Connect with us

Kitaifa

Matumaini mapya tiba ya Ukimwi

Wakati kukiwa na taarifa kuwa mgonjwa wa tano jijini Dusseldorf nchini Ujerumani ametibiwa na kupona kabisa ugonjwa wa Ukimwi, nchini Tanzania Serikali imesema bado inaendelea na utafiti wa matibabu hayo, kwani bado kuna utata wa njia inayotumika kutibu na wagonjwa hao kupona.

Mgonjwa huyo, aliyepewa jina la ‘the Dusseldorf Patient’ mwenye umri wa miaka 53, watafiti wamesema ni wa tano kupona kabisa maradhi hayo tangu kuingia kwa ugonjwa huo mwaka 1980.

Mgonjwa huyo alitibiwa na kufuatiliwa kwa miaka minne tangu mwaka 2019, kabla ya wataalamu hao kujiridhisha kuwa hana tena virusi vya ugonjwa huo unaouisumbua dunia kwa zaidi ya miongo minne sasa, kwa mujibu wa Shirika la CBC News ya Marekani.

Tangu walipotangaza kumtibu mgonjwa huyo mwaka 2019, watafiti hao walikuwa hawajajiridhisha kwamba amepona kweli, hivyo kulazimika kumfuatilia kwa ukaribu na jana wakatangaza kila kitu kimekwenda sawa.

“Ni tiba halisi, ya kweli na ya kudumu. Matokeo haya chanya yanaleta matumaini lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya,” alisema Dk Bjorn-Erik Ole Jensen, alipowasilisha taarifa za utafiti wao kwenye Jarida la Nature Medicine.

Kauli ya Tacaids

Akizungumzia utafiti huo Ofisa Mwitikio wa Taasisi za Umma wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) , Dk Hafidh Ameir alisema njia ya kupandikiza seli za shina (Stem cells) iliyojaribiwa kutibia virusi vya Ukimwi (VVU), ipo majaribioni kwa sasa kwa muda mrefu na tiba hiyo hutumika kwa wagonjwa wenye saratani.

“Njia hii ni ghali na ni ngumu, ilikuwa ikitumika kutibu saratani lakini baadaye wakagundua inaweza kuondoa shina la virusi, lakini sasa shida ya njia hii ina madhara makubwa, mtu anayepandikizwa seli za shina ni lazima apewe dawa ya kuzuia kinga yake ya mwili isipambane na pandikizo hilo kwa maisha yake yote. “Lengo ni kuhakikisha seli za shina anazopandikizwa kutoka kwa mtu mwingine hazimletei madhara,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba imeripotiwa kusaidia kuondoa uwepo wa VVU mwilini, ila njia hiyo husababisha kinga ya mtu kushuka kutokana na mabadiliko ya ghafla yaliyotokea mwilini mwake, hali inayotokana na kinga za mwili kuanza kupambana zenyewe kwa zenyewe.

Alisema hadi sasa VVU haina chanjo zaidi ni tiba ya kupunguza makali yake (ARVs), na utafiti unaoendelea kufanyika duniani bado ni wa majaribio tu.

Teknolojia iliyotumika

Watafiti walitumia teknolojia ya upandikizaji uboho (stem cell transplant) ambayo imezoeleka kwa wagonjwa wa saratani na selimundu.

Teknolojia hiyo ni hatari kutokana na uwezekano wa mgonjwa kupoteza maisha wakati wa upasuaji, huzibadilisha kabisa kinga za mwili za muhusika na kupandikiza mpya. Miaka minne iliyopita, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kilianza kutoa tiba hiyo nchini kwa wagonjwa wa selimundu, lakini miaka ya hivi karibuni magonjwa mengine yanatibika ukiwamo Ukimwi.

Virusi vya Ukimwi hushambulia kinga za mwili na mashambulizi yakidumu muda mrefu huufanya mwili wa mgonjwa ushindwe kupambana na maradhi madogomadogo.

Mtu wa kwanza kutibiwa na kuthibitishwa amepona Ukimwi alikuwa Timothy Ray Brown, mzaliwa wa Seattle nchini Marekani. Watafiti walichapisha taarifa zake wakimwita “the Berlin patient” mwaka 2009. Akafuatiwa m wingine aliyetibiwa jijini London miaka 10 baadaye. Hivi karibuni, mgonjwa mwingine alitibiwa huko City of Hope na New York, Marekani na taarifa zao kuchapishwa mwaka jana. “Nafikiri tunaweza kupata mengi ya kujifunza kutoka kwa mgonjwa huyu na wengine wa aina yake. Kutokana na majibu yaliyopatikana tutapata uelekeo wa nini cha kufanya kuelekea kuipata tiba ya uhakika,” alisema Dk Jensen.

Wagonjwa wote watano wamepandikizwa uboho kutibu saratani ya damu waliyokuwa nayo hata waliowachangia damu nao walikuwa na kinga ya kupambana na virusi vya Ukimwi ambayo ni protini iitwayo CCR5. Upandikiaji wa uboho ni upasuaji unaohitaji umakini mkubwa na ni hatari zaidi kuufanya kwa yeyote mwenye maambukiziya Ukimwi ingawa madaktari wamekuwa wakileta namna mpya kila wanapofanikiwa kumtibu mgonjwa.

Matumaini kwa wenye VVU

Licha ya matokeo hayo, Hellen Thomas mwalimu mstaafu anayeishi na maambukizi ya Ukimwi kwa zaidi ya miaka 20 alisema ana mashaka na utafiti huo kwani unaweza kuwafanya watu wengi kuacha dawa za kufubaza makali virusi vya Ukimwi.

“Siwezi kuamini utafiti huu, tangu mwaka 2004 nilipoanza kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi ninachojua unapotumia dawa vizuri virusi havionekani lakini usipotumia virusi vinazidi kuwa vingi mwilini,”alisema. Naye Alex Juma (si jina halisi )kutoka mkoani Kilimanjaro alisema hiyo ni habari njema kwa wenye maambukizi, lakini mbaya zaidi kwa wasio na maambukizi kupuuza tahadhari kutokana na fununu hizo. “Kwetu sisi ni habari njema japo hakuna uhakika kamili juu ya haya matibabu, kwa wasio na ugonjwa huu kwao itawafanya kujiachia zaidi,”alisema.

Tafiti nyingine za Ukimwi

Katika jitihada za kutafuta tiba ya ugonjwa huu, Agosti 2021, kampuni ya Moderna ya Marekani ilianza kufanya utafiti wa chanjo ya virusi vyake kwa wagonjwa 56. Kampuni hiyo bado inaendelea na utafiti wa chanjo za aina mbili za Ukimwi ambazo zimeshafuzu hatua za awali za majaribio, hivyo kuanza kutumika kwa binadamu katika awamu ya tatu.

Chanjo hizo ni mRNA-1644 na mRNA-1644v2-Core, zilizofanyiwa majaribio ya awali na kuonekana kuwa salama kwa binadamu.

Kampuni ya Mordena inayo matumaini ya kuipata chanjo hiyo kutokana na teknolojia ya mRNA, inayoitumia ambayo ni sawa na iliyotumika kutengeneza chanjo ya Uviko-19 na kufanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90.

Wakati utafiti wa chanjo ya Ukimwi ukiendelea, Mei mwaka jana watafiti walitangaza kugundua mbinu mpya ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), kwa wanawake.

Watafiti hao walileta pete maalumu iitwayo ‘Dapivirine Vaginal Ring’ inayopewa nafasi kubwa ya kushusha maambukizi kwa wanawake kwani ina madini ya silikoni na ikivaliwa ukeni hudumu kwa siku 28 kutoa dawa kinga inayoua virusi hivyo. Kinga hiyo imekuja baada ya utafiti wa miaka zaidi ya 10 kufanyika nchini Marekani na Afrika na mwaka 2020 Shirika la Afya Duniani (WHO), liliruhusu kutumika na mpaka sasa nchi nne zimeanza kuitumia ikiwemo Afrika Kusini, Uganda, Zimbabwe na Malawi huku Tanzania ikiendelea kuifuatilia kabla ya kuiingiza nchini ianze kutumika.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi