Connect with us

Kitaifa

Rais Samia awaongeza ‘boom’ wanafunzi vyuo vikuu

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la viongozi wa Shirikisho la Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso) la kutaka kuongezewa fedha za kujikimu kutoka Sh8,500 kwa siku hadi Sh10,000.

 Hata hivyo, amesema ombi la Tahliso la kuwapatia mikopo wanafunzi wa ngazi ya cheti na stashahada halitawezekana kwa sasa, hata hivyo watakwenda kuliwekea mipango ya kulitekeleza siku zijazo.

Leo Jumamosi, Februari 11, 2023 Ikulu jijini Dodoma, Rais Samia amekutana na viongozi wa Tahliso na Zahlife kwa upande wa Zanzibar ambapo amewapa nafasi ya kuuliza maswali na kuzungumza nao kuhusu mambo mbalimbali yanayowahusu.

Katika mkutano huo, Rais wa Tahliso, Frank Nkinda amewasilisha maombi yao kwa Rais Samia ili aweze kuwasaidia wanafunzi hapa nchini kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.

Moja ya maombi yaliyowasilishwa na Nkinda ni pamoja na kuongezewa kiasi cha fedha za kujikimu kinachotolewa na serikali kwa wanafunzi kwa siku kutoka Sh8,500 za sasa hadi kufikia Sh10,000 kwa sababu maisha yamepanda.

“Kwa sasa tunapata 8500 kwa siku kama fedha ya kujikimu lakini Mheshimiwa Rais hali ya maisha imepanda kwa sasa haiendani na kiasi tunachopata. Tunakuomba kiasi hiki kipande angalau kiwe Sh10,000 au kiasi kitakachokupendeza,” amesema Nkinda.

Vilevile, Nkinda amesema kwa sheria za sasa wanafunzi wanaosoma masomo ya ngazi ya cheti na stashahada siyo wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu, hivyo alimwomba Rais Samia kuwasaidia nao ili wanufaike na mikopo hiyo.

“Tunakuomba sana, ikikupendeza Mheshimiwa Rais, kadri utakavyoona inafaa, kwa mwaka mpya wa fedha wa 2023/24, utusaidie wanafunzi hawa wa ngazi ya cheti na diploma nao wawe wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu,” amesema kiongozi huyo wa Tahliso.

Mbali na maombi hayo, Nkinda pia katika hotuba yake, amemwomba Rais Samia wapate ofisi itakayowawezesha kuendesha shughuli zao za kila siku. Pia, ameomba wapata gari litakalowasaidia katika shughuli zao za kila siku.

Akijibu hoja za viongozi hao wa serikali za wanafunzi wa vyuo, Rais Samia ameridhia ombi lao na kuwaongezea fedha za kujikimu hadi Sh10,000 kwa siku ili kuwawezesha kumudu maisha ya kila siku wawapo vyuoni.

“Waziri wa Elimu, nenda kaangalie, tutaanza na Sh10,000,” amesema Rais Samia, kauli ambayo iliibua shangwe kwa viongozi hao ambao walianza kuimba “tuna imani na Samia” huku wakipiga makofi. Hata hivyo, Rais Samia hakueleza ni lini itaanza kutekelezwa.

Kuhusu wanafunzi wa ngazi ya cheti na stashahada kupata mikopo hiyo, Rais Samia amesema jambo hilo halitawezekana kwa sasa, wanakwenda kujipanga na kuweka mipango ya kulitekeleza siku zijazo.

“Kwa kazi tunazozifanya sasa hivi na hali ya bajeti, hili bado hatujafikia huko, kwa hiyo tunalifikiria, tunaliweka kwenye mipango yetu.

“Nilikuwa nanong’ona na Waziri (wa elimu) hapa, nikamwambia nenda kajipekue vizuri, ukiwa unaliweza niambie, nami nipekue kwingine kidogo nikujazie ili uweze…kama tutashindwa mwaka huu, tuachieni tujipange mbele tutakwenda nalo,” amesema Rais Samia.

Kuhusu suala la Tahliso kusaidiwa ofisi, Rais Samia ametoa maelekezo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kwamba wizara yake ikihamia mji wa serikali wa Mtumba, basi majengo wanayoyatumia sasa wawaachie Tahliso.

Ameongeza anakwenda kuangalia uwezekano wa kutoa samani na vifaa vingine vya ofisini kwa Tahliso na Zahlife ili viwasaidie katika kuendesha shughuli zao za kila siku katika taasisi hizo.

Awali, Profesa Mkenda alisema wakati Rais Samia anaingia madarakani, mikopo iliyokuwa inatolewa ilikuwa Sh464 bilioni lakini aliagiza iongewe hadi Sh570 na baadaye tena ikafikisha Sh654 bilioni.

Waziri Mkenda amesema Rais Samia alielekeza Wizara ya Elimu kutoa ufadhili wa masomo ya sayansi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri. Alisema hadi sasa wanafunzi 640 wamepata ufadhili huo wa masomo nchini humo.

“Kuna scholarship zimetolewa pia kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu. Wakati wa kujadili mradi wa HIT, uliagiza kujenga uwezo wa wahadhiri kwa kusomesha wahadhiri wengi zaidi. Fedha zimetengwa kwa ajili ya wahadhiri kwenda kusoma popote duniani, tuna Dola 1 milioni,” amesema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi