Connect with us

Kitaifa

Rais Samia atoa onyo la mwisho kwa mawaziri

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa onyo la mwisho kwa wateule wake wasioelewana kwenye utekelezaji wa majukumu yao akisema ameachana na mtindo wa kuwapangua badala yake atawaengua.

“Sipendi sana, nataka niwaambie, hii itakuwa mara ya mwisho kutumia sababu hii kupangua wizara, likijitokeza tena maana yake hamwezani na hamuwezi kufanya kazi, wote wawili mtakwenda. Kama ni katibu mkuu na naibu wake mtakwenda wote au waziri na naibu wake mtakwenda wote.”

Hiyo ni kauli ya Rais Samia aliyoitoa jana Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma mara baada ya kuwaapisha watendaji mbalimbali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na watendaji taasisi aliowateua juzi.

Onyo hilo la Rais Samia limekuja siku chache, baada ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kusisitiza ushirikiano kati ya mawaziri, manaibu na makatibu wakuu katika wizara zao akieleza bado kuna changamoto.

“Ushirikiano baina ya watendaji bado tunaona changamoto katika wizara mbalimbali. Tumezungumza mara kadhaa na Rais Samia ameshalieleza, hii mivutano kati ya waziri, naibu waziri au waziri katibu mkuu haina tija, mkae kama timu kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania kwa sekta mnazoziongoza,” alisema Dk Mpango mara baada ya uapisho wa mawaziri wawili, Mohamed Mchengerwa (Maliasili na Utalii) na Balozi Pindi Chana (Utamaduni, Sanaa na Michezo).

Onyo la watendaji hao wakuu wa nchi limewaibua wasomi na wachambuzi wakisema kuna haja ya kuangalia mipaka ya majukumu ya viongozi ili kuepusha migongano hiyo ya mara kwa mara na ofisi ya Rais inapaswa kuwasaidia kwa hilo.

Jana, katika hotuba yake ambayo haikuzidi dakika 15 mbele ya viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Rais Samia alisema kutoelewana huko kunafikia hatua anaona kuna hatari ya kazi kutofanyika kwa ufanisi.

“Jambo hili silipendi kwa sababu nitakuwa kama nawadekeza vile, maana yake mnagombana huko ili nipangue, nimweke huyu, nimtoe hapa… silipendi. Nataka nikiwapanga mfanye kazi. Sio sababu ya kugombana lakini Arusha tarehe 2 na 3 tutaelezana,” alisema Rais Samia.

Katika uteuzi huo uliotangazwa juzi, Rais Samia alimpandisha Abdallah Ulega kutoka naibu waziri wa mifugo kuwa Waziri kamili wa wizara hiyo, akichukua nafasi ya Mashimba Ndaki ambaye uteuzi wake ulitenguliwa, huku akiwahamisha baadhi ya manaibu mawaziri na makatibu wakuu katika wizara mbalimbali.

Jana Rais Samia alimtaka Ulega kuhakikisha ugomvi wao ukamalizwe kwa kufanya kazi akisema anataka kuona wizara ya mifugo na uvuvi ikinyanyuka.

“Nakuamini na nadhani utaweza, kama wakati ule ulikuwa hufanyi kwa sababu ulikuwa chini ya mtu, sasa utaonekana unafanya kwa sababu hauko chini ya mtu au na wewe utakuwa kama wale. Safari bado ni ndefu tuna miaka miwili mbele yetu, nikuombe sana ukafanye kazi,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo, Rais Samia alisema alidhani jeshi lililokuwapo (baraza la mawaziri) angekwenda nalo hadi mwisho wa muhula wake, lakini katika safari ajali hutokea. Alisema mabadiliko hayo ni ya kawaida katika kuimarisha utendaji ndani ya Serikali.

Rais Samia alisema ndiyo maana mabadiliko makubwa yamefanyika katika ngazi ya makatibu wakuu lengo ni kuweka nguvu moja kwenda na kasi inayohitajika.

“Tumejitahidi kunyofoa katika maeneo mliyopo kujaza nafasi hizo tukijua kuwa kila mtu anaelewa eneo alilopo.

“Tumeamua kuwavuta watu walio nje ya Serikali kwa kudhani kuwa watakuja na mawazo mapya kwa kuona ndani ya Serikali nini kinafanyika, wakichanganya na wao mambo yatakwenda vizuri.

“Tutaendelea kunyofoa huko na kuleta ndani ili watusaidie Serikalini kwa sababu wakikaa nje kazi ni kulaumu tu, hajui ugumu uliomo ndani ya Serikali, wakiingia tutafanya nao watupe uzoefu wao waone yaliyopo serikalini kwa pamoja twende,” alisema.

Uwekezaji

Kuhusu uwekezaji kutokuwa na waziri, Rais Samia alisema amemua kumtanguliza katibu mkuu ili kuweka mambo sawa ikiwemo kupanga yanayotakiwa kupangwa huku akieleza kuwa anataka maeneo matatu muhimu yarudi chini ya Ofisi ya Rais na baadaye michakato na sheria vikikamilika itakuwa wizara kamili.

“Kwa sasa tunamleta msajili wa hazina, tume ya mipango na uwekezaji zinakuja chini ya Rais, tutakuwa na waziri wake na naibu waziri wake tukimaliza mchakato wa sheria itakuwa wizara kamili kwa sasa tumetanguliza katibu mkuu atusaidie kupanga, tunafanyaje wanakaaje, mambo ya uchumi…mkubwa na mdogo tunafanyaje atusaidie kupanga,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia alimteua na kumthibitisha Yahya Samamba kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, baada ya waliopaswa kumuidhinisha kushindwa.

Alitangaza kumteua, akitangulia kumuita Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko na kujibiwa kwamba hayupo, ndipo alipozungumzia suala hilo la kusuasua kumuidhinisha na kuhitimisha k mchakato wa kumuidhinisha.

Awali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema watumishi walioapa wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu.

“Kuwapo kwao hapa tunaamini wanakuja kuimarisha utendaji ndani ya Serikali, spika ameeleza mengi na mimi kwa niaba ya watendaji wote tukuhakikishie kuwa tutawajibika kikamilifu kutekeleza maelekezo yako,” alisema Majaliwa.

Kwa upande wake, Dk Tulia aliwataka viongozi wapya walioapishwa kutunza siri huku akieleza kuwa hatarajii kuona watakapomaliza dhamana waliyopewa wanaanza kuzitoa kwa sababu kiapo hakijasema kinaishi lini.

“Siri ambazo utazijua kipindi ambacho umeaminiwa katika uongozi unatarajia uendelee kuzitunza hata ile koma ambayo mheshimiwa Rais alisema ameiweka itakapokupitia zile siri unapaswa kuendelea kuzitunza,” alisema Dk Tulia.

Wajue mipaka yao

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk George Kahangwa alisema,” kauli ya Rais inaweza kuwa onyo la mwisho lakini tutarajia wanadamu bado wanaweza kuwa na udhaifu na tutarajie atasimamia maneno yake kwani ameyasema hadharani.

“Ofisi yake inapaswa kuyafanyia kazi kwa kuwajuza majukumu yao kama kazi ya waziri ijulikane wazi, kazi ya naibu waziri, kazi za katibu mkuu, kazi za naibu katibu wakuu na kazi za wakurugenzi, kila mmoja ajue lake na hili litasaidia lasivyo yataendelea kujitokeza,” alisema mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)

Dk Kahangwa aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma UDSM (Udasa) alisema, “kwangu ni jambo la kusikitisha kwamba watu wanaoaminiwa katika nafasi kubwa wanashindwa kuelewana.” Alisema kutofautiana kimawazo ni jambo la kawaida kwa binadamu, “lakini kutofautiana hadi mnakwamisha shughuli kuendelea ni hatari,” alisema.

Alisema ukiondoa kutofautiana na migogoro, unaweza kuharibu mambo, bora iwe migogoro chanya ama kutokuelewa na kama waziri, naibu waziri na katibu mkuu wanashindwa kuelewana huenda si nafasi zao, bali kuna shinda kwenye majukumu.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Aviti Mushi alisema Rais Samia amechelewa kutoa onyo hilo, akisema hali ilivyo kuna baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu hawajui majukumu yao na ndiyo maana wanajikuta wanaingilia katika utendaji kazi wao.

“(Rais) alitakiwa kuliona hili mapema tu, kazi katibu mkuu na mawaziri zinajulikana, lakini imekuwa tofauti kwa watendaji hawa. Rais alitakiwa kuwaondoa maana watu wapo wengi tu wanaoweza kazi hizi.

“Lakini inapaswa watu hawa kujengewa uwezo wa namna ya kutekeleza majukumu yao, ili kuondokana na hali hii. Kwa sababu kuna wengine wanakuwa wageni, sasa ukichanganya na hofu inakuwa tatizo,” alisema Dk Mushi.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi