Kimataifa
Vijana wadaiwa kupewa makahaba kutimiza mila
Kenya. Imeelezwa kuwa miongoni mwa sababu za kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kingono kwa wavulana nchini hapa ni tabia za kuwapa vijana wanawake makahaba ili kutimiza sharti la kimila waonekane wametakaswa.
Hayo yameelezwa na Naibu Kamishna wa Thika nchini Kenya, Mbogo Mathioya wakati wa kufungua kituo kipya cha kuhifadhi wasichana na wavulana waliokutana masaibu hayo eneo la Section 9 mjini Thika Februari 11, 2023.
Mathioya amesema vijana wanaotoka jandoni wamejikuta kwenye mtego wa unyanyasaji wa kingono baada ya kufanyiwa tohara.
“Tumegundua ya kwamba wavulana baada ya kutoka jandoni hutafutiwa makahaba ili kufanya nao ngono kwa kile kinachoelezwa ni kutakaswa ili wajihisi wakamilifu kwa kuondoa maovu mwilini,” amefafanua Mathioya.
Amesema tayari Serikali imeanzisha uchunguzi ili kubaini tabia hiyo kwa madai ya kutimiza matakwa ya mila.
Kiongozi huyo amewata wazazi kuchukua hatua dhidi ya tabia hiyo wanayofanyiwa wavulana baada ya wana wao kupitia jandoni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Magharibi, Alfred Wanyoike amesema vijana wengi wanaofanyiwa vitendo hivyo ni kutoka katika vijijini
“Wazazi wengi hawafuatilii mambo yanayofanywa na watoto wa shuleni. Ni vyema wazazi kuwa macho ili kuelewa tabia zao,” amefafanua kiongozi huyo.
Amewalaumu baadhi ya walezi wa vijana hao wavulana wanaowapeleka kwa makahaba baada ya kutoka jandoni.
“Tabia hiyo ni hatari kwa sababu yaweza kuhatarisha maisha ya vijana hao kiafya kutokana na kuambukizwa magonjwa kama Ukimwi na hata kisonono,” akasema Wanyoike.
Akizungumza awali, Mkurugenzi wa Shirika la Girl Child Network nchini Kenya, Mercy Musomo ametoa wito kwa wasichana na wavulana wanaokutana na vitendo vya unyanyasaji wa aina hiyo kutoa taarifa kwenye kituo hicho kipya.
“Vijana wengi siku hizi wanatumiwa vibaya kusafirisha dawa za kulevya katika sehemu tofauti, jambo linalosababisha wao kunaswa na mtego, huku wengine wakinyanyaswa kingono,” amefafanua Musomo.
Amesema hata wanafunzi wengi hasa walio kwenye shule za bweni wamejikuta katika tabia za kulawitiana.