Kitaifa

Sintofahamu kivuko cha Mv Magogoni

Dar es Salaam. Gharama za ukarabati wa kivuko cha Mv Magogoni kwa Sh7.5 bilioni  wakati chenyewe kilinunuliwa kwa Sh8 bilioni umeendelea kugonga vichwa na kuibua maswali juu ya uhalali wa kiwango hicho cha fedha.

Katika mjadala huo mambo yaliyoibuka ni pamoja na zabuni ya ukarabati huo kutolewa kwa kampuni ya kigeni badala ya kampuni za ndani, huku wengine wakihoji kuwa fedha zote hazikuwa kwenye bajeti ya mwaka huu.

Kufuatia maswali na hoja zilizoibuka katika mitandao ya kijamii baada ya Serikali kutangaza ukarabatiwa wa kivuko hicho Februari 16, 2023, Mwananchi imezungumza na watalaamu mbalimbali wenye uzoefu katika eneo hilo huku Serikali ikifafanua kwa nini gharama hizo ni kubwa.

Kivuko cha Mv Magogoni kilichoanza kazi mwaka 2008 kikiwa na uwezo wa kubeba tani 500 (sawa na abiria 2,000 na magari madogo 60), ni kiunganishi muhimu kati ya Kigamboni na Magogoni.

Alipoulizwa kwa simu jana ukubwa wa gharama hizo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,  Profesa Makame Mbarawa alisema kuhusu suala hilo Temesa (Wakala wa Ufundi na Umeme) wamelitolea ufafanuzi vizuri.

Kuhusu hoja ya kwa nini kazi hiyo haikutolewa kwa kampuni ya ndani, Mbarawa alisema, zabuni hiyo ilikuwa ya kimataifa na kampuni ya Kitanzania iliishindania kwa kuweka kiwango kikubwa zaidi, yaani Sh10 bilioni.

“Wanaosema tungewapa kazi kampuni ya ndani wanatakiwa kujua kuwa tenda ilikuwa wazi nao walishiriki lakini gharama zao zilikuwa kubwa, lakini hata wengepewa wao hizo fedha zisingebaki nchini, kwa kuwa kazi kubwa inahusisha ununuzi wa vitu ambavyo vinapatikana nje ya nchi,” alisema Profesa Mbarawa.

Akizungumza Februari 16 mwaka huu wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya ukarabati huo, Profesa Mbarawa alisema wakati wa kutoa zabuni Serikali inaangalia mambo mawili makubwa; “Jambo la kwanza ni bei, nani ni mwenye gharama za chini, kama alivyosema mtendaji mkuu Temesa, mkandarasi ambaye alikuwa na bei ya chini alikuwa na Sh7.5 bilioni, aliyemfuatia alikuwa na Sh 10 bilioni, tofauti ya Sh2.5 bilioni, kama hizi ni pesa zako wewe utampatia nani mkataba wa kazi hiyo?

Miongoni mwa kampuni za ndani zilizoomba zabuni hiyo ni kampuni ya Songoro Marine ambayo mkurugenzi wake mkuu, Major Songoro alililieleza Mwananchi jana kuwa waliomba kazi hiyo kwa Sh10 bilioni kutokana na uhalisia wa gharama za vifaa.

Songoro alisema Sh7.5 bilioni kwa shughuli hiyo si gharama kubwa kwa kazi inayokusudiwa kufanyika, hivyo hana uhakika kama fedha hizi zitakamilisha kazi na ana wasiwasi kiwango kilichotajwa kwa ajili ya matengenezo hayo ni kidogo ikilinganishwa na gharama za vifaa zilivyo sasa.

“Ukweli ni kwamba gharama za hayo matengenezo ziko juu na hata hao waliosema Sh7.5 bilioni sijui wamejipangaje ila ninachofahamu zitaongezeka, bei za vifaa ziko juu na karibu vyote vinatoka nje, sasa hicho kiwango walichosema sielewi na sijui kama Serikali nayo kama imejipanga kuongeza ili kukamilisha kazi,” alisema.

