Kitaifa
Mafuriko huku, ukame kule
Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitoa tahadhari ya mvua kubwa za Masika zinazoweza kusababisha mafuriko kwa baadhi ya maeneo, wadau wameeleza walivyojipanga kudhibiti madhara endapo yatatokea.
Kwa upande mwingine, TMA pia imetaja maeneo mengine yatakayopata mvua za wastani na chini ya wastani ikitoa ushauri kwa wakulima kupanda mazao yanayohimili ukame.
Mikoa inayotarajiwa kupata mvua za juu wastani ni Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro pamoja na Kisiwa cha Unguja, Zanzibar.
Hayo yalielezwa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a wakati akitoa utabiri wa mvua za masika katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua, zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi ujao hadi Mei.
Dk Chang’a alisema baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua chini ya wastani zitakaosababisha upungufu wa unyevu kwenye udongo na upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Kwa mujibu wa Dk Chang’a, mikoa itakayopata mvua za wastani au chini yake ni Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Madhara, jinsi ya kuepuka
“Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani na juu ya wastani, mvua hizo zitasababisha unyevu wa udongo kupita kiasi na kuathiri ukuaji wa mazao yasiyohitaji maji mengi. Pia yanaweza kuathiri ukuaji wa mazao kama mahindi na jamii ya mikunde yanayolimwa katika maeneo hayo.
“Mamlaka za miji zinashauriwa kuiboresha na kutunza mifumo ya mifereji ya maji ili kupunguza athari za maji pamoja na mafuriko yanayoweza kujitokeza,” alisema Dk Chang’a.
Kuhusu mikoa itakayopata mvua za wastani wa chini, Dk Chang’a alisema viwango vya maji katika mito na mabwawa havitarajiwi kuathirika zaidi.
Hata hivyo, alisema baadhi ya maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chache zenye mtawanyiko hafifu, alizataka menejimenti za maafa kuchukua hatua, hasa katika maeneo yanayotarajiwa kuwa na upungufu wa mvua, akisema hali hiyo inaweza kusababisha upungufu wa chakula, malisho ya mifugo na maji.
Kutokana na hali hiyo, TMA imewashauri wa wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati na kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba kwa ajili ya msimu huu wa Masika.
Vilevile imeshauri wakulima waimarishe miundombinu ya kilimo, uvunaji maji ya mvua na kudhibiti visumbufu vya mimea ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wa wafugaji, kasha maeneo yatakayopata mvua kidogo, TMA imeshauri kutumia mbinu bora za ufugaji kama vile malisho ya mzunguko ili kutunza malisho na kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya baadaye huku wakifuatilia tabiri za hali ya hewa na ushauri kutoka kwa maofisa ugani.
Kuhusu usafiri na usafirishaji, mamlaka hiyo imesema matukio ya hali mbaya ya hewa yanaweza kuharibu miundombinu ya barabara na reli na kusababisha kuchelewa au kusitishwa kwa safari za ndege, mawasiliano hafifu angani na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji katika usafiri wa anga.
Hata hivyo, TMA imesema sekta ya usafirishaji, hususan ya usafiri wa nchi kavu, inatarajiwa kunufaika katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
“Tuko tayari”
Kufuatia taarifa hiyo ya TMA, Idara ya maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu na viongozi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wameeleza utayari wao katika kukabiliana hali itakayojitokeza.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Msaidizi
Idara ya Menejimenti ya Maafa anayeshughulikia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, Prudence Constantine alisema wapo tayari wakati wote, ingawa hawaombei maafa kutokea lakini yanapotokea wanakibiliana nayo.
“Kama TMA imeshatangaza, maeneo yaliyotajwa yanapaswa kuchukua tahadhari mapema, wakuu wa mikoa na wilaya wanapaswa ‘ku-react’ (kufanyia kazi) moja kwa moja, sisi utayari wetu ni kwa ngazi ya kitaifa.
“Tupo tayari wakati wote kukabiliana na majanga yanapotokea, tuna miongozo na wananchi wana nafasi yao maafa yanapotokea na kila janga linakabiliwa kulingana na lilivyokuja.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge alisema kwa kuwa hakuna mito au mifereji mikubwa iliyopita katikati ya makazi ya watu mkoani mwake, jambo la linalopaswa kufanyika ni kuweka mazingira katika hali ya usafi na kukwepa utupaji wa taka kiholela.
Alisema licha ya jiografia mkoani wa Pwani kutokuwa na uwezekano mkubwa wa kupata mafuriko, wao wamekuwa na utaratibu wa kusafisha mito na kuhakikisha wanazuia uchepushaji wa maji.
“Wapo wanaochepusha maji na kuingiza kwenye mashamba, hili ni hatari kwa sababu yanapoongezeka yanaweza kuleta madhara kwa jamii ikiwemo kuharibu mashamba yenyewe,” alisema Kunenge.
Naye Gerald Sondo, mratibu wa maafa Mkoa wa Dar es Salaam alisema kunapokuwa na viashiria vyovyote vya maafa huwa wanazingatia utayari.
Alisema taarifa inapotolewa ofisi ya mkoa inashirikisha wadau ikiwemo Jeshi la Polisi, TMA, hospitali na viongozi wa dini.
“Muda wote tuko tayari kukabiliana na maafa, lakini jambo kama hilo lazima kushirikisha wadau na kutoa elimu kwa jamii hasa kwa wale wanaoishi maeneo hatarishi. Wanaoishi mabondeni na maeneo hatarishi hutaakiwa kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara,” alisema.
Akizungumzia upungufu wa mvua, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk Yahya Nawanda alisema tangu mwaka jana mkoa huo umeweka mkakati ya kukabiliana na hali hiyo kwa kuwashauri wakulima kulima mazao yanayostahimili ukame.
“Tumewashauri walime mazao yanayokomaa kwa muda mfupi kuanzia siku 75 hadi 90 badala ya yale ya siku kuanzia 120,” alisema Dk Nawanda.
Dk Nawanda alisema Serikali pia imewasisitizia wakulima kutumia vema mavuno yao na kuweka akiba kwa matumizi ya baadaye.
Matukio ya mafuriko hapa nchini hutokea mara kwa mara katika maeneo tofauti na kusababisha madhara kadhaa.
Mwaka 2012, zaidi ya kaya 500 zilihamishiwa katika eneo la Mabwepande baada ya makazi yao ndani ya jiji la Dar es Salaam kukumbwa na mafuriko, jambo ambalo lilifanya Serikali kuwagawia viwanja katika maeneo hayo.
Pia, kukosekana kwa miundombinu ya kupitisha maji kumeendelea kuathiri mikoa na maeneo mbalimbali na kusababisha mafuriko ambayo huathiri watu na makazi yao.
Novemba 2015, zaidi ya kaya 100 katika maeneo ya Magaoni mkoani Tanga, zililazimika kuhama makazi kutokana na nyumba kuzingirwa na maji baada ya mvua kubwa kunyesha.
Mbali na makazi na watu, pia mafuriko huwa yanaathiri miundombinu ya barabara na reli na wakati mwingine kusimamisha shughuli za usafirishaji.
Hali hiyo ilijitokeza Januari mwaka huu, mkoani Morogoro baada ya mvua kusababisha madhara mbalimbali kwa wakazi wa mkoa huo ikiwa ni pamoja na mafuriko na foleni ya magari katika barabara ya Morogoro – Dodoma.