Kitaifa
Ma-DC wapya wateuliwa, waapishwa kimyakimya
Wilaya za Mbogwe na Kyerwa zimepata viongozi wapya baada ya walioteuliwa Januari 25, mwaka huu kutoripoti kazini.
Walioteuliwa na kuapishwa kushika nyadhifa hizo juzi ni Sakina Mohamed anayekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita na Zaitun Abdallah aliyeteuliwa na kuapishwa kuongoza Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella na mwenzake Albert Chalamila wa Kagera hawakupatikana jana kuthibitisha kuwaapisha viongozi hao wa wilaya, lakini Mwananchi ilipata uthibitisho kuwa viongozi hao waliapishwa juzi kushika nyadhifa hizo.
Kabla ya kuapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina alikuwa mtumishi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Makao Makuu huku nafasi ya Zaitun kabla ya uteuzi haikujulikana mara moja.
Mwananchi ilifanikiwa kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Shigella kwa njia ya simu ambayo hata hivyo ilikatika ghafla baada ya kuulizwa kuhusu kumwapisha mkuu mpya wa Wilaya ya Mbogwe.
Kiongozi huyo hakupokea tena simu yake ya kiganjani hata ilipopigwa tena, kwani iliita mara kadhaa bila kupokelewa huku akijibu kwa kifupi ujumbe wa maandishi aliotumiwa kwa kusema; “niko barabarani,”
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Vicent Rubaga alithibitisha kuapishwa na kuhudhuria hafla ya uapisho wa mkuu mpya wa Wilaya ya Mbogwe.
“Ni kweli Mbogwe tumempata Mkuu wa Wilaya na tayari ameapishwa katika hafla tuliyohudhuria viongozi kadhaa wakiwemo wajumbe wa kamati ya ulinzi ya wilaya, viongozi wa CCM na Halmashauri ya Mbogwe,” alisema Rubaga.
Alisema kwa mujibu wa taarifa alizonazo, mkuu huyo mpya wa wilaya anatarajiwa kuripoti ofisini leo na wananchi na viongozi wa Wilaya ya Mbogwe wanamsubiri kwa hamu, ili washirikiane kujenga wilaya hiyo iliyokaa bila mkuu wa wilaya kwa takribani mwaka mzima sasa.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Charles Kabeho aliondoka kimya kimya bila kujulikana sababu za kutokuwepo ofisini na nafasi yake ilikaimiwa na Mkuu wa Wilaya jirani ya Bukombe, Said Nkumba.
Ofisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Ruth Binamungu licha ya kuthibitisha mkuu mpya wa Wilaya ya Kyerwa kuapishwa, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa sababu hakuhudhuria hafla ya uapisho.
“Taarifa za mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaitun Abdallah kuapishwa nimezipata kutoka wilayani Kyerwa kwa sababu sikuwepo ofisini wakati anaapishwa,” alisema Ruth
Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Wilaya ya Kyerwa, Deocres Kagunila aliithibitishia Mwananchi kuwa mkuu huyo mpya wa wilaya aliapishwa juzi Februari 15, mwaka huu.
Viongozi wa CWT
Kuteuliwa na kuapishwa kwa Sakina na Zaitun kuwa wakuu wa Wilaya za Mbogwe na Kyerwa kulikofanyika kimya kimya umeziba nafasi zilizobaki wazi baada ya viongozi wa juu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) walioteuliwa kushika nyadhifa hizo kutoripoti kwenye vituo vyao hadi kufikia jana.
Wakati Rais wa CWT, Leah Ulaya aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe; Katibu wake, Japheth Maganga aliteuliwa kuongoza Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Maganga na Ulaya waliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya Januari 25, mwaka huu, uteuzi ambao pia ulimwangukia aliyekuwa Makamu wa Rais wa CWT, Dinah Mathamani ambaye tayari ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Ulaya na Maganga ambao wanaendelea na nyadhifa zao ndani ya CWT hawakupatikana jana kuzungumzia nafasi zao kujazwa.