nasi tukaifuatilia hadi kijiji cha Mwanambaya, tuliifuatilia kwa umakini maana hatukujua ni watu wa aina gani,” alisema.
Alisema ilipofika Kisemvule waliona mtu akishuka kwenye gari hilo, hivyo wakaipita na kuwa mbele yao.
“Baadaye tukaamua tusubiri itupite hadi Vikindu, kuna kituo cha Polisi tuone kama wataingia pale, lakini hawakuingia,” alieleza.
Alisema walipofika kituo cha ukaguzi cha Mwandege, pikipiki yao ikapata pancha tairi la mbele.
“Tukamkuta askari kwenye kibanda, tukamwambia tunafukuzia gari tuna wasiwasi nalo limemchukua ndugu yetu. Askari akatuuliza mnaifahamu namba, tukasema ndio na tukamtajia.
“Lakini akatujibu kejeli, alisema ninyi sio mgambo, askari ni sisi tunaolipwa mshahara, tunabeba bunduki, ninyi ni vijana wakakamavu,” alisema.
Kwa upande wake, mke wa Maliki, Zainab Shabani alisema alisikia sauti ya mumewe kwa mara ya mwisho Februari mosi alipompigia simu.
“Naona wale watekaji walimpa nafasi ya mwisho kutoa taarifa, maana alipiga simu na nilipopokea akasema nenda kachukue hela na simu dukani, wakati huo mimi nilishachukua. Nilipotaka kuuliza alipo, simu ikakatika,” alisema.
Akisimulia tukio lilivyokuwa, Zainabu alisema ilikuwa saa 3 usiku, akiwa ndani anapika, alifika kijana na bodaboda na kumuuliza alipo mumewe.
“Ghafla akaja bodaboda wake akauliza kaka yupo huku? Nikamwambia yupo dukani, akasema kuna watu wamemchukua kwenye gari na hawajui kama ni polisi au majambazi. Nilipokwenda dukani nikakuta fedha na simu nikazichukua,” alisema.