Kitaifa
Mapya mwanafunzi aliyedaiwa kufa kwa kipigo
Moshi. Tukio la kifo cha mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Bishop Alpha Memoria High School Moshi, Walter Swai linazidi kuchukua sura mpya, baada ya uchunguzi wa awali kubaini alikuwa na tatizo la mapafu.
Awali kulikuwa na taarifa na madai kutoka kwa ndugu wa mwanafunzi huyo kuwa kifo chake kilitokana na kuoza mapafu kulikosababishwa na damu kuvia kwenye mapafu kulikosababisha na adhabu aliyopewa shuleni na kupigwa teke mbavuni.
Lakini chunguzi wa kitaalamu wa mwili wa marehemu uliofanywa na mtaalamu wa patholojia wa hospitali ya Mount Meru Jijini Arusha alikofia na kushuhudiwa na ndugu, umebaini mapafu yake yalikuwa yamejaa maji.
Hata hivyo, pamoja na majibu hayo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema kwa sasa wamechukua sampuli zaidi na kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
“Taarifa ya awali ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa huyu mwanafunzi ilionyesha chanzo cha kifo ni mapafu yalijaa maji, lakini tumeenda mbali zaidi katika uchunguzi ili tujiridhishe tusibaki kwenye kitu kimoja.
“Mimi si daktari kuweza kuelezea sana, tunasubiri majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ndipo tutoe uamuzi,” alisema Kamanda Maigwa bila kuthibitisha au kukanusha kama wanaendelea kumshikilia mwalimu mkuu ama la.
Februari 22, Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, lilimkamata kwa mahojiano mkuu wa shule ya sekondari ya Bishop Alpha Memoria High School Moshi, Naaman Samwel kutokana na kifo cha mwanafunzi huyo mkazi wa Arusha.
Shule hiyo iliyopo Pasua Manispaa ya Moshi, inamilikiwa na Dayosisi ya Mlima Kilimanjaro ya Kanisa la Anglican nchini Tanzania na ndugu wanashikilia msimamo kuwa na hisia kuwa kifo cha mwanafunzi huyo kilitokana na kipigo cha mwalimu. Kulingana na ndugu hao, wanadai Februari 13, 2023, mwanafunzi huyo alipewa adhabu ya kupiga pushapu na katikati alishindwa na kuanguka na mwalimu aliyempa adhabu, alimpiga teke sehemu za mbavu.
Baada ya tukio hilo, wanafunzi wenzake walimchukua na kumpeleka bwenini na hakuweza kuingia darasani kwa siku nne na ndipo Februari 16, baba mzazi alipigiwa simu na kwenda kumchukua na kwenda naye nyumbani Arusha.
Esther Kimaro, bibi wa marehemu alidai walipofika nyumbani mtoto huyo alimweleza baba yake kuwa alipewa adhabu na kupigwa teke, na baadaye hali ilibadilika kumpeleka hospitali ya Mount Meru.
Kwa upande wake, mama mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Neema, alisema baada ya kufikishwa hospitali alipatiwa matibabu, lakini baadaye hali ilibadilika na kulazwa ICU na kupoteza kufariki dunia Februari 19.