Kitaifa

Polisi mbaroni kwa madai ya utekaji

Mkuranga. Zikiwa zimetimia siku 14 tangu Maliki Lukonge alipotekwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha Koraga wilayani Mkuranga, giza nene limetanda kuhusu kupatikana kwake, huku Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji likiwa linawashikilia watu watatu akiwamo askari polisi wanaodaiwa kuhusika.

Jeshi hilo limewataka ndugu wa Lukonge kuwa wavumilivu wakati wanaendelea kufanya uchunguzi wao. Maliki alichukuliwa na watu wasiojulikana waliokuwa na gari linalotajwa kuwa ni Toyota Land Cruiser akiwa dukani kwake kijijini hapo saa 3 usiku.

Tukio lilitokea Februari 1 katika eneo la Korogwa Dundani Wilaya ya Mkuranga.Akizungumza jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Protas Mutayoba alisema bado wanaendelea na upelelezi hivyo ndugu wawe wavumilivu.

“Tunaendelea na uchunguzi, tumeshawahoji watu walioshuhudia tukio na wameandika maelezo yao na kuna watu wanaoshukiwa pia tumewakamata. Mpaka sasa tunashikilia watu watatu,” alisema.

Alisema miongoni mwa waliokamatwa ni askari Polisi mwenye uhusiano na mmoja wa watuhumiwa. “Tunafanya pia searching kuangalia watu aliokuwa akiwasiliana kabla ya kutekwa na kama mazungumzo hayo yanahusiana na tukio,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu madai ya ndugu wa Maliki ya kuchelewesha upelelezi, Kamanda Mutayoba alisema walipopata taarifa walianza kazi kwa taratibu zao ambazo si lazima wajue kila wanachokifanya.

“Kwa mujibu wa mashuhuda walisema kuna watu walifika nyumbani kwake wakiwa na gari muda wa jioni, wakamkuta akiwa kwenye fremu yake ya biashara.

“Wanaendelea kusema hao watu walimwita Maliki kisha wakamwingiza kwenye gari na kuondoka naye.

Ndipo majirani walipoona hali hiyo wakaanza kulikimbiza lile gari kwa pikipiki na bahati nzuri walinukuu namba za lile gari,” alisema.

Tukio lilivyokuwa

Mmoja wa askari mgambo wa kijiji hicho, Habibu Salum, alisema yeye na wenzake walikuwepo wakati wa tukio hilo na walifukuzia gari la watekaji bila mafanikio.

“Siku hiyo nilikuja hapa dukani, nikakuta gari hapa, Toyota Land Cruiser yenye mkonga nyeusi na ina mstari mweupe, kulikiwa na watu kama wanne wanazungumza na Maliki. Mimi sikutilia shaka, sikujua wanaongea nini.

“Ghafla wakati naongea na wenzangu, ikaja taarifa kuwa ile gari iliyoondoka imeondoka na Maliki, ni kama vile walimsukumia kwenye gari,” alidai shuhuda huyo.

Alisema, walishauriana na wenzake na kuamua kuifuatilia ile gari iliyokuwa ikielekea barabara kuu ya Lindi Mtwara.

“Tukaamua kuifukuzia tukaikuta maeneo ya Mtundani, tukaisoma namba, tuliendelea kuifuatilia kama inaelekea Mkuranga Polisi tutoe taarifa.

“Lakini ile gari ikaelekea njia ya Dar es Salaam, ikatuacha nasi tukafuatilia hadi Mwanambaya, tulikuwa makini maana hatukujua ni watu wa aina gani,” alisema.

Ilipofika Kisemvule, shuhuda huyo anasema waliona mtu akishuka kwenye gari hilo, wakalipita na kwenda kusimama mbele.

“Baadaye tukaamua tusubiri litupite, hadi Vikindu, kuna kituo cha Polisi tuone kama wataingia pale, lakini hawakuingia.”

Tukaenda hadi kituo cha ukaguzi Mwandege, ghafla pikipiki yetu ikapata pancha tairi la mbele.”

“Tukashuka na kuelekea kituo cha ukaguzi, wakati tunaelekea tukamwona askari kando ya barabara, mmoja wetu akatoa taarifa, lakini akaambiwa aje atoe taarifa kwenye kibanda.

“Tukamkuta askari kwenye kibanda, tukamwambia tunafukuzia gari, tuna wasiwasi nalo, limemchukua ndugu yetu. Akatuuliza tunaifahamu namba, tukamtajia lakini hakutusaidia na hivyo tukarudi kijijini tukatoa taarifa kwa mwenyekiti” alisema.

Mke wa Maliki

Akizungumza nyumbani kwake kijijini hapo, mke wa Maliki, Zainab Shabani alisema, alisikia sauti ya mumewe kwa mara ya mwisho Februari Mosi alipompigia simu.

“Naona wale watekaji walimpa nafasi ya mwisho kutoa taarifa, maana alipiga simu na nilipopokea akasema, nenda kachukue hela na simu dukani, wakati huo mi nilishachukua. Nilipotaka kuuliza alipo, simu ikakatika na mpaka leo haipatikani,” alisema.

Zainabu anasema mpaka sasa hajui hatima ya mumewe huku akishikwa na kigugumizi kuwaambia watoto wao wawili wanaosoma shule za bweni.

“Tumeoana 2005 tumezaa watoto watatu, wa kwanza ana miaka 15, wa pili miaka 13 na wa tatu miaka sita. Watoto wawili wapo shule ya bweni, hata sijawaambia, huyu mdogo yupo,” alisema Zainabu ambaye pia ni mjamzito.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi