Connect with us

Kitaifa

Mtuhumiwa mauaji ya mke amtumia sms mama mkwe

Moshi. Ni matukio nadra kutokea katika jamii, baada ya mtuhumiwa anayesakwa kwa udi na uvumba na polisi kwa tuhuma za mauaji ya mkewe, kumwandikia mama mkwe ujumbe mfupi (SMS), kuelezea ushiriki wake katika tukio hilo.

Mtuhumiwa anadaiwa kutuma ujumbe huo wakati polisi wakiwa tayari wamechukua sampuli kwa ajili ya kupima vinasaba (DNA) ili kuthibitisha kama mwili uliokutwa umeteketea kwa moto Februari 19, 2023 ni wa Josephine Mngara (27).

Mwili wa mwanamke huyo ulikutwa umeteketea kwa moto kwenye nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika (pagale) ambapo kulikutwa pia michirizi ya damu kutoka kwenye nyumba ya mkazi wa eneo hilo.

Katika ujumbe huo aliomtumia mama mzazi wa marehemu, Theodora Msuya, mtuhumiwa anadaiwa kusema roho inamuuma kwa tukio lililofanyika. Mwanamume huyo ambaye jina limehifadhiwa ndiye alikuwa akiishi na marehemu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Msuya alisema katika sms aliyotumiwa, mtuhumiwa alielezea nini kilitokea siku hiyo na kwamba alimkuta mwanamume mwingine na mkewe na ukatokea ugomvi na ametaja jina la mtu anayedai ndiye muuaji.

SMS hiyo iliyohaririwa inasomeka “Mama samahani si kosa langu, nilimkuta (anamtaja) na mke wangu kwangu, nikavunja mlango tukaanza kupigana. Mimi nikashika panga na yeye akachukua mpini wa jembe.

“Akawa anarusha nikakwepa ndo akampiga mke wangu mpaka chini. Akanipa nauli akaniambia sepa niachie mimi… Muulize (anamtaja), mama mimi sijui roho yangu inauma sana mchana mwema.”

Mama wa binti huyo, alidai kama waliotenda tukio hilo wamejitokeza na kuomba radhi, wanaliomba Jeshi la Polisi kuwapa mabaki ya mwili wa mtoto wao kwenda kuzika kwa kuwa ni muda wameweka msiba nyumbani bila kujua mwafaka. “Mpaka sasa hatujapewa mwafaka na Jeshi la Polisi juu ya kuzika na nini kinachoendelea, tumeweka msiba hapa nyumbani tuna zaidi ya wiki sasa, watu wamekaa hapa wameacha shughuli zao na familia zao wako hapa nyumbani.

“Hapa nilipo nimechoka jamani, tunaomba tupewe hayo mabaki ya mwili wa mwanangu tukazike maana kwa kweli nimechoka,” alisema mama huyo.

Inadaiwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori alieleza kuwa, baada ya polisi kuchunguza walikuta michirizi ya damu kutoka nyumba jirani kuelekea eneo ambalo mwili ulikutwa.

Alisema mabaki ya mwili huo, ikiwemo mifupa na sehemu nyingine za mwili huo vimehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC kwa ajili ya taratibu nyingine za kiuchunguzi.

Februari 23, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Simon Maigwa alisema tayari Jeshi la Polisi limechukua sampuli ya vinasaba (DNA) kwa ajili ya kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kujiridhisha kama ni mwili wa mwanamke huyo.

“Tumepeleka DNA kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili tuthibitishe ule mwili ni huo au ni mwingine, hivyo tumechukua vitu muhimu kwa mama mzazi wa huyu binti ili kujiridhisha na tukio hilo,” alisema Kamanda Maigwa.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi