Connect with us

Kitaifa

Shauri watu waliopotea, kuuawa kujulikana Machi

Dar es Salaam. Hatima ya uhai wa kuwepo mahakamani shauri la watu waliokumbwa na madhila ya kupotea, kushambuliwa na kuuawa sasa kujulikana Machi 22, 2023, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itakapotoa uamuzi wa pingamizi la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuhusu uhalali wake.

Shauri hilo limefunguliwa na mwanahabari, Luqman Maloto dhidi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na DPP.

Katika shauri hilo la mwaka 2023, Maloto pamoja na mambo mengine, anaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa DCI anawajibika kwa maisha ya watu waliopotea, walioshambuliwa, walioteswa na waliouawa kwa kuwa wajibu wake ni kulinda maisha ya Watanzania.

Maloto amewataja waathirika hao kuwa ni pamoja Azory Gwanda na wanasiasa Ben Saanane, Simon Kanguye, Daniel John, Tundu Lissu, Mdude Mpaluka Nyagali, maarufu Mdude, Leopord Lwajabe.

Wengine walioathirika ni Akwilina Akwilini, Ibrahim Mshana, maarufu kama Roma Mkatoliki na Allan Kiluvya.

Pia anaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa DCI ameshindwa ama kwa kutokuwa na uwezo au kwa makusudi kufanya upelelezi kuhusu madhila yaliyowakuta watu hao, kutokana na kushindwa kutoa taarifa kwa umma na kwa familia za waathirika hao kuhusu madhila yaliyowapata.

Anaiomba pia Mahakama itamke kuwa kuchelewa au kushindwa kukamilisha upelelezi dhidi yao, hakuongozwi na kanuni yoyote. Hivyo itoe amri dhidi ya DCI kuwasilisha mahakamani hapo taarifa yenye maelezo ya kina kuhusu kupotea, kuuawa na kuteswa kwao, kwa uchunguzi zaidi.

Hata hivyo, DPP ambaye ni mjibu maombi wa pili, ameweka pingamizi la awali akiwasilisha hoja sita akiiomba Mahakama hiyo ilitupilie mbali shauri hilo bila hata kusikiliza hoja msingi.

Awali, wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa tuhuma au matukio anayoyalalamikia Maloto, yametokea katika mikoa Mbalimbali.

Alisema matukio hayo yalifanyika katika mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma na Rufiji (Pwani), hivyo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam haina mamlaka ya kusikiliza shauri la matukio yaliyofanyika nje ya mamlaka yake.

DPP pia anadai kuwa kiapo chake ambacho ni miongoni mwa viapo vinavyounga mkono maombi hayo kina kasoro ya kisheria.

Akifafanua hoja hiyo, wakili Kishenyi alidai kuwa kuna aya zinazoelezea habari za uvumi hasa kuhusiana na habari za Azory, Lissu, Saanane na Roma.

Alisema ni za uvumi kwa kuwa hakuna viapo vya waathirika hao wenyewe kuthibitisha taarifa hizo au viapo vya watu walioshuhudia matukio hayo.

Hoja nyingine ya pingamizi ni kutokumshtaki Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), ambaye ndiye mkuu wa chombo hicho hivyo ndiye aliyepaswa kushtakiwa.

Pia kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye anapaswa kushtakiwa kwa mashauri yanayoihusu Serikali.

Hoja nyingine DPP anadai kuwa mwombaji (Maloto), hana masilahi katika shauri hilo, kwa mujibu wa Ibara ya 26(2), 30(3).

Akijibu hoja hizo, wakili wa Mwasipu alidai kuwa katika shauri la jinai Mahakama Kuu kwa mujibu wa Ibara ya 108(2) ya Katiba ya Tanzania ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Alidai kuwa ni kesi za madai pekee ndio sheria inasema kuwa shauri lifunguliwe mahali tukio lilikotokea.

Kuhusu hoja ya kasoro za kiapo, Mwasipu alidai kuwa taarifa zilizomo si uvumi kwa kuwa mwombaji ametaja chanzo chake.

Hata hivyo alidai kuwa kama Mahakama itaona kuwa aya zilizolalamikiwa zina kasoro, hata ikiziondoa zitakazobakia bado zinajenga msingi wa kesi kuendelea kusikilizwa.

Kuhusu kutokumshtaki IGP wakili Mwasipu alidai kuwa DCI ndiye mwenye dhamana na hata kutokuwepo kwa IGP hakuna athari yoyote na kuhusu kutokumshtaki AG, alidai kuwa sharti hilo linatumika katika mashauri ya madai.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi