Kitaifa

Kesi ya uraia pacha kuanza kusikilizwa Mei 2

Telegram

Dar es Salaam. Kesi ya uraia pacha iliyofunguliwa na Watanzania sita wanaishi na kufanya kazi nje ya nchi sasa itaanza kusikilizwa Mei 2, 2023, katika hatua ya awali ya mapingamizi ya Serikali.

 Kesi hiyo ya Kikatiba namba 18 ya mwaka 2022 imefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu na  Shaban Fundi, Patrick Nyelesa  Nhigula, Restuta Kalemera, Nkole Muya, Emmanuel Emmanuel na Bashir Kassam dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika kesi hiyo Watanzania hao wanapinga sheria ya Uraia hasa vifungu vinavyozuia huo uraia pacha hasa kifungu cha 7(1) na (2) (c), (4)(a) (6) vya Sheria ya Uraia ambavyo wanadai kuwa vinakiuka haki zao nyingine za Kikatiba

Hivyo wanaiomba mahakama itamke kuwa vifungu hivyo ni batili wakidai kuwa vinakiuka haki zao za Kikatiba kwa kuwa vinawanyanya haki ya asili isiyonyang’anyika yaani uraia wa kuzaliwa.

Kesi hiyo iliyopangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mustafa Ismail akishirikiana na  jaji Hamidu Mwanga na jaji Obadia Bwegoge imetajwa leo kwa mahakamani hapo mara ya kwanza leo Jumatatu, Februari 2023 mbele ya majaji wawili, Mwanga na Bwegoge.

Wakili wa wadai, Peter Kibatala ameieleza mahakama kuwa wadaiwa wameshajibu madai yao kwa maandishi na pia wamewasilisha pingamizi la awali.

Mdaiwa, Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewakilishwa na Wakili wa Serikali, Ayub Sanga.

Nje ya Mahakama wakili Kibatala amezitaja hoja za pingamizi hili kuwa ni pamoja na kuna kasoro za kisheria katika hati za viapo vya wadai.

Nyingine ni kwamba hati ya madai kutokusainiwa na wadai pamoja na wakili wao na kwamba kesi hiyo inakiuka masharti ya lazima ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Utekelezaji Wajibu na Haki, katika kutafuta haki za Kikatiba.

Kutokana na kuwepo pingamizi hilo la Serikali, kama ilivyo kawaida mahakama imepanga kulisikiliza kwanza pingamizi hilo kabla ya kusikiliza kesi ya msingi na imepanga kulisikiliza Mei 2, 2023, mbele ya jopo kamili, akiwemo kiongozi wa jopo ambaye jana hakuwepo.

Wakati kesi hiyo ilipotajwa, wadai ambao wote sita ambao wako nje ya nchi hawakuwepo mahakamani badala yake waliwakilishwa na Liberatus Mwang’ombe aliyesafiri kutoka Washington DC. Marekani kwa ajili hiyo, akiungana na wadau wengine wa uraia pacha walioko hapa nchini.

Kwa mujibu wa viapo vyao, hawa ni Watanzania kwa kuzaliwa walioondoka nchini na kwenda ughaibuni kwa nyakati tofautitofauti hususani katika nchi za Marekani, Uingereza na Canada wanakoishi na kufanya kazi ambako pia walishapata uraia.

Katika viapo vyao wanaeleza kuwa wameathirika sana kitendo cha kunyimwa haki mbalimbali katika nchi yao waliyozaliwa kwa kuzingatia kwamba walipata uraia wa nchi hizo kwa sababu za kiuchumi na ustaki wa kijamii tu.

Wanadai kuwa wao ni Watanzania kwa damu na kwamba wanatamani kuendelea kuwa Watanzania, lakini kwa vifungu hivyo vya Sheria ya Uraia wananyimwa haki hiyo.

Wanadai kuwa wenzao wanaotoka katika nchi nyingine za Afrika Mashariki kama vile Kenya, Rwanda na Uganda wanaoishi nje ya nchi wanaruhusiwa kuwa hati za kusafiria za Afrika Mashariki kwa kuwa nchi zao zinaruhusu uraia pacha lakini wao hawawezi kupata hati hizo.

Miongoni mwa haki wanazozikosa nchini walikozaliwa ni pamoja na kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi na kwamba wanapotembelea nchini wanaishia kuishi katika nyumba za ndugu zao au hotelini.

Wanataja haki nyingine wanazozikosa kuwa ni pamoja na kutokuchagua viongozi wala kushiriki kugombea nafasi ya umma katika uchaguzi nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi