Connect with us

Kitaifa

TCRA kuzima laini za simu zisizohakikiwa leo

Dar es Salaam. Wakati laini za simu ambazo hazijahakikiwa zikizimwa leo Jumatatu Februari 13, 2023 na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), asilimia 96.8 ya laini zote za simu zilizosajiliwa kwa alama ya vidole zimehakikiwa.

Hiyo ni kwa mujibu wa TCRA walipozungumza na Mwananchi huku wakieleza, hadi Februari 5, 2023, laini za simu 58.691 milioni zilikuwa zimehakikiwa kati ya laini milioni 60.620.

Hiyo ikiwa na maana kuwa, idadi ya laini ambazo zilikuwa hazijahakikiwa zimepungua kutoka zaidi ya milioni mbili kwa mujibu wa TCRA zilizokuwapo Januari 19, 2023 hadi 1.92 milioni Februari 5.

Takwimu hizo zinatolewa ikiwa ni baada ya Serikali kuongeza siku 14 mbele ili kutoa ruhusa kwa ambao walikuwa hawajahakiki laini zao ikiwa ni baada ya ukomo wa awali kuwa Januari 31, 2023.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Semu Mwakyanjala ambaye ni Ofisa Mwandamizi Mkuu Mawasiliano wa TCRA amesema usajili wa kutumia alama za vidole haukushindwa kudhibiti udanganyifu wa mtandao ila kinachofanyika sasa ni maboresho zaidi.

“Hadi Februari 5 laini za simu 58.691 milioni zilikuwa zimehakikiwa kati ya laini milioni 60.620 ambayo ni sawa na asilimia 96.8 Februari 5 mwaka huu, na kwa siku za hapo nyuma hadi leo (jana) idadi ya waliohakiki itakuwa imeongezeka,” amesema Mwakyanjala.

Amesema kusajili laini kwa alama ya vidole ilikuwa kama njia ya kufungua vingi huku akieleza kinachofanyika sasa ni sawa na aliyenunua baskeli akaitumia kwa miezi mitatu na kuamua kuifanyia maboresho.

“Ukiamua kukagua nati gani imetoka kwenye baskeli siyo kwamba haifanyi kazi ila unataka uiendelee kuwa bora, ndiyo kinachofanyika,” amesema Mwakyanjala.

Kuhusu laini ambazo zitafungiwa kama upo uwezekano wa watumiaji kuzirejesha (renew) alisema taarifa kamili itatolewa baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo.

Siku chache nyuma akitoa maelezo mbele ya waandishi wa habari, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema lengo la uhakiki ni kuendelea kudhibiti utapeli unaofanywa kwa njia ya simu.

“Kumekuwa na utapeli mwingi kwa kutumia laini za simu, hatua ya awali ilikuwa ni usajili kwa alama za vidole na kila laini iliyokuwa imelengwa kusajiliwa ilisajiliwa,” amesema Nape na kuongeza.

“Baadaye kampeni ya pamoja ya kuhakiki ilianzishwa na ilikubaliwa kuwa ambazo hazijahakikiwa zifungwe na 31 ilikuwa mwisho lakini tumeona tuongeze siku hadi Februari 13 mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti ya TCRA ya robo ya nne ya mwaka, hadi Desemba 2022 mitandao ya simu ilikuwa imesajili jumla ya laini milioni 60.277.

Laini hizo ni sawa na ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na zile milioni 58.1 waliokuwapo mwisho war obo ya tatu ya mwaka 2022 yaani Septemba.

Kati ya laini hizo, Vodacom ilikuwa na jumla ya laini milioni 18.18, Airtel 16.61 milioni, Tigo milioni 15.94, Halotel milioni 8.02 na TTCL ikiwa na laini 1.49 milioni huku Smile wakiwa na laini15,547.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi