Kitaifa

Mradi wa kurejesha takataka kunufaisha vijana 600 Tanzania

Mwanza. Zaidi ya vijana 600 nchini wanatarajia kunufaika kupitia kampeni ya elimu kwa umma ya kurejesha taka ngumu na za plastiki kuwa bidhaa kwa lengo la kuhifadhi na kulinda mazingira katika fukwe na ndani ya majini ya Maziwa Makuu ya Victoria, Nyasa na Tanganyika.

Kampeni hiyo itakayohusisha vijana kutoka fukwe 60 unalenga siyo tu kuhifadhi na kulinda mazingira na vyanzo vya maji, bali pia kutoa fursa za ajira kwa vijana kwa kujiongezea kipato kwa kugeuza taka kuwa bidhaa.

Akizungumza leo Ijumaa Machi 3, 2023 wakati wa kampeni ya kufanya usafi katika mwalo wa Mswahili jijini Mwanza, Mhadhiri Msaidizi wa Sayansi ya Akua na Teknolojia ya Uvuvi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bahati Mayoma amesema pamoja na kunufaisha vijana 600, kampeni hiyo pia itawafikia zaidi ya watu 100, 000.

“Watu 6, 000 watafikiwa moja kwa moja kupitia kampeni ya elimu kwa umma mwaloni wakati wengine zaidi 100, 000 watafikiwa kupitia vyombo vya habari,” amesema Mayoma

Kampeni hiyo inayoratibiwa na Shirikisho la Biashara za Rejereja na Bidhaa za Plastiki Nchini kwa kushirikiana na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Utunzaji Rasilimali za Uvuvi (EMEDO), Shirika la Arena na Taasisi ya Utafiti (NORCE) kutoka Norway ifanyika katika fukwe 30 za Ziwa Victoria, fukwe 15 Ziwa Nyasa na zingine 15 za Ziwa tanganyika.

Amewaomba Watanzania kila mmoja katika eneo na nafasi yake kutunza mazingira kwa kuacha kutupa hovyo takataka, hasa ndani ya maji kunusuru viumbe hai vya majini.

“Hadi kufikia mwaka 2022, wastani wa tani milioni 8 hadi 11 za taka za plastic zilibainika kuingia kwenye vyanzo vya maji duniani; taka hizi hutapakaa katika fukwe, ndani ya maji na sakafu ya Bahari, Maziwa na Mito. Hali hii ikiachwa iendelee kuna hatari ya takataka kuwa nyingi zaidi ya viumbe hai majini,” amesema Mayoma.

saku Kumanya, mmoja wa wavuvi katika Mwalo wa Mswahili aliyeshiriki kampeni ya usafi mwaloni hapo amepongeza kampeni hiyo akiwaomba wadau wote wa mazingira kuunganisha nguvu kulinda na kuhifadhi vyanzo na mazingira ndani na nje ya maji ya mito, maziwa na bahari.

“Elimu hii ya uhifadhi wa mazingira kwenye fukwe na ndani ya maji ifikie makundi yote ya kijamii kuanzia wavuvi, wachuuzi, wakulima na wafanyabiashara ambao shughuli zao zinagusa vyanzo vya maji,” amesema Kumanya

Mchuuzi wa dagaa mwalo wa Mswahili, Felista Jackson ameziomba halmashauri za jiji la Mwanza na manispaa ya Ilemela kutoa mikopo kuwezesha makundi ya vijana wanaofanya usafi katika maeneo ya mialo kupata mitaji ya kurejesha taka ngumu na za plastiki kuwa bidhaa.

Kampeni hiyo ambayo imezinduliwa jijini Mwanza Machi Mosi, 2023 inatarajiwa kuendelea hadi Septemba, mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi