Kitaifa
Mwili wa bodaboda wakutwa msituni Dar
Dar es Salaam. Wakati bado tukio la kutekwa kwa Maliki Lukonge wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani, likiwa halijapata ufumbuzi, mwili wa mtu ambaye jina lake halijafahamika, umekutwa umetupwa kwenye msitu wa Pugu Kazimzumbwi wilayani Ilala, ukiwa na majeraha kwenye mikono na kutobolewa macho.
Akizungumza na Mwananchi jana, mjomba wa Lukonge, Audax Lukonge alisema wakati wanamfuatilia ndugu yao walipata taarifa ya kuokotwa kwa mwili wa mtu maeneo ya Pugu.
“Tumeuangalia mwili ule, lakini tumebaini siyo ndugu yetu,” alisema.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Bangulo Kata ya Stesheni wilayani humo, Gudluck Mohere alithibitisha kutokea kwa kwa tukio hilo na kueleza kwamba mwili wa kijana huyo anayekadiriwa kuwa na miaka 25-30 ulichukuliwa na polisi.
“Ni kweli jana ‘juzi’ asubuhi nilipigiwa simu na mjumbe wangu wa shina akanieleza kuna mwili umetupwa msitu wa Pugu -Kazimzumbwi kwenye hii barabara ya kutoka Pugu Mnadani kwenda Kifuru.
“Nilikwenda eneo la tukio, nikamkuta ni kijana akiwa na majeraha kwenye mikono na machoni, nahisi ni bodaboda aliyeporwa pikipiki au vinginevyo, inawezekana waliotenda ukatili huo walipotimiza dhamira zao ovu waliutupa mwili kwenye huu msitu huu, tuliwajulisha polisi ambao walikuja na kuuchukua mwili na kuondoka nao,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Debora Magiligimba, alipoulizwa kwa simu na Mwananchi, jana kuhusu tukio hilo alieleza kulifuatilia na atalitolea ufafanuzi.
Hata hivyo, Mwenyekiti Mohere alisema hilo si tukio la kwanza kutokea kwenye eneo la msitu huo kwa miaka ya hivi karibuni ambapo watu zaidi ya sita wamekutwa wamefariki katika mazingira kama hayo kwenye msitu huo.
“Ni kipande ambacho wananchi wanatupwa cha kama ekari 45 kirudi kwa wananchi, Serikali ikiweza kutupunguzia hii adha basi eneo ili walipangiwe kazi nyingine za kijamii, aidha michezo, makaburi, kujenga kituo cha afya au cha polisi inaweza kusaidia kukifanya kiwe salama na hata kuulinda huu msitu,” alisema.
Baadhi ya wananchi wa jirani na eneo hilo wameeleza kupitia changamoto za hofu ya kukabwa, kuporwa na hata kupoteza maisha.
“Niliwahi kucharangwa mapanga pale, nilinusurika kutobolewa macho na vibaka,” alisema mkazi mmoja wa Pugu aliyejitambulisha kwa jina la Chiando Masatu.
Aliendelea, “Nilikuwa narudi nyumbani saa 12 jioni, vijana watatu wakanifuata na kuniambia bro (kaka) tunaomba hela, niliwajibu kwani mimi shamba? Mmoja akasema kumbe baba mjeuri muonjeshe kwanza, wakanicharanga mapanga na mmoja kutoa msumari na kunichoma kwenye jicho la kulia.
“Bahati nzuri niliwahi kukinga mkono haukufika kwenye jicho, walinipora kila kitu na kutokomea. Ukabaji huku Pugu kwa sasa umekithiri,” alisema.
Mkazi mwingine wa Pugu Kajiungeni, Samwel Paul alisema wananchi wa eneo hilo wana matatizo mengi yanayotokana na eneo hilo, ambayo yamewachosha na kuomba Serikali iwasaidie kuboresha eneo hilo liwe salama kwao.
“Kuna dada tulimkuta kakabwa kavuliwa nguo mchana saa 9, sisi ndiyo tulimsaidia kumpa fulana na mmoja akampa pensi ili ajistiri, lakini eneo hili linatutesa wananchi,” alisema mkazi mwingine.