Connect with us

Kitaifa

Sheikh Alhad atupwa nje kamati ya Mwezi Bakwata

Mufti mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar bin Zubeir ameivunja kamati ya Mwezi iliyokuwepo awali na kuunda kamati mpya ambayo Mwenyekiti atakuwa yeye mwenyewe.

Kamati hiyo imevunjwa ikiwa ni siku chache kabla Waislamu kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kuvunjwa kwa Kamati hiyo kunamuondoa, aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salim ambaye pia alikuwa Katibu wa Kamati ya mwandamo wa Mwezi Bakwata-Taifa.

Mabadiliko hayo yametangazwa leo Februari 18 na Katibu wa Baraza la Ulamaa na Msemaji wa Mufti wa Tanzania, Sheikh Said Hassan Chizenga wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa.

Amesema kamati hiyo pia itakuwa chini ya Katibu Muhammad Khamisi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Dini.

“Wajumbe wa kamati hiyo ni Sheikh Abdallah Myasi Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ally Muhudiin Mkoyogore Naibu kadhi Mkuu, Sheikh Haamid Masoud Jongo Mjumbe wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Mussa Hemedi katibu wa Mufti, Sheikh Waliid Al-haadi Omar Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam,” amesema.

Ili kuiongezea nguvu kamati hiyo, Mufti pia ameteua wajumbe wengine watano kutoka katika kanda zote za Tanzania.

Katika Kanda ya Kusini, Sheikh Nurudden Mangochi ameteuliwa kuwa mjumbe, Kanda ya ziwa, Sheikh Hassan Kabéke, Kanda ya magharibi Sheikh Uwesu Khalfani Kiumbe, Kanda ya Kaskazini, Sheikh Ally Juma Luwuchu, Kanda ya nyanda za juu Sheikh Msafiri Njalambaha.

Baraza pia lilitumia nafasi hiyo jitihada zinazofanyika katika kuhakikisha unafuu wa bei za vyakula na mahitaji mengine kwa wananchi, hasa katika kuelekea kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani.

“Baraza linawataka na kuwanasihi wafanyabiashara kuunga mkono jitihada hizi kwa kuacha tabia ya kupandisha bei za vyakula na mahitaji mengine.

“Kufanya hivyo kunawaumiza walaji na kunakwenda kinyume na jitihada za mheshimiwa Rais wetu na ni kinyume cha ucha Mungu,” amesema Chizenga.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi