Makala
Sh2 milioni zilivyomvusha Lema mpakani
Katika simulizi ya kukimbia nchini baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, tuliona Mbunge wa zamani wa Arusha Godbless Lema, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na aliyekuwa Meya wa Ubungo, Jacob Boniface walivyokamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha wananchi wafanye vurugu, kuharibu mali na kudhuru viongozi, leo tunaendelea kuangazia hatima ya viongozi hao.
Lema anasema wakiwa kituo kipya cha polisi Oystebay, kuna eneo walisimamishwa kwa muda mrefu wakiangaliana na watuhumiwa wengine wa makosa mbalimbali waliokamatwa kwa nyakati tofauti.
Anasema mmoja wa askari aliwaambia sababu za wao kusimamishwa ni watuhumiwa hao kukaririshwa sura zao, ili wapate urahisi wa kutoa ushahidi mahakamani kwamba walishirikiana na viongozi wa Chadema.
“Askari huyo alitudokeza kwamba tumepangiwa tumepewa kesi mbaya na hatuwezi kutoka jela hadi mwaka 2024 au 2025. Niliingia katika moja ya chumba ya ofisa, nikamuuliza kwa nini tumesimamisha muda mrefu halafu tumeangaliwa kwa muda mrefu?
“Nikajibiwa kwamba wale si watu wenu hamuwajui?
Lema anasema baada ya hapo Wambura (Camillius- Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini sasa), aliwaambia kila mtu ajidhamini mwenyewe kwa kuandika maelezo.
Lema anasema alifuatwa na askari mmoja na kuelezwa sababu za wao kutakiwa kujidhamini ili iwe rahisi kuripoti kila siku kituoni hapo.
Hata hivyo, anasema alimfuata msaidizi wa Wambura kumweleza anataka atafute mtu wa kumdhamini kwa sababu anaishi Arusha, hivyo asingeweza kila siku kuwa Dar es Salaam.
Anasema polisi walilegeza masharti kwa kuwaambia wanaweza wasiende kuripoti polisi kwa siku mbili, hivyo aliitumia nafasi hiyo kuanza safari hadi Arusha. Lakini kabla ya kuondoka aliwekewa mtu wa kumfuatilia kila hatua anayoipiga.
“Kila nilipokwenda anilifuata iwe Posta au Mbezi, nikwambai aache kunifuatilia, akaniambia hana nia mbaya bali ni maelekezo ya viongozi wake wa juu,” anasema. Kabla hajaenda Arusha, Neema (mkewe) alimpigia simu na kumueleza ana wasiwasi kwa kuwa nyumbani kwao polisi wanakwenda mara kwa mara.
“Nikiwa uwanja wa ndege, nikwambia nakuja Arusha, ila asimwambie mtu yeyote, nilipofika KIA (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro), Neema akiwa njiani na mtoto wao kwenda kumpokea alimuambia kuna gari linawafuatilia,” anasema Lema.
Anasema Neema alimweleza kadiri anavyojaribu kuipa nafasi ya kuipisha gari iliyokuwa inawafuatilia haitaki kupita. Lema alimwambia Neema waingie katika kituo cha mafuta cha karibu kisha wakae karibu na usawa wa kamera.
Lema anasema Neema alifuata maelekezo hayo, huku yeye akichukua teksi hadi katika eneo hilo na kuungana nao kwa ajili ya kuelekea Arusha. Wakati wanakwenda Arusha mwanaye aliona tena gari hiyo ikiwafuatilia kwa karibu, ikamlazimu kuongeza mwendo.
“Nikwambia Neema wakiendelea hivi hawa wanaotufuatilia nitakwenda kuingiza gari kituo kikuu cha polisi Arusha kama wana nia mbaya basi waitekeleza hapo,” anasema na kuongeza wakati wanakaribia Mjini aliingia barabara ya Njiro (nyumbani kwake) na gari iliyowafuatilia ilipitiliza.
“Wakati naingia nyumbani gari la polisi tukasikia imeegeshwa nje ya nyumba ilinipa wasiwasi sana, baadaye nilipata mawasiliano muhimu kutoka kwa watu waandamizi, ningewapuuza ningekuwa mpumbavu… kupita maelezo,” anasimulia.
Lema anasema katika mawasiliano hayo watu hao walimpa tahadhari ya kwamba kama anaweza kuondoka Tanzania kwa muda afanye hivyo haraka, hata hivyo aliwaambia ana mahali pa kujificha maeneo ya Rombo na Marangu mkoani Kilimanjaro.
“Walinisisitizia niondoke, baadaye nikapigiwa simu na mtu mwingine akaniuliza nina namna ya kuondoka Tanzania kwa muda, nikamwambia naweza, basi akanitaka niondoke haraka, nilipanga niondoke mwenyewe niende Dubai au Cyprus niache familia.
“Baadaye nikajiridhisha kwamba nikiondoka mwenyewe, mke na watoto watapata shida, kuna wakati nikiwa jela, Neema aliteswa sana hadi kupewa kesi ya wizi wa gari. Nikamwambia Neema tunaondoka akaniuliza tunaelekea wapi nikamwambia Cyprus,”anasema.
Lema anasema Neema alihoji kwa nini wanakwenda Cyprus, akamjibu kwa mazingira yaliyopo hana muda wa kutafuta visa, lakini kwa Taifa hilo hakuna changamoto kubwa za kutakiwa hivyo vitu cha msingi watoke nje ya Afrika.
Mwanasiasa huyo anasema Neema alimshauri kwa nini wasiende nchi za Afrika Mashariki, akamjibu wakienda huko watamalizwa.
“Tukiwa katika majadiliano, tulifanya hesabu pia ya kwenda Singapore ikaonekana ni gharama kubwa, mwishowe nikamwambia Neema wao watakwenda kwanza Kenya.
Simu kwa Wajackoyah.
Lema anasema alimpigia simu rafiki yake, George Wajackoyah aliyewania urais katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana kuwa maisha yake yapo hatarini kwa kuwa anawindwa, hivyo inamlazimu kuondoka Tanzania.
“Nikamwambia nimeshatafuta nyumba, nikamuomba sana aje kuichukua familia yangu, alikubali na kuja kwa haraka hadi Namanga (mpaka wa Tanzania na Kenya). Pia niliandaa mazingira na marafiki zangu waliokuwa wakifanya kazi Serikali ya Kenya, ili wawe salama zaidi” anasema.
Lema anasema ilikuwa hali ngumu na hataisahau katika maisha yake kufunga nyumba na kukimbia nchini na wakati huo wote wa kuratibu mchakato huo hakuwaaga wazazi wake wala ndugu zake wa karibu kutokana na hofu iliyotanda.
Kwa mujibu wa Lema, siku ya safari Neema alitangulia na watoto hadi Namanga na mpango uliokuwapo yeye kupitia njia nyingine ikiwemo ya Rombo au Sanya kwenda katika nchi hiyo jirani.
Anasema alitaka familia itangulie ili aweke mambo sawa ikiwemo hati za nyumba, magari, mashamba na kufunga baadhi ya shughuli zake.
“Tulikubaliana na Neema kuwa nitapitia Sanya (Hai) au Rombo kisha tutaonana Kenya, Neema alipofika mpakani maofisa wa Uhamiaji walikataa kuweka muhuri katika hati zao za kusafiria. Wakati huo mimi nilikuwa mbali na eneo hilo na nilikaa ndani ya gari ndogo.
“Walimuuliza Neema wewe ni mama Lema?akajibu ndio, unakwenda wapi, akawajibu nakwenda kuwatafutia shule watoto maana za Tanzania changamoto na kutokana sera mpya walimu wanahama, walikaa karibu saa tano wakihojiwa,” anasema.
Baadaye maofisa wa Uhamiaji walimuuliza Lema yuko akawaambia yupo Jijini Arusha, wakamwambia hapa mbona anaonekana katika gari ndogo aina ya Toyota Carina, aennde ukamuite. Anasema Neema alimpigia simu na kumtaarifu kwamba anahitajika na maofisa wa Uhamiaji.
Kwa mujibu wa Lema, pembeni mwa gari alilopanda kulikuwa na gari jingine lililoegeshwa likipiga muziki mkubwa, lakini waliokuwa ndani hawashuki badala wanakunywa pombe. Hata hivyo, Lema alibaini gari lile lilikuwa likimfuatilia toka akiwa Arusha kwenda Namanga.
“Nikaonana na maofisa wa Uhamiaji wakaniuliza hii ni familia yangu, nikawaambia haya maswali yameanza lini? Kwani Kenya imekuwa Marekani, lazima kuwepo na maswali mengi?
“Wakaniambia nisubiri maelekezo kutoka kwa kamishna wa Uhamiaji, muda mfupi baadaye simu ikapigwa kwamba kama ni mke na watoto waruhusiwe, wakati huo Wajackoyah alishafika upande wa pili,” anasimulia.
Lema anasema kutokana mazingira kuwa magumu Namanga, alishauriwa na Neema arudi Arusha ili akapitia Longido, lakini alimjibu mkewe haiwezi kufanya hivyo kwa sababu atakamatwa haraka.
“Nikaamua kushika fedha mkononi kama Sh 2milioni na kuanza kutafuta eneo la kubadilisha, nikawauliza Uhamiaji wapi kuna viwango vizuri, wakaniambia niingie ndani kisha nivuke lango karibu na eneo la Kenya.
“Nikasema hapa ndipo wamenipa njia ya kutoka nikavuka lango, nikabadilisha fedha kidogo, nikachukua bodaboda, nikawaona Wajackoyah na Neema wakinisubiria kwa mbele baada ya kukamilisha taratibu za uhamiaji,” anasema Lema.
Anasema baada ya kuvuka simu zikaanza kupigwa kwa mtandao, ikiwa ni kupita kilomita 10 kutoka mpakani ambapo walikutana na lango la kwanza na walisimamishwa na polisi wa Kenya lakini hawakuulizwa hati za kusafiria.
Wakiwa wanaendelea na safari mbele tena walikuta daladala ya abiria imesimamishwa mfano wa kuziba barabara huku pembeni kukiwa na gari la polisi wa kikosi maalumu cha Kenya. Lema anasema polisi walisikika wakisema wamepata taarifa za watu wanataka kuipindua Serikali ya John Magufuli (hayati).
“Walinikamata na kunipeleka katika kituo cha polisi cha Kajiado, tukiwa hapo mawasiliano yalikuwa hayaishi kati Tanzania na Kenya, yakihusu namna gani tunaweza kurudishwa Tanzania.Baadaye Neema na watoto wakaambiwa wakae nje.