Kitaifa
Lema: Asimulia alivyopanga mkakati kutoroka
Dar es Salaam. Wakati maandalizi ya kumpokea mbunge wa zamani wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema anayetarajia kuwasili nchini Machi 1 mwaka huu, akitokea nchini Canada alikokimbilia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, mwanasiasa huyo ameeleza Canada haikuwa miongoni mwa nchi alizotaka kwenda.
Mwanasiasa huyo aliondoka nchini Novemba 18, 2020 kwa kile alichodai ni kunusuru maisha yake na familia yake dhidi ya baadhi ya watu aliodai walikuwa na malengo ya kumuangamiza.
Katika simulizi ya mkasa uliomtokea, mwanasiasa huyu anasema nchi zilizokuwa akilini mwake ni Singapore, Cyprus na jiji la Dubai lakini baada ya kufanya tathmini ya gharama za kuishi ambazo hakuwa tayari kuzitaja alishindwa kwenda huko.
Lema anasema safari ya Canada ilianzia nchini Kenya baada ya hali kuwa tete akiwa jijini Nairobi alikokaa kwa wiki tatu, hivyo alilazimika kuondoka kuepusha misuguano kati ya Tanzania na Kenya iliyoanza kujitokeza.
Anasema mke wake, Neema alihoji kwa nini anataka kwenda Cyprus?, akamjibu kwa mazingira yaliyopo hana muda wa kutafuta visa na kwa kuwa Taifa hilo halina vikwazo vingi kwa wageni. “Neema alinishauri twende katika nchi mojawapo za Afrika Mashariki, nikamjibu tukienda huko tutamalizwa kirahisi, tulifanya majadiliano ya kina ikiwemo mahesabu ya kwenda na kuishi, kwenda Singapore ikaonekana ni gharama kubwa,” anasema Lema katika mahojiano na gazeti hili.
Misukosuko ilivyoanza
Lema ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, anasema dalili za kuwa katika maisha ya hatari zilianza kuonekana mapema baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni kumkamata yeye, Boniface Jacob (meya wa zamani wa Ubungo) na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema, anasema walikuwa katika maandalizi ya maandamano ya amani ya kupinga mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Anasema vikao hivyo vilikuwa vikifanyika kwa nyakati tofauti nyumbani kwa Mbowe.
Novemba 2, mwaka 2020, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alitangaza jeshi hilo kuwashikilia viongozi hao, kwa madai ya kuwashawishi vijana kuandamana.
Kwa mujibu wa Mambosasa, usiku wa kuamkia Novemba 2, mwaka 2020 polisi walifanya msako kuwakamata viongozi hao wanaodaiwa kuwashawishi vijana kushiriki maandamano, kuharibu mali kama kuchoma magari, kuchoma visima vya mafuta, kuchoma matairi hivyo kuvuruga amani na kuleta taharuki ili shughuli za wananchi zisimame.
Lema anasimulia kuwa baada ya kumaliza kikao nyumbani kwa Mbowe, maeneo ya Mbezi, walichukua gari dogo iliyokuwa ikiendeshwa na Jacob kwa ajili ya kwenda katika moja ya hoteli aliyoifikia ili kuhama kutokana na taarifa za kuwindwa.
“Tukiwa katika barabara ya chini maeneo ya Mbezi Kilongawima, karibu kabisa na lango na nyumba ya Mkuu wa Majeshi (CDF) mstaafu Davis Mwamunyange tulizingirwa na askari wenye silaha nzito (kikosi maalumu) waliovalia kiraia. “Majira ya saa moja usiku tukiwa na Mbowe tulikamatwa kikatili sana…sitosahau, tulipelekwa moja kwa moja hadi Oysterbay kituo cha zamani eneo la gereji na kuwekwa hapo, huku polisi wakisubiri maelekezo kutoka juu,” anasema Lema.
Lema anasimulia kuwa wakiwa Oystebay polisi waliamriwa kutoa simu zao na kuondoa password ‘nywila’, lakini yeye Lema aligoma. Anasema aliwaambia polisi atatoa nywila za simu yake endapo ataingizwa kituoni ili kuweka kumbukumbu sawa.
Anaeleza baada ya kukataa polisi waliamua kumfunga pingu mikono ikiwa imezungushwa nyuma ya mgongo na kumtenganisha gari na kuamuru kumpeleka moja kwa moja Kibaha mkoani Pwani, kwa maelezo ya kwamba wanakwenda kumalizana naye na kumtaka asali sala yake ya mwisho. “Tulifika hadi Kibaha Mjini gari likaegeshwa pembeni katika pori, wakawa wanasubiri maelekezo, walikuwa askari zaidi ya watano hivi katika ile gari wakiwa na bunduki. Niliwekwa katikati nikiwa na pingu kushoto na kulia kuna askari. “Baada ya muda nikasikia ‘code’ mpango umebadilika, nakumbuka sana hilo neno, wakasema tunakwenda safari nyingine, nikapelekwa tena hadi Mlandizi kituo cha polisi. Nilipofika OCD (mkuu wa kituo) alikataa, akiwaambia askari wenzake hachukui mtu kwa sababu wanampelekea watu… halafu wanamuachia kesi,” anasema. Hata hivyo, Lema anasema OCD huyo aliwaambia askari wenzake, yupo tayari kupokea watu endapo atapewa maelekezo na viongozi wake wa juu akiwamo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani.
Anasema kulikuwa na mabishano makubwa na mwisho wa siku OCD alimpigia simu RPC, kisha kwa Mambosasa, baadaye alikuja katika gari na kufungua mlango na kubaini kumbe alikuwa Lema.
OCD- kumbe mheshimiwa Lema, salama?
Lema –nikamjibu salama afande
OCD- wamekuumiza au kukugusa popote?
Lema -Hapana afande
OCD- una uhakika?
Lema- Ndiyo afande hawajanigusa wala kuniumiza.
Anasema baada ya mazungumzo ya muda mfupi na OCD, alishushwa katika gari na kuingizwa kituo cha polisi na katika upekuzi polisi walifanikiwa kuchukua simu yake janja huku simu yake ndogo ‘kitochi’ akiificha chini ya kiatu.
Lema anasema akiwa kituoni alimpigia mkewe (Neema) simu kwa siri akimtaarifu kwamba yupo kituo cha polisi cha Mlandizi, yupo pekee bila Mbowe wala Jacob. Alimtaka Neema kusambaza taarifa hiyo ingawa Neema alimuarifu kuwa Kamanda Mambosasa alitangaza kukamatwa kwao.
Lema anasema hali hiyo ilimpa faraja na amani katika moyo wake, kwa sababu watakuwa salama zaidi tofauti na awali. “Naweza kusema mkutano wa Mambosasa ndiyo uliokoa maisha yetu, kwa hali iliyokuwa kulikuwa na dalili za sisi kupotezwa…Nikiwa kituoni hapa, alikuja Naibu Mkuu wa upelelezi wa makosa ya Kanda Maalumu Dar es Salaam kunihoji. “Katika karatasi ya mahojiano iliandikwa tunashtakiwa kwa makosa makubwa ya uhaini, nilikataa kuhojiwa nikawaambia bila mwanasheria wangu siwezi kuhojiwa. Niliwaambia kwa makosa haya sitoandika chochote,”anasema.
Hata hivyo, Lema anasema ofisa huyo wa polisi alimbembeleza aandike maelezo yake yote ili kesi hiyo akaipiganie mahakamani. Lema anasema aliendelea na msimamo wake huo akiwaambia yupo tayari kwa lolote lakini sio kuandika maelezo bila mwanasheria wake.
Anaeleza baada ya muda maofisa hao walitoka kwa majadiliano, kisha kurudi tena ndani ya chumba alikohifadhiwa na kumweleza kwamba endapo hatoandika maelezo ataendelea kukaa rumande na hakuna atakayejua alipo.
“Waliniomba namba ya mwanasheria wangu (John Mallya), niliwapa na kunieleza wanakwenda kushauriana na viongozi wa juu ili kujua cha kufanya. Kesho yake walikuja kunichukua na kunihamishia Oysterbay kituo cha zamani, tena chini ya mti baada ya kukaa Mlandizi kwa siku mbili.
“Baada ya muda mfupi gari mbili zilikuja kwa nyakati tofauti ndipo nilipomuona Mwenyekiti (Mbowe) na Jacob. Tulishushwa wote na kupelekwa katika kituo kipya cha polisi cha Oystebay na kila mtu alipelekwa katika chumba chake ili kutoa maelezo,” anasema.
Kwa mujibu wa Lema, wakiwa kituoni hapo kuna eneo walisimamishwa kwa muda mrefu wakiangaliana na watuhumiwa wengine wa makosa mbalimbali waliokamatwa kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo, Lema anasema mmoja wa askari aliwaambia sababu za wao kusimamishwa ni watuhumiwa hao kukaririshwa sura zao, ili kupata urahisi wa kutoa ushahidi mahakamani kwamba walishirikiana na viongozi wa Chadema.
“Askari huyo alitudokeza kwamba tumepewa kesi mbaya na hatuwezi kutoka jela hadi mwaka 2024 au 2025. Niliingia katika moja ya chumba cha ofisa , nikamuuliza kwa nini tumesimamishwa na kuangaliwa kwa muda mrefu?
“Nikajibiwa kwamba wale si watu wenu hamuwajui? Nikathibitisha maneno niliyoambiwa na mmoja wa askari.