Kiwango husika

Kwa mujibu wa ufafanuzi Meneja Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini, Lukombe King’ombe akizungumzia ukarabati huo, alisema aliyeshinda zabuni atatumia dola za Marekani 90,000 (Sh209 milioni) kwa ajili ya injini na gia boksi zake na zinatakiwa zifungwe nne na moja ya akiba, ambayo itakuwa inatumika pindi moja wapo inapokuwa katika matengenezo.

Alisema yeye ameitembelea kampuni ya Africana Marine ya Kenya  iliyoshinda tenda hiyo na kujiridhisha kuwa ina uwezo wa kufanya kazi hiyo.

 Alisisitiza kuwa matengenezo makubwa kama haya yana gharama kubwa kama ilivyo kwenye gari ambako bei huwa karibia na nusu ya manunuzi; na kwa vyombo vya majini gharama ni kubwa zaidi.

King’ombe alijibu pia hoja ya uwezekano wa kununua kivuko kipya badala ya kukarabati  cha sasa akisema: “Kwa wanaouliza kwanini hatujanunua kivuko kipya thamani ya kivuko kipya kama hiki cha Mv Magogoni si chini ya Sh25 bilioni.”

Mapema, siku ya kutia saini mkataba huo, Mtendaji Mkuu wa Temesa, Lazaro Kihalala alisema kazi ya ukarabati wa kivuko hicho itahusisha kazi za chuma, kuondoa mabati yaliyochakaa ya muundo wa chini na wa juu, ujenzi wa milango mipya ya kushushia na kupakia abiria, ukarabati wa chumba cha kuongozea kivuko, ufungaji wa injini mpya nne aina ya caterpillar pamoja na gia boksi zake.

Pia itahusisha matengenezo makubwa ya pampu jeti, marekebisho makubwa ya mfumo mzima wa umeme na kielektroniki, kufunga kangavuke (majenereta) mapya mawili, mfumo wa tahadhari ya moto, kufunga kamera za CCTV, kuweka vifaa vya kisasa vya kuongozea kivuko, vifaa vya tahadhari na vya uokoaji, pamoja na kupaka rangi kivuko chote.

Wakati watendaji hao wa Serikali wakieleza hayo, mhandisi mmoja wa meli ambaye amefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 20 ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema Sh7.5 bilioni hazina uhalisia kwa kuwa  sehemu kubwa ya gharama ni kwenye ununuzi wa injini, gia boksi na jenereta; kwa kuwa chuma na mabati havichakai vyote kwa wakati mmoja.

“Injini za caterpillar zinazofaa na gia boksi zake ambazo zitawekwa katika kivuko hicho gharama yake hazizidi Sh300 milioni kila moja na ziko nne sawa na Sh1.2 bilioni na hiyo ndiyo kazi kubwa, nyingine ni ndogo ndogo,” alisema akifafanua kuwa hesabu zikipigwa upya bei hiyo inaweza kupungua.

Bajeti yake

Katika bajeti ya ujenzi na uchukuzi ukarabati huo wa kivuko cha Mv Magogoni haujatajwa licha ya kuwa Temesa ilitengewa Sh5.52 bilioni kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wwa vivuko kadhaa ikiwemo Mv Magogoni na kufuatilia, kutathmini miradi hiyo ya ukarabati.

Bajeti hiyo ni ya vivuko vya Mv Musoma, Mv Mara, Mv Temesa, Mv Kome II, Mv Misungwi, Mv Nyerere, Mv Kyanyabasa, Mv Kitunda, Mv Kazi, Mv Magogoni, Mv Tanga pamoja na ukarabati wa kivuko cha Mv Kilombero II na kukihamishia Mlimba – Malinyi.

Hata hivyo kwenye mgawanyo wa fedha za bajeti ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/23 zimetengwa Sh420 milioni kwa ajili ya ukarabati wa Mv Kazi na Mv Magogoni.

Akizungumzia suala hilo Waziri Mbarawa alitaka rejea iwe kitabu cha bajeti na kuwa kuna utaratibu wa advance payment (malipo ya awali) na si lazima fedha zote ziwekwe kwenye akaunti kwa wakati mmoja kwa kuwa zinaweza zikapangwa kidogo kidogo.

Njia Mbadala

Huku suala la vivuko likizidi kusumbua jijini Dar es Salaam, watalaamu mbalimbali wameshauri njia nyingi mbadala zinazoweza kusaidia katika eneo la Magogoni-Kigamboni, kama daraja au handaki badala ya kutumia vivuko.

Hata hivyo, Profesa Mbarawa alisema kujenga daraja au handaki zote ni njia zinazohitaji kiwango kikubwa cha fedha lakini pia kihandisi hesabu yake ni ngumu.

“Kwenye uhandisi hamna kisichowezekana, inawezekana kujenga handaki au kuwa na daraja la juu ambalo meli zinaweza kupita chini, lakini njia zote hizo zinahitaji eneo kubwa kwa kuwa daraja haliwezi kuinukia na kuibuka katika umbali mfupi kama ule.

“Ni rahisi kuwa na miradi kama hiyo eneo lenye urefu walau wa kilometa 3 au nne,” alisema Mbarawa akisema umbali ulipo ni mita 400.

Alisema hata upatikanaji wa fedha za kutekeleza mradi kama huo ni changamoto kwa kuwa idadi ya magari yanayotumia eneo hilo ni ndogo, hata ukisema uweke gharama za kupita, itachukua muda mrefu kurejesha gharama za uwekezaji, iwapo utasema uwe mradi wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi.

Kulingana na mapendekezo hayo yanayotokana na kilichofanyika katika nchi mbalimbali, upo uwezekano wa kuweka daraja kutoka Kivukoni hadi Kigamboni Feri au handaki chini ya bahari kuunganisha maeneo hayo muhimu.

Hata hivyo, changamoto iliyopo ni kuwa eneo hilo ni lango la bandari ambao ni muhimu la kiuchumi hivyo hofu iliyopo ni kuziba mlango huo.

Licha ya changamoto hiyo, kutokana na maendeleo ya teknolojia kuna madaraja ya aina nyingi yanayoweza kujengwa eneo lile na kuondoa ulazima wa kutumia vivuko, ukizingatia kuwa njia ya barabara inaweza kusafirisha watu wengi zaidi na kwa haraka kuliko vivuko.

Tofauti na daraja wa Julius Nyerere linalounganisha Kigamboni na Kurasini, eneo la Magogoni na Kigamboni panaweza kuunganishwa na daraja la juu ambalo linakuwa na urefu wa mita 70 kutoka usawa wa bahari, urefu ambao hauwezi kufikiwa na meli zote za mizigo zilizopo sasa na pengine zinazojengwa.

Meli ndefu zaidi kuliko zote iliyopo hivi sasa ni The Ever Ace ambayo urefu wake kwenda juu ni mita 75.7 lakini ikiwa kwenye maji eneo linalobakia kuanzia usawa wa maji ni mita 61.5.

Mfano wa madaraja yaliyopo ambayo meli ya namna hiyo inaweza kupita chini yake bila wasiwasi ni daraja la 1915 Çanakkale Bridge nchini Uturuki ambalo linakatiza katika eneo la maji kwa umbali wa kilometa 4.6 kwenye maji na upana wa mita 45.  Lilijengwa kwa miaka mitano hadi 2022 na kutoka usawa wa maji inaweza kupita meli hadi yenye urefu wa mita 70.

Gharama ya daraja hilo ni Dola za Kimarekani 2.7 bilioni (Sh6.3 trilioni).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi