Connect with us

Kitaifa

Hatima mgogoro KKKT Machi mosi

Mtwara. Hatima ya mgogoro wa Kanisa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki uliodumu kwa zaidi ya miaka sita, huenda ukafikia mwisho Machi 1 mwaka huu baada ya Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo kwenda kuwasikiliza.

Askofu Shoo anakwenda katika dayosisi hiyo kwa ziara ya siku tatu kuanzia Februari 27 mwaka huu pamoja na mambo mengine, atashiriki mkutano ulioitishwa baina ya dayosisi hiyo na wachungaji wote utakaofanyika Machi 1.

Mkuu huyo wa kanisa, anafanya ziara hiyo ikiwa umepita takribani mwezi mmoja tangu wachungaji wa sharika 33 kutoa tamko la kumtaka Askofu Lucas Judah wa dayosisi hiyo na watendaji wake kutokanyaga katika sharika wanazoziongoza.

Wachungaji hao walitangaza uamuzi huo kwa pamoja Januari 15 mwaka huu, kuwa wanarudi katika utawala wa majimbo hadi mgogoro huo ulioibuka mwaka 2016 utakapotatuliwa na Askofu Shoo.

Tamko hilo lilisomwa na Mkuu wa Jimbo la Lindi, Mchungaji Wayzime Simwinga katika Kanisa la KKKT Mtwara akiwa amezungukwa na wenzake huku waumini waliohudhuria ibada iliyoongozwa na Mchungaji Daudi Nalima wakisikiliza.

Simwinga alisema wanapinga uendeshaji mbaya wa shughuli za dayosisi unaofanywa na Askofu Judah anayedaiwa kuhamisha kiti cha uaskofu kutoka kanisa kuu lililowekwa wakfu kwenda kanisa dogo la Magomeni, Mtwara mjini.

Kutokana na migogoro isiyoisha kwenye dayosisi hiyo, walimtaka Askofu Judah na wasaidizi wake wasifike kwenye sharika zote za Nanyamba, Ndanda, Liwale, Tandahimba, Masasi na Mtwara zilizoshiriki kutoa tamko hilo.

Ziara ya Askofu Shoo

Jana, gazeti hili lilipata taarifa ya uwepo wa ziara hiyo ya Askofu Shoo atakayeambatana na Katibu Mkuu wa KKKT, Robert Kitundu.

Mwananchi limefanikiwa kuona barua ya mwaliko kutoka kwa mmoja wa wachungaji wanaotakiwa kuhudhuria mkutano wa Machi 1, utakaofanyikia Ushirika wa Magomeni.

Mwaliko huo uliotumwa Februari 22 mwaka huu kwenda kwa wachungi wote wa Dayosisi ya Kusini Mashariki na Katibu Mkuu msaidizi wa Dayosisi hiyo, Mchungaji Erick Malindi, ukiwataka kuhudhuria mkutano huo pasina kukosa huku ajenda zikiwa hazijabainishwa.

Gazeti hili, lilifika jana ofisi kwa Mchungaji Malindi kujua undani wa ziara hiyo ya Askofu Shoo. Alisema: ”Ni kweli mkuu wa kanisa anakuja akiambatana na katibu wake ambapo itakuwa ni ziara ya kikazi Februari 27 ambapo ataondoka Machi Mosi atafanya vikao na viongozi mbalimbali wa kanisa ili kuweka sawa hali iliyopo.”

“Mimi ni msaidizi, kuna Kaimu katibu mkuu ambaye amesafiri pia hali ni shwari ugeni unakuja kuweka sawa hali ambayo mmeisikia nyie mimi siwezi kuizungumzia lakini ujio wake Serikali inatambua na tumeshatoa taarifa,” alisema

Aliongeza: “Sisi tulimuita kutokana na hali iliyokuwepo kwa hatua tuliyofika ilikuwa ni muhimu yeye afike kutatua mgogoro huo lililopo ndani ya kanisa ila kwa sasa Askofu Lucas Mbedule hayupo Mtwara yupo mkoani Njombe kwenye semina ya kikazi tangu Jumatano ya wiki hii. Aliondoka na atarejea wiki ijayo,” alisema Mchungaji Malindi

Kwa upande wake, Mkuu wa Jimbo la Lindi, Wayzime Simwinga alisema: “Tumepokea kwa furaha ujio wake, yeye ni baba anapokuta mtu na kaka wanagombana, anakuwa mtatuzi wa migogoro nyumbani akija baba tunaamini kupata suluhisho hata kama Dayosisi ina katiba yake lakini yeye ni baba tunaamini ujio wake ni chachu kwetu.”

Wakati Askofu Shoo akisubiriwa Dayosisi ya Kusini Mashariki, mmoja kati ya wachungaji waliotoa tamko la kumkataa Askofu wao, Francis Mandamo wa Mtwara Usharika wa Naliendele alisema ujio wa kiongozi wao unategemea kupeleka amani ambayo ilipotea katika kanisa hilo.

“Wachungaji wote tumeitwa katika kanisa la Magomeni Machi Mosi, yapo mambo mengi tunapaswa kuyafanya lakini kutokana na kukosekana kwa amani tumekuwa hatufanyi. Naamini kuwa kukutana na Baba Mkuu Askofu Shoo utakuwa na neema katika dayosisi yetu”alisema mchungaji Mandamo

Kwa upande wake, Eriud Mkondola, mmoja wa waumini wa kanisa hilo mkoani Mtwara alisema usharika wa Mtwara Mjini umekuwa ukimuomba Askofu Shoo kufika ili kumaliza mgogoro huo.

Migogoro KKKT

Mgogoro huo ni kama ule wa Dayosisi ya Konde uliodumu kwa miaka kadhaa na hatimaye kushuhudia Edward Mwaikali, aliyekuwa askofu wa dayosisi hiyo akiondolewa na nafasi yake akichaguliwa Mchungaji Geofrey Mwakihaba.

Askofu Mwaikali ambaye sasa ameanzisha Kanisa la Kilutheri la Afrika Mashariki (KKAM), aliondolewa na wajumbe wa mkutano mkuu wa Dayosisi hiyo uliofanyika Machi 22 mwaka jana na kuhudhuriwa na Askofu Shoo.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